29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 20 wapata ujauzito likizo ya corona

Na JANETH MUSHI-LONGIDO

 WANAFUNZI wa kike zaidi ya 20 wa shule za msingi na sekondari wilayani Longido mkoani Arusha, wamepewa ujauzito na wengine kuolewa wakati wa kipindi cha likizo kutokana na ugonjwa wa corona, baada ya shule kufungwa.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imesema itawachukua hatua za kisheria baadhi ya wazazi na walezi wanaoozesha watoto wao kike na kuwakatisha masomo,huku wengine wakiwalazimisha watoto kuharibu ushahidi pindi mashauri hayo yanapofikishwa katika vyombo vya sheria.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Longido,Frank Mwaisumbe wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Engikareti,baada ya uzinduzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Embalwa, yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na wadau wa elimu.

Alisema wakati wa likizo, baada ya ugonjwa wa corona kuingia hapa nchini,shule zilipofunguliwa zaidi ya wanafunzi 20 walishindwa kuendelea na shule baada ya kubainika kuwa wamepata ujauzito.

Alisema Serikali haitaendelea kuvumulia baadhi ya wazazi na walezi wanapolazimisha na kuwahamasisha watoto wao wa kike kuolewa kabla ya wakati na kuwakatisha masomo na kuwa watashirikiana na jamii katijka kupinga hilo ikiwemo viongozi wa mila.

“Kipindi hiki cha corona ambapo shule zilifungwa kwa miezi kadhaa tumepata watoto zaidi ya 20 waliopata ujauzito,sasa hili ni janga kwetu sisi kwani pamoja na maendeleo na kasi kubwa tunayoenda nayo ya kielimu katika mkoa,linaturudisha nyuma na  kiasi kikubwa.

“Tunarudishwa nyuma na baadhi ya  walezi na wazazi wa watoto kwa kutokutoa ushirikiano unaotakiwa, tunapohitaji ushahidi wazazi mnawatishia watoto wenu mnawaambia wakimtaja waliyempa mimba hamtakuwa na ushirikiano naye na mnamfukuza  katika koo zenu, jambo hili tumelivumilia kwa muda mrefu.

“Hatuwezi kuvumilia haiwezekani mzazi mtoto amerudi likizo,wewe unamwambia shule imeinapokea mahari unachukua ng’ombe au mbuzi halafu yule mtu anamuoa yule mtoto na mzazi unakuja shuleni unasema mtoto amepotea,unadai alikuwa anakuja shule wewe mwenyewe hujui alipo,”alisema.

Mmoja wa wadau walioshiriki ujenzi wa madarasa hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la MPDI,Mohamed Ninde,alisema shirika hilo ambalo linatoa huduma mbalimbali kwa jamii ya kifugaji imeamua kushirikiana na serikali kuboresha sekta ya elimu.

Alisema uwepo wa madarasa hayo utasaidia kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu wanayokumbana nayo wanafunzi wengi wilayani humo huku ikihatarisha usalama wao kufuatia uwepo wa wanyamapori katika baadhi ya njia.

“Tumeangalia watoto wanatembea umbali mrefu kwenda shule,tukaona mazingira ni magumu na baada ya kuona jamii wana moyo tukasema tuwaunge mkono.

“Mwamko wa elimu kwa kiwango kikubwa katika jamii unazidi kuongezeka kwani wametambua umuhimu wa kusomesha watoto wao,”alisema.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Longido,Dk.Juma Mhina alisema licha ya changamoto mbalimbali za elimu,wilaya hiyo imeendelea kufanya vizuri katika elimu kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa, hali iliyochangiwa na mwamko chanya wa jamii juu ya umuhimu wa elimu.

Alisema katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, wameongoza na kushika nafasi ya kwanza kimkoa huku matokeo ya drasa la nne kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo wakiwa wa pili kitaifa na kufanikiwa kuingia katika tano bora kitaifa kwa matokeo ya  kidato cha pili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles