33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Dk Mwinyi: Tunataka ushindi usio na malalamiko

 ANDREW MSECHU– DAR ES SALAAM

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapindizi (CCM) upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa mwaka huu chama hicho kinataka ushindi usio na malalamiko ya aina yoyote.

Amesema CCM inataka ushindi wa kishindo usio mwembaba ili kuondoa uwezekano wa kuwepo malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama.

Kauli hiyo ya Dk. Mwinyi, inakwenda kuzihakikishaia jumuiya za kimataifa kwamba CCM itapa ushindi unaotokana na maamuzi ya wananchi.

Akizungumza katika mapokezi aliyoandaliwa na wanachama wa mikoa miwili ya Pemba jana, alisema kuwa mapokezi aliyoyaona tangu alipowasili katika visiwa vya Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita hana shaka kuwa ushindi utakuwa mkubwa na atatengeneza serikali itakayowatumikia wananchi.

Dk. Mwinyi aliwaahidi waliokuwa wakimsikiliza kuwa atahakikisha wanaboresha maisha ya Wazanzibari katika nyanja zote.

Alisema yapo maneno yanayosemwa na baadhi ya wagombea wanaopita wakijinadi kuwa wametumwa na Dk. Hussein Mwinyi kugombea kwa sababu anataka kuwateua, akisisitiza kuwa hajatuma mtu na kila mtu apambane na hali yake.

MASLAHI YA ZANZIBAR

Pamoja na hali hiyo Dk. Mwinyi, alisema kuwa iwapo atafanikiwa kupata ushindi kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu atahakikisha analinda maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano.

Alisema hilo ni mojaya vipaumbele vyake, ikiwemo kulinda pia maslahiya Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ulimwenguni.

“Ninawahakikishia, iwapo nitashinda katika uchaguzi ujao nitasimamia kuhakikisha ninalinda maslahi ya Zanzinbar kwenye muungano, kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani, lengo likiwa ni kuhakikisha wanzanzibar wanakuwa na maslahi yao,” alisema.

Alisema dhamira yake ya kuwania nafasi ya urais ni kuwatumikia Wazanzibari kwa nguvu zake zote na kwamba iwapo watashika dola yatakuja mambo makubwa ikiwemo miradi ya kuendeleza Wazanzibar na kwamba atahakikisha anayapatia matatizo ya ajira kwa vijana ufumbuzi mapema.

Dk. Mwinyi alisema baada ya mchakato wa kumpata mgombea wa urais ndani ya chama kumaliika nay eye kuibuka mshindi, kazi yao sasa ni moja ya kuhakikisha wanapata ushindi utakaowawezesha kushika dola.

Alisema anawahakikishia kuwa atayaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kuudumisha na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania, ambao ni wa kupigiwa mfano duniani, hivyo viongozi lazima wawe mstari wa mbele kuudumisha na kuulinda.

Dk. Mwinyi ambaye alithibitishwa na CCM kupitia mkutano wake mkuu mjini Dodoma wiki iliyopita na kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, alisema suala la amani ni la kipaumbele kwake kama chanzo cha maendeleo na kwamba katika kipindi cha miaka 10 ya Rais wa sasa, Dk Mohamed Shein nchi imetulia na imekuw ana amani, hivyo akiwa rais jukumu lake itakuwa kuhakikisha amani inaendelea kudumu.

Alisema suala jingine ni kujenga umoja na kuondoa suala la Upemba na Uunguja, Ukusini na Ukaskazini na kwamba atahakikisha wote wanakuwa ni Wazanzibar.

Alieleza kuwa aatahakikisha hawatabagua kuwa mtu anatoka upande gani katika masuala yote muhimu ya kiserikali ikiwemo ajira na huduma zote za jamii, bila kujali mtu anatoka upande gani.

Alisema katika serikali ya Dk. Shein amefanya mambo makubwa na kwamba alipoachia yeye ndipo atakapoanzia, kuendeleZa miradi mikubwa ya miundombinu, huduma za jamii na ustawi wa watu.

Dk Mwinyi alieleza kuwa lazima ahakikishe anaboresha maisha bora kwa kila Mzanzibar na kwamba ukitaka kuyafanya hayo lazima watu wawajibike, kwa kuwa huwezi kuyafanya hayo na wala rushwa, wabadhirifu na wazembe.

“Sitakuwa na huruma wala muhali na mtu yeyote atakayekuwa kwenye kundi hili la wala rushwa, wabahirifu na wazembe, na nitahakikisha serikali tutakayoiunda inakuwa na maslahi kwa Wazanzibar wote.

“Wapo wanaosema mimi ni mpole sana na kwamba hawajaniona, mimi nasema watanielewa, kwa sababu moja tu, pengine hawajanisikia kwa vile nilikuwa katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo mambo yetu mengi tunayafanya kimya kimya kwa usiri, tunafanya kwenye ofisi zetu.

“Lakini ninasema kwa wale walio kwenye kundi la ubadhirifu, wala rushwa, wazembe na wasiowajibika hao watanielewa mapema sana,” alieleza.

KAULI YA DK. SHEIN

Awali, Rais anayemaliza muda wake, Dk Mohamed Shein aliwausia viongozi wa CCM kuwa Dk. Mwinyi tayari ameshajitolea na kuomba uongozi kisha kuchaguliwa, ila hawezi kuongoza peke yake, bali anahitaji kupewa viongozi wenzake kama yeye, wakiwemo wabunge na madiwani.

Aliwataka kuchagua viongozi vijana wazuri wenye sifa kama Dk Mwinyi, wasiwaletee watu wanaotaka kupewa shikamooo, kwa kuwa urais si kazi ya mpito, hivyo wanahitaji viongozi makini wenye uwezo, wabnaochaguliwa kwa sifa zao si kwa upendeleo ili waipe CCM ushindi.

“Safari hii tunataka tuonyeshe mfano Pemba, tunataka Pemba mpya kwa hiyo msiwachague wababaishaji wenye tamaa, bali wachagueni viongozi watakaokijenga chama chetu,” alisema

Alisema CCM ni chama kikubwa sana kina viongozi wengi wenye sifa hivyo hawana haja ya kung’ang’ania watu wasiofaa. 

Alisema ushindi kwa CCM ni lazima kama inavyoeleza Katiba yao kwamba lazima ishinde katika chaguzi zote za dola za Zanzibar na wana uwezo mkubwa kwa sababu ni chama kikubwa, wananchi wanakipenda na kina historia ndefu, cha watu waadilifu, wakweli, chenye viongozi wenye uwezo na upeo.

NAHODHA

Kwa upande wake, mgombea aliyefanikiwa kuingia tatu bora kwenye mcujo wa kura za urais, Shamsi Vuai Nahodha alisema Mwenyezi Mungu anapokutabiria jambo na akasema liwe litakuwa kama lilivyo, hakuna mganga wala mchawi atakayeweza kulibadili.

Alisema wanatakiwa kuunga mkono kila mmoja ili mgombea wao ashinde kwa kuwa ushindi wake ni wa chama na ni wa nchi.

Alisema kuna kauli inayorudiwarudiwa na maadui wao wa chama ambayo wanatakiwa waitafakari vizuri.

Alisema katika kujifunza kwake uongozi kwa zaidi ya miaka 20 suala la upole linazungumziwa kama kasoro ya uongozi suala ambalo si sahihi, kwa kuwa anaona upole ni sifa nzuri katika uongozi.

DK KHALID

Mgombea mwingine aliyefanikiwa kuingia katika tatu bora, Dk Khalid Mohamed alisema baada ya kumalizika kwa mchakato wa ndani na kupata mshindi wanatakiwa kuungana kuhakikisha kuwa CCM inashindsa kwa kishindo na Dk. Hussein Mwinyi anakuwa rais.

Aliwataka mashabiki wote katika maeneo yote Zanzibar, kutoka Unguja na Pemba kurejea na kuwa wa timu moja na kuachana na mwelekeo wa makundi yaliyokuwepo wakati wa mchakato huo

Alisema sasa kazi ni moja kwa kuwa wote ni kitu kimoja na wasitumie fursa ya uchaguzi ndanbi ya chama kukigawa chama.

 MBARAWA

Kwa upande wake, mmoja wa watia nia aliyekuwa ameingia kwenye tano bora, Profesa Makame Mbarawa alisema amefanya kazi kwa karibu zaidi na Dk. Hussein na kwamba ni mtu mkarimu na muungwana, anayependa kutenda haki bila ubaguzi, watu wote kwake ni sawa.

Alisema atakuwa kimbilio la wanyonge na ana uwezo mkubwa wa kuwaletea maendeleo kwa watu wote wa Unguja, Pemba an Watanzania na kwamba ataifanya Zanzibar ya kesho kuwa tofauti na leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles