25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

TRA: Kulipa kodi si lazima uwe mfanyabiashara

KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa kulipa kodi si lazima mtu awe mfanyabiashara na kwamba analipa kodi kutokana na bidhaa alizonunua na kudai risiti.

Hayo yalizungumzwa juzi jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo wakati wa mahafali ya pili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao ni wanachama wa klabu za Kodi (UDTA) zilizo chini ya mamlaka hiyo.

Alisema kila pato analopata mtu anatakiwa kulilipia kodi kwa mujibu wa sheria na kwamba ili kujiridhisha kodi imefika serikalini baada ya kufanya manunuzi ya bidhaa mtu anatakiwa kudai risiti.

Alisema lengo la kuanzisha klabu za kodi mashuleni na vyuo vikuu ni kuwezesha vijana kuwa na elimu ya kodi na kutambua umuhimu wake ambao utawafanya kuwa walipakodi wazuri wa baadae.

“Bila kulipa kodi tusingekuwa na barabara nchi nzima na kwamba miaka ya nyuma ili uweze kuifikia Bukoba ilikuwa lazima upite katika nchi mbili za Kenya na Uganda ndipo ufike Bukoba lakini hivi sasa tuna barabara nzuri zinazotuwezesha kwenda moja kwa moja bila kupita nchi za wenzetu”, alisema Kayombo.

Alisema vijana wote waliojiunga na klabu za kodi wapo katika njia sahihi kutokana na kuwa kodi ni moja ya sababu itakayoiwezesha Tanzania kuwa kama nchi za Ulaya zilizoendelea.

Alisema ili nchi iendelee kupata mafanikio Zaidi ya haya yaliyopo sasa ni lazima TRA ikusanye mapato na kwamba ili mapato yakusanywe mamlaka inatakiwa kutoa elimu ya kodi kwa kila mwananchi na sio kuwalazimisha kulipa kodi pasipokuwa na uelewa wa umuhimu wake.

“Kulipa kodi sio kwamba mfanyabiashara anaonewa ila analipa kwa mujibu wa sheria na kwa upande wa TRA kazi yake ni kuhakikisha mfanyabiashara biashara yake inaimarika kwa kumjengea uelewa wa umuhimu wa kodi, kumuwekea mazingira mazuri ya kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho endelevu ya takayowezesha kutatua changamoto za walipakodi wake”, alisema Kayombo.

Alisema ili klabu hizo ziweze kuendelea na kupeleka elimu ya kodi katika maeneo mbalimbali ambako wanachama hao wa klabu za kodi  wanakoishi, TRA itakuwa ikiwapa elimu za mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vituo vya kazi vya mamlaka hiyo ili wajifunze kwa vitendo.

Naye rais wa UDTA, Wiseman Lucas alisema kuwa uwepo wa klabu hizo za kodi mashuleni na vyuo vikuu kutawezesha vijana kukuwa wakiwa na uelewa wa umuhimu wa kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kuifanya elimu hiyo kumfikia kila mwananchi alieko jirani naye kutokana na kuwa kila mwanachama wa klabu ni balozi ambaye anatakiwa kuipeleka elimu hiyo katika maeneo anayoishi.

Alisema katika matawi 12 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, matawi matano tayari yana wanachama wa klabu za kodi na kwamba lengo lao matawi yote yawe na wanachama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles