FARAJA MASINDE – DAR ES SALAAM
SASA ni rasmi. Mhariri wa Magazeti ya Mtanzania na Rai yanayochapishwa na NewHabari (2006) Ltd, Bakari Kimwanga amechukua fomu ya kuwania udiwani wa Kata ya Makurumla katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, Mwaka huu.
Kimwanga aliyeteuliwa kuwania nafasi hiyo na Chama Cha Mapinduzi(CCM) alichukua fomu hiyo leo katika ofisi za Kata ya Makurumla zilizoko Magomeni Mwembe Chai Jijini Dar es Salaam.
Mapema leo, Kimwanga alifika katika Ofisi za Kata ya Makurumla saa 8:30 mchana akisindikizwa na wafuasi wa chama hicho kwa nderemo na vifijo, alikabidhiwa fomu hiyo na Mtendaji wa Kata hiyo, Willieth Muganila.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, mgombea huyo mteule amekishukuru chama chake cha CCM kwa kumuamini kupeperusha bendera katika Kata hiyo na kuongeza kuwa anazifahamu changamoto za kata hiyo.
“Awali ya yote nakishukuru chama changu kwa kuniteua kuwania nafasi hii ya kupeperusha bendera katika katika ngazi ya udiwani pia nawashulkiru viongozi wangu wa Kamati ya siasa Kata ya Makurumla.
” Sisi tunajua na ndani ya CCM tunamiongozo, shida za Wananchi wa Kata ya Makurumla tunazifahamu, hivyo leo nimechukua fomu na nitakwenda kuijaza na kuirejesha kama utaratibu wa NEC(Tume ya Taifa ya Uchaguzi) unavyotaka, mengi zaidi nitaeleza wakati wa kurejesha fomu,” amesema Kimwanga.