24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa: Uongozi uliojaa maarifa kujiamini na misimamo thabiti

Na Profesa Kitila Mkumbo-DAR ES SALAAM 

Tarehe 16 Februari 1999 aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, alitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuzungumza na jumuiya ya wanafunzi na wafanyakazi. Wakati huo mimi nilikuwa Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa chuo hicho, maarufu kama DARUSO (Dar es Salaam University Students’ Organisation). Kabla ya ujio wa Rais Mkapa, uongozi wa chuo uliniita na kuniagiza wapate orodha ya maswali kutoka kwa wanafunzi ambao wangependa kumuuliza Rais Mkapa ili waweze kuyachambua na kuyachuja. Nilikataa. Badala yake nikashauri kuwa wanafunzi na wafanyakazi wawe huru kuuliza maswali, nikisisitiza kuwa kwa umahiri aliokuwa nao wa kujieleza hakuna swali ambalo Rais Mkapa angeshindwa kulijibu. Hatukuelewana hadi Rais Mkapa alipoingia chuoni mchana na mimi sikupeleka orodha ya maswali.

Mara Rais Mkapa alipofika chuoni, na baada ya kusaini kitabu cha wageni ofisini kwa Makamu Mkuu wa Chuo, alienda katika Ukumbi wa Baraza la Chuo (Council Chamber). Huko nami nilikuwemo kama mwakilishi wa wanafunzi. Katika mazungumzo yetu na Rais Mkapa Makamu Mkuu wa Chuo, wakati huo akiwa ni Prof. Mathew Luhanga, akatoa ratiba fupi ya matukio katika Ukumbi wa Nkrumah. Nilipopata nafasi ya kuzungumza nikatoa maoni yangu kuwa Rais akishamaliza kuhutubia yeye mwenyewe awe mwenyekiti na aruhusu maswali kadri atakavyoona inafaa na hadi atakapoona inatosha. Nikaeleza kuwa hii itaondoa dhana ya kwamba kuna watu wamepangwa kuuliza maswali. Rais Mkapa alikubali na kusema “good idea”! 

Tulipofika Ukumbi wa Nkrumah Rais Mkapa alitoa hotuba kali sana kwa lugha ya Kiingereza. Wakati huo ilikuwa lazima uzungumze kwa Kiingereza katika Ukumbi wa Nkrumah, vinginevyo ungezomewa sana! Katika hotuba yake Rais Mkapa alieleza kwa kirefu dira yake na akaweka wazi kwamba kipaumbele chake kitakuwa ni uchumi. Msimamo huu haukupokelewa vizuri sana na Jumuiya ya chuo kwa kuwa wakati huo kulikuwa na matatizo makubwa kabisa ya elimu; tulitarajia angeeleza mipango yake katika eneo hili. Lakini hata wakati wa kujibu maswali Rais Mkapa aliweka wazi msimamo wake kuwa alikuwa amesimamisha ajira za walimu chuo kikuu ili ajenge kwanza uchumi! 

Ulipofika wakati wa maswali, ninakumbuka mtu wa kwanza kuuliza swali alikuwa Dkt. Francis Michael, ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Wakati huo Francis alikuwa Makamu wa Rais wa DARUSO. Pamoja na kwamba Francis alikuwa moja ya wanafunzi mahiri sana kwa lugha ya Kiingereza aliomba aulize swali lake kwa Lugha ya Kiswahili. Swali lake lilihusu uamuzi wa serikali kuongeza umri wa kustaafu wakati kuna vijana wengi waliomaliza shule na hawakuwa na ajira. Francis alieleza pia kuwa fedha ambazo zingetumika kulipa mishahara ya waliongezewa muda wa kustaafu zingeweza kusaidia kujenga madarasa mengi ya shule za msingi na sekondari. 

Katika jibu lake, Rais Mkapa alionesha mshangao kidogo kuhusu swali hilo. Akasema yeye alipokuwa anakuja chuo kikuu alijiandaa akitarajia anakuja kujadiliana na wasomi wenzake. Akaongeza kuwa alitarajia muuliza swali aonesha ‘data’ za wahitimu ambao hawana ajira na jinsi ambavyo kutoongeza muda wa kustaafu kungesaidia kuokoa fedha za kujenga madarasa. Kwa maelezo hayo akawa amemaliza kujibu swali na akahitimisha kwa kusema: “no research, no right to speak”! Ukweli ni kwamba maswali yetu na majibu ya Rais Mkapa yalionesha wazi kwamba sisi wana jumuiya wa chuo kikuu tulipwaya sana kwa kuwa yeye alikuwa amejiandaa vizuri sana kuliko sisi.

Ziara ya Rais Mkapa katika Chuo Kikuu imebaki katika kumbukumbu zangu daima. Ziara hii, pamoja na maisha yake ya uongozi kwa ujumla, inatukumbusha mambo mawili muhimu kuhusu uongozi. Mosi, uongozi unahitaji maarifa. Hakuna shaka, kupitia hotuba zake na ushiriki wake katika midahalo mbalimbali, Rais Mkapa alionesha kuwa na maarifa mengi na hilo lilimsaidia sana kumjengea kujiamini na kuwa na misimamo thabiti katika uongozi wake. Pili, Rais Mkapa alikuwa haogopi kujadiliana na alikuwa haoni shida kuweka msimamo wake wazi bila kujali kama utaungwa mkono au la. 

Tunapoomboleza kifo na kusheherekea maisha ya Rais Mkapa, sisi ambao tumerithi nafasi za uongozi wa nchi yetu, na vijana wanaowania kuwa viongozi huko mbeleni, tukumbuke kusaka maarifa ili tuwe na msingi mzuri wa uongozi. Kupitia maarifa tutaweza kujiamini na kuwa  na misimamo thabiti kisera na kimatendo. 

Ninaungana na watanzania wengine kumpa pole Mama Anna Mkapa, familia na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa msiba huu mkubwa. Mungu aipumzishe Roho ya Marehemu mahala pema peponi. Amini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles