30.4 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Imani huzaa imani

 WAANDISHI WETU– DAR/MIKOANI

IMANI huzaa imani. Ndilo neno sahihi ambalo unaweza kusema, baada ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli kuwaomba kuwasisitiza wananchi kuwa anataka tochi ya maendeleo iendelee kuwaka kama alivyoanza.

Dk. Magufuli ambaye alianza kampeni Agosti 29, mwaka huu hadi sasa amefanya mikutano mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza, alisema wananchi wakiamuani atafanya mambo makubwa zaidi.

Mara zote katika mikutano hiyo, amekuwa akiwaeleza Watanzania bado ana deni kubwa la kuwatumikia na wameshapanga mikakati mingi ya kufanya ambayo ipo katika ilani ya uchaguzi na kuwaomba wamwamini aweze kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

“Hatuombi kura kwa sababu ya madaraka, hatuombi kwa sababu tunataka sifa, tunaomba kwa sababu tunaamini tutawafanyia kazi. Tuna upendo na jukumu la kuiletea maendeleo nchi yetu.

“Unaweza ukakosea kupata mke, kupata mume lakini ukikosea uchaguzi madhara yake ni makubwa. Mchagueni rais wa CCM, wabunge wa CCM, kachagueni madiwani wa CCM, nitakuwa mwaminifu kwenu, sitajikweza…nataka tochi ya maendeleo iendelee kuwaka kama tulivyoanza,” alisema Dk. Magufuli.

Katika mikutano ya kampeni, Dk. Magufuli amekuwa akisisitiza kuboresha huduma za afya, elimu, maji, umeme, ujenzi wa stendi, masoko, utatuzi kero za wakulima na wafanyabiashara, usafiri wa nchi kavu, majini na anga, masilahi ya wafanyakazi na kuongeza fursa za ajira.

Alisema mambo yaliyofanyika miaka mitano iliyopita yalikuwa rasharasha na kwamba mvua yenyewe inakuja.

MAELFU WAMSIMAMISHA

Jana akiwa njiani kuelekea jijini Mwanza akitokea mkoani Mara, Dk. Magufuli alisimama na kuzungumza na wananchi maeneo ya Nyamikoma, Mtangakuona na Nyashimo yaliyopo Jimbo la Busega mkoani Simiyu pamoja na Kihangara, Magu, Nyanguge, Igoma, Nyakato, Buzuluga na Mabatini jijini Mwanza.

Maelfu ya wananchi walikuwa wamejipanga pembezoni mwa barabara hatua iliyosababisha Dk. Magufuli kusimama kwenye gari na kuzungumza nao huku akiwapa nafasi wagombea ubunge na udiwani kuomba kura.

“Yaani kuanzia Kisesa watu wamejaa kote kwakweli leo (jana) ni kazi, nitafika saa ngapi Mwanza ndugu zangu kwa sababu kesho (leo) tuna mkutano,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema anataka jiji hilo liwe la mfano ambapo aliahidi kuunda wilaya nyingine ili liwe na wilaya tatu na kusisitiza wananchi wanaoishi milimani hawataondolewa.

“Wananchi wanaoishi milimani wataendelea kukaa huko na hakuna yeyote atakayetolewa, awe wa chama chochote maendeleo hayana chama tuchagueni yale mambo yaliyobaki tutayabeba.

“Tuna mipango mikubwa ya kusaidia vijana ikiwemo kufufua viwanda vitakavyoongeza fursa za ajira,” alisema.

Akiwa eneo la Igoma, Dk. Magufuli alisema changamoto ya maji imeshaanza kufanyiwa kazi na kwamba tayari mkandarasi ameshasaini mkataba.

Akiwa Nyamikoma, Dk. Magufuli aliahidi kuchangia ujenzi wa Shule ya Msingi Nyamikoma.

“Jimbo la Busega limekuwa likifanya kazi nzuri, mlituamini katika kipindi cha miaka mitano tunaomba mtuamini tena miaka mitano mingine.

“Tumejenga vituo vya afya, tumejenga hospitali tunataka haya tuyaendeleze. Suala la maji tuna mradi mkubwa wa kuyafikisha hapa yatakwenda mpaka Bariadi, Maswa…ninaomba muamini tuko tayari kutimiza ahadi zetu tulizopanga,” alisema.

Dk. Magufuli pia alisema atampatia kazi mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni, bado ni kijana na ana nguvu.

“Sisi tuna taratibu zetu huwa tuna vipindi vya kufanya kazi, Chegeni amefanya kazi yake vizuri kwa miaka 10, nitamtafutia mahala pengine pa kufanya kazi bado ni kijana ana nguvu…kwa sasa mnichagulie Simon Sonde (mgombea ubunge),” alisema Dk. Magufuli.

Akiwa eneo hilo, alimtaka mgombea udiwani awaombe radhi wananchi na atakapochaguliwa akashirikiane nao.

“Uchaguzi CCM tumemaliza wala hatutabadilisha katika kampeni kila mmoja alikuwa na mgombea wake, hamchagui sura, tunachagua mtu lakini pia chama.

“Magoti (mgombea udiwani) aliwakosea nini, panda kwenye gari waombe msamaha wananchi wako. Siku utakapochaguliwa uje ufanye mkutano hapa, ni lazima uwe mnyenyekevu kwa hawa (wananchi),” alisema Dk. Magufuli.

Akiwa eneo la Matangakuona, alisema tatizo kubwa ni maji na kwamba tayari kuna mpango wa kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza maeneo yote jirani.

“Nchi nzima maeneo yote ya kandokando ya ziwa tayari kuna miradi, tulianza kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza Igunga, Nzega na Tabora. Tulianzia mbali ili hapa karibu tuje tumalizie, yale tuliyoyafanya 2015 ilikuwa ni rasharasha mvua yenyewe inakuja,” alisema Dk. Magufuli.

Pia wananchi wa Nyanguge walimuomba Dk. Magufuli kuwasaidia ujenzi wa stendi na soko la kisasa kwani tayari eneo lipo.

WAGOMBEA UBUNGE

Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula, alimshukuru Dk. Magufuli kwa kuwezesha wakazi wanaoishi milimani kupewa leseni za makazi na hati.

Mgombea wa ubunge wa Ilemela, Angelina Mabula, alishukuru kwa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa stendi ya maroli iliyotoa ajira zaidi ya 200, uwanja wa ndege, zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya na kuahidi kuwa watamlipa Dk. Magufuli kwa kuhakikisha anashinda kwa kishindo.

Mgombea ubunge jimbo la Busega, Simon Sonde alisema kuna mafanikio makubwa katika sekta za elimu na afya kutokana na uwezeshaji uliofanywa na Serikali miaka mitano iliyopita.

Alisema zilitolewa Sh bilioni 4.9 kwa ajili ya elimu bure, Sh milioni 238 ujenzi wa Shule ya Msingi Fogofogo, Sh milioni 99 (Shule ya Sekondari Kabita), Sh milioni 30 (wodi ya wazazi) na Sh milioni 25 (jengo la huduma za ushauri nasaha).

“Zamani wananchi walikuwa wanakwenda Mwanza, Magu kupata huduma ya afya, kwa uongozi wako umetupatia Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali, nawaombeni wananchi mnipe kura za kutosha mimi, mheshimiwa rais na diwani ili tukasimamie yote yaliyoko kwenye ilani,” alisema Sonde.

Mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Raphael Chegeni, alisema; “Awamu yako hii ya tano umefanya mambo makubwa sana, wananchi wa Nyamikoma kwa sasa hivi wanasubiri wakuenzi kwa kukupa kura nyingi Oktoba 28. Uliyoyafanya Busega ni historia.

ACT

Katika hatua nyingine, Chama cha ACT Wazalendo kimeiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kuwarejesha wagombea wake wote walioenguliwa Bara na Zanzibar.

Kimesema kuwarudisha wagombea hao kutasaidia kurejesha amani, na haki ya msingi yao ya kikatiba.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema jitihada zozote za kuporwa haki na ushindi wao zitakutana na nguvu kubwa ya umma.

“Tume iwarejeshe wagombea wetu wote, Bara na Zanzibar waliongeliwa, hatutakubali hata mgombea wetu mmoja kuenguliwa.

“Dhamana ya amani ya taifa ipo mikononi mwa tume kwa kuzingatia hoja tulizozianisha hapo juu, inapaswa kuwarejesha wagombea wetu wote,” alisema Zitto.

Alilitaka jeshi la polisi kuzingatia amani ni tunda la haki, huku akimtaka mkuu wake, IGP Simon Sirro kugusia juu ya wasimamizi wa uchaguzi.

LISSU

Kwa upande wake mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeoleo (Chadema), ameahidi kuboresha mazingira ya wafanyakazi endapo chama kitachaguliwa kushika dola

Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye uwanja wa Sabasaba Mikondani mkoani Mtwara jana, Lissu atahakikisha wafanyakazi wanafanyakazi katika mazingira huru na haki na kuhakikisha anawapa wanapata stahiki zao, ikiwemo nyongeza ya mishahara.

 Alisema endapo wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima na watumishi wakiwa huru wanaweza kufanyakazi kwa bidii na kuongeza ajira.

“Watanzania wote wapate haki zao za msingi kwenye kilimo ili wauze mazao yao kwa uhuru, watumishi pia wapate haki ikiwemo nyongeza za mishahara ili kuboresha maisha yao ili kuwe na mfumo huru ambao utaondoa ukandamizaji.

“Uhuru tunaoutaka uambatane na haki kwa wafanyakazi wapate nyongeza za mishahara kwa mujibu wa sheria za nchi zinavyosema, ikiwemo kupandisha madaraja kwa waanaostahili hatutanyang’anya haki ya mtu.

“Chadema ikiingia madarakani tutahakikisha maeneo yote yanayopatikana rasilimali za nchi yanaanza kunufaika yenyewe kwanza, kisha kwenda maeneo mengine hii itasaidia maeneo hayo kupata manufaa kimaendeleo,”alisema.

Alisema atahakikisha hakikisha kila mwananchi anapata haki ya kutumia gesi nyumbani

Taarifa hii, imeandaliwa na Faraja Masinde (Dar), Nora Damian (Mwanza) na Florence Sanawa (Mtwara)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles