30.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

KATA FUNUA KURA ZA MAONI CCM

WAANDISHI WETU -DAR/MIKOANI

WAKATI mawaziri wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli wakifanya kufuru kwenye kura ya maoni ndani ya CCM, ambao baadhi wamepata ushindi wa zaidi ya asilimia 95, wenzao wawili wameungana na wabunge ambao wameshindwa kutetea nafasi zao na sasa wanasubiri neema za vikao vya juu.

Miongoni mwa mawaziri waliotetea majimbo yao kwa kishindo ni pamoja na Waziri wa Ardhi, William Lukuvi aliyepata kura 453 akiwapita wagombea wenzake sita aliopambana nao katika Jimbo la Isimani mkoani Iringa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo naye alifanikiwa kuibuka kidedea Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani, kwa kupata kura 588 kati ya 601 zilizopigwa.

Mwingine ni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye alipata kura 367 sawa na asilimia 97.6 Jimbo la Nzega Mjini, huku mpinzani wake wa karibu, Mashili akiambulia kura sita.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko naye aliibuka kidedea Jimbo la Bukombe kwa kupata kura 555 kati ya 569 zilizopigwa akiwaacha wenzake 11 wakigawana kura 14.

Jimbo la Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipata kura 845 huku mgombea wa pili akipata kura 3 na wa tatu kura 2.

Katika Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameibuka mshindi kwa kupata kura 1,138 kati ya 1,218 zilizopigwa huku zilizoharibika zilikuwa nne na halali 1,214.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu naye aliongoza kura za maoni Jimbo la Ilala, Dar es Salaam baada ya kupata kura 148 akifuatiwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema aliyepata kura 103.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga naye alishinda kwenye kura za maoni katika Jimbo la Vwawa mkoani Songwe, akipata kura 552 dhidi ya Erick Minga aliyepata kura 129 na Dismas Haonga ambaye alipata kura 9.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula naye ameongoza kwenye kura za maoni katika Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza kwa kupata kura 502 kati ya 685, akifuatiwa na Israel Mtambalike aliyepata kura 112.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel alipata ushindi mwembamba wa kura 148 dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliyepata kura 147.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba amefanikiwa kushinda kura za maoni Jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida kwa kura 27, akifuatiwa na Jumbe Katatla (14) na Naoel Kingu (6).

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa naye ameongoza Jimbo la Karagwe mkoani Kagera kwa kupata kura 587, huku wapinzani wake Vedasto Gotfrida akipata kura 7 na Joseph Kahama 48.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, ameshinda kwa kura  108 Jimbo la Kikwajuni, Unguja huku Hamid Yussuf akipata kura 6, Aboud Hassan Mwinyi 9 na Mansabu Haji Ramadhan 4.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni mara yake ya kwanza kugombea jimbo, alishinda kwa kishindo kwa kupata kura 405 huku aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Daniel Nsanzugwanko akiambulia kura 80.

MAWAZIRI WALIOSHINDWA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyekuwa Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, aliambulia kura 245, akiachwa na Ally Kinanasi aliyeibuka kidedea kwa kupata kura 493 akifuatiwa na Hunter Mwakifuna aliyepata kura 283. 

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliangushwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti katika Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni, Kitwanga alipata kura 260 huku Mnyeti akiongoza kwa kura 406.

Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii ambaye ni mbunge anayemaliza muda wake Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, Profesa Jumanne Maghembe, ameshindwa kwa kupata kura 130 dhidi ya mshindi wake, Anania Thadayo aliyepata kura 176. 

WALIOCHEZEA KAMARI NAFASI ZA UTEUZI

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye aliacha nafasi hiyo na kwenda kugombea Jimbo la Kigamboni, ni miongoni mwa walioshindwa akipata kura 122 huku aliyekuwa anatetea jimbo hilo, Dk. Faustine Ndugulile akiibuka kidedea akipata kura 190.

Mwingine aliyeacha uongozi na kwenda kugombea na kushindwa ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi ambaye aligombea Jimbo la Shinyanga Mjini  akiambulia kura 12 huku aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Stephen Masele akipata kura 152, akifuatiwa na Jonathan Ifunda aliyepata 65.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba naye aligombea Jimbo la Kawe na kushindwa akipata kura 3 huku mshindi Furaha Dominic akipata kura 101 akifuatiwa na Angela Kizigha aliyepata kura 85 na Askofu Josephat Gwajima akipata kura 79.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, David Kafulila ambaye aligombea Jimbo la Kigoma Kusini, aliambulia kura 64 huku Hasna Mwilima akiongoza kwa kura 273 akifuatiwa na Nashona Bidyanguze aliyepata kura 143 na January Kizito kura 117.

WALIOACHA UTEUZI NA KUSHINDA 

Walioacha nafasi zao na kushinda ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda ambaye aligombea Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro na kupata kura 285 akifuatiwa na Athony Mseke aliyepata kura 87 na Colman Kanje kura 31.

Mwingine aliyeshinda ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo akipata kura 172 huku Mwantum Mgonja akipara kura 73, Shamsa Mwangunga kura 9 na Tatu Mapunda kura 11. 

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti naye aligombea Jimbo la Misungwi na kushinda kwa kura 406 huku Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kitwanga akiambulia kura 260.

WABUNGE WALIOANGUSHWA

Mbunge wa Mufindi Kusini mkoani Iringa anayemaliza muda wake, Mendrad Kigola, aliangukia pua kwa kupata kura 8 kati ya 615 zilizopigwa.

Msimamizi wa uchaguzi, Sadiki Kaguo alimtangaza David Kihenzile kuwa mshindi kwa kupata kura 216 akifuatiwa na Dickson Litevele kura 162 na Josephat Mwagala kura 160.

Matokeo ya uchaguzi wa kura za maoni CCM katika Jimbo la Temeke, Abbas Mtemvu aliibuka kidedea kwa kupata kura 203 kati ya 367 huku tatu zikiwa zimeharibika huku mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake, Abdallah Mtolea akiambulia kura 22.

Mbunge wa Kinondoni aliyemaliza muda wake, Maulid Mtulia, naye alishindwa kutetea nafasi yake akipata kura 11 huku Abbas Tarimba akiongoza kwa kura 171 akifuatiwa na Iddi Azzan aliyepata kura 77.

Mbunge mwingine aliyeshindwa ni aliyekuwa Mbunge wa Momba, David Silinde kupitia Chadema kabla baadaye kuhamia CCM na kugombea kura hizo za maoni katika Jimbo la Tunduma ambako alipata kura 118 huku Aden Mwakyonde akiibuka mshindi kwa kura 250 na Daines Sichalwe kura 20. 

Aliyekuwa Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali kupitia Chadema na baadaye kujiunga CCM na kugombea nafasi hiyo kwenye kura za maoni za chama hicho tawala, naye alishindwa akiambulia kura 5 huku Abubakar Asenga akishinda kwa kura 368, Vitus Lupagila kura 54 akifuatiwa na Bhimji Rocky kura 22.

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia Chadema, Joshua Nassari ambaye alijiunga na CCM hivi karibuni, naye aliangukia pua katika kura za maoni katika jimbo hilo akishika nafasi ya nne akipata kura 26.

Aliyeibuka mshindi kwenye kura hizo za maoni ni Dk. John Pallagyo aliyepata kura 536 akifuatiwa na Dan Pallagyo kura 63.

MAWAZIRI WATATU WAANGUSHWA ZANZIBAR

Kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya CCM visiwani Zanzibar kimesababisha pia mawaziri watatu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wabunge wawili wanawake wa zamani kuanguka katika majimbo ya uchaguzi.

Miongoni mwa walioanguka ni Waziri wa Katiba na Sheria, Khamis Juma Maalim ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha kutafuta mwakilishi wa Jimbo la Pangawe huku kukiwa kumetokea sintofahamu katika kuhesabu kura.

Mwingine ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo ambaye aliangushwa kwa kupata kura 30 na kushindwa na mpinzani wake Suleiman Haroub Bape aliyepata kura 50.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango katika awamu ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Dk. Sada Mkuya aliangushwa katika Jimbo la Kikwajuni kwa nafasi ya uwakilishi.

Awali mbunge huyo alikuwa katika Jimbo la Welezo ambalo amelihama na kuhamia jimbo jipya.

Sambamba na hilo, mfanyabiashara maarufu, Mohamed Raza Dharamsi aliangushwa katika Jimbo la Uzini kwa nafasi ya ubunge huku mbunge mkongwe aliyepata kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Muungano tangu awamu ya pili ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Mohamed Seif Khatib akiibuka mshindi.

Dk. Khatib aliyepata kuwa waziri wa muda mrefu wa Muungano pamoja na Mambo ya Ndani katika awamu tofauti ikiwemo ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, amekuwa mshindi kwa awamu hii baada ya kupumzika kwa muda mrefu katika nafasi za uongozi wa kisiasa.

Mbunge mwingine mwanamke kwa muda wa  vipindi viwili, Bahati Nassir Abeid ameangushwa katika kura za maoni Jimbo la Mahonda na Kamal Abdulsatar Haji, huku aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo la Kiwengwa ambalo limefutwa na kuamua kugombea Jimbo la Mahonda, Asha Abdalla Mussa ameshika nafasi ya pili.

Waziri wa Maji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Professa Makame Mnyaa Mbarawa ameibuka kidedea katika kura za maoni na kupata 74 dhidi ya 13 alizopata mpinzani wake, Omar Abdallah.

Awali Professa Mbarawa alikuwa mgombea wa Jimbo la Mkanyageni kwa tiketi ya CCM ambalo kwa sasa limefutwa.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri ameshindwa kura za maoni Jimbo la Mkoani Pemba kwa kupata kura 53  dhidi ya mpinzani wake Abdalla Hussein Kombo aliyepata kura 57.

Mjawiri alikuwa miongoni mwa wanachama 32 waliochukua fomu kuwania kuteuliwa na chama nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) na mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis ameangushwa kwa kupata kura 30 na Soud Mohamed ambaye ni Mkurugenzi wa Hifadhi ya Misitu aliyeibuka mshindi kwa kupata kura 33.

Aidha aliyegombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM na kuibuka katika tatu bora, Dk. Khalid Salum Mohamed ameibuka na ushindi wa kishindo kwa kupata kura 83 na kumwangusha mpinzani wake Khamis Ame Mussa aliyepata kura 15.   

HABARI HII IMEANDALIWA NA ELIZABETH HOMBO (DAR ES SALAAM) na MAUWA MOHAMMED (ZANZIBAR)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles