MADRID, HISPANIA
BEKI wa kati wa timu ya Real Madrid, Sergio Ramos, amempigia magoti nahodha wa Barcelona, Lionel Messi aweze kubaki katika kikosi chake.
Messi ameleta mtikisiko ndani ya klabu hiyo baada ya kutangaza kuwa anataka kuondoka ndani ya viwanja vya Camp Nou wakati huu wa kiangazi.
Jumatano wiki hii baba wa Messi, Jorge Messi, ambaye ndiye wakala, aliweka wazi kwamba itakuwa ngumu kwa kijana wake kuendelea kuwa mchezaji wa Barcelona kwa sasa.
Messi anahusishwa kutaka kutua katika klabu ya Manchester City ambayo inafundishwa na kocha wake wa zamani Pep Guardiola, lakini Ramos amedai ni bora mchezaji huyo aendelee kuwa hapo kwa ajili ya manufaa ya soka la Hispania na ushindani wa Barcelona na Real Madrid.
“Hatutakiwi kumshawishi mchezaji kubaki au kuondoka, lakini mwenyewe anajua yapi maamuzi sahihi kwa upande wake, lakini naweza kusema kwamba kwa soka la Hispania na kwa Barcelona na wote kwa ujumla tunahitaji aendelee kuwa nasi,” alisema Ramos.
Kwa upande wake Ramos mwenye umri wa miaka 34, anaingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake na klabu ya Real Madrid, lakini ameweka wazi kuwa, hana wasiwasi na hatima yake na anaamini atafikia makubaliano na uongozi wa timu hiyo.
“Hadi sasa bado hatujaanza kuzungumzia hatima yangu, lakini ninaamini kila kitu kitakuwa sawa kwa kuwa nimekuwa hapa kwa miaka mingi, jambo ambalo ninaliangalia kwa sasa ni kuona jinsi gani nitaendekea kuwa kwenye ubora wa hali ya juu mara msimu mpya utakapoanza,” aliongeza mchezaji huyo.
Msimu uliomalizika mchezaji huyo alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu akiisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania.