26.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Wagombea CCM Watakiwa kujiandaa kisaikolojia

 WAANDISHI WETU– DAR/MIKOANI

WAKATI mchujo wa kuwapata wagombea watakaokiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye Uchaguzi Mkuu ukianza leo na kesho, wanachama waliojitokeza kutia nia kuteuliwa kugombea nafasi wametakiwa kujiandaa kisaikolojia kumuunga mkono yeyote atakayepitishwa na chama hicho ili kuendelea kulinda amani na utulivu ndani ya chama.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Julius Peter wakati akisoma taarifa ya jumla ya watia nia wote waliojitokeza kwenye mchakato huo.

Alisema wanachama 551 walichukua fomu katika nafasi za ubunge na udiwani huku 543 wakirejesha fomu, pia wanachama 148 walichukua fomu za viti maalumu na waliorejesha ni 146.

Peter alisema mpaka sasa ni kweli idadi ya watia nia imeonekana kuwa kubwa tofauti na miaka iliyopita na kusisitiza uwingi huo hautaathiri demokrasia ndani ya chama, jambo la kuzingatia ni wote waliojitokeza kuwa watulivu, kutojihusisha na rushwa pamoja na kujiandaa kisaikolojia kumuunga mkono yeyote atayebahatika kupitishwa kwenye kura za maoni pamoja na Kamati Kuu.

Alisema ili kupata wateule kutoka kwa watia nia waliojitokeza, mchakato wa kura za maoni utafanyika kuanzia leo Jumatatu na majina yatapelekwa kwenye Kamati Kuu kwa ajili ya kufanyiwa tathimini, hivyo watia nia wote wawe watulivu kwani kura za maoni pekee siyo hitimisho la kuchaguliwa badala yake sifa zingine pia zitaangaliwa na kamati kuu.

Dk. Andrew Luhanga, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambaye ni mmoja wa watia nia katika nafasi ya Ubunge Jimbo la Nyamagana alisema yeye amejiandaa kikamilifu kukiwakilisha chama na kuwatumikia wananchi iwapo atapewa dhamana na yupo tayari kumuunga mkono yeyote atakayepitishwa.

Alisema idadi ya watia nia siyo tishio kwake na kwa mtu yeyote anayejiamini na aliyejiandaa kuwa kiongozi, na kusisitiza yupo tayari kuzingatia miongozo kama ilivyotolewa na viongozi wakuu wa chama ikiwemo katibu mkuu wa CCM mkoa wa Mwanza na aliwashauri watia nia wengine kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na chama.

ILALA

Jijini Dar es Salaam, wagombea ubunge 274 katika majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea wanatarajia kuchuana katika mchakato wa kura za maoni unaoanza leo.

Idadi ya wagombea na majimbo kwenye mabano ni 95 (Segerea), 146 (Ukonga) na 35 (Ilala).

Akizungumza jana kwa niaba ya Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Mwenezi wa Wilaya, Said Sidde, alisema wagombea watatu hawakurudisha fomu.

“Mwamko umekuwa mkubwa kwa makada wa Chama cha Mapinduzi kuchukua fomu kwa sababu ya utendaji kazi mzuri wa Rais Dk. John Magufuli, Watanzania wengi hivi sasa wanaunga mkono juhudi za rais wetu,” alisema Sidde.

Aidha alisema kura za maoni kwa Wilaya ya Ilala zinatarajiwa kufanyika leo Jumatatu na kesho kwa majimbo yote matatu.

Alisema kwa Jimbo la Segerea uchaguzi utafanyika Tabata wakati Jimbo la Ilala utafanyika Lamada na Jimbo la Ukonga utafanyika kesho Kitunda Relini.

Alisema vitambulisho vya wajumbe wa mkutano mkuu vitatolewa na makatibu wa CCM wa kata na kuwataka wapigakura wote kufika kwa wakati.

DODOMA

Mkoani Dodoma, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa, Pili Mbanga alisema waliojitokeza katika Majimbo 10 ya Mkoa huo kuchukua fomu katika kinyang’anyiro cha ubunge ndani ya CCM wako 330 ambapo kati yao waliorejesha fomu ni 324 wasiorejesha fomu wako sita.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Katibu huyo alisema kwa upande wa UWT waliochukua fomu wako 97 na wote wamerejesha fomu hizo.

Alisema kwa upande wa UVCCM waliochukua fomu wako 28 na wote wamerejesha na Jumuiya ya Wazazi waliochukua fomu wako wawili na wote wamerejesha.

Alisema Dodoma Mjini waliochukua fomu 58 huku wanaume wakiwa 52 na Wanawake sita ambapo wote wamerejesha fomu.

Kaimu Katibu huyo alisema Kondoa Mjini wamechukua fomu 47 ambapo Wanawake ni watatu na wanaume 42 ambapo waliorejesha ni 45 huku wawili wakiwa hawajarejesha.

Kwa upande wa Mtera waliochukua fomu ni 18 na kurejesha wote ambapo wote ni wanaume.

Alisema Bahi waliochukua fomu ni 36 ambapo Wanawake ni wanne na wanaume ni 32 huku mmoja akiwa hajarejesha.

Kwa upande wa Chilonwa alisema wagombea waliochukua na kurejesha fomu ni 35. Kaimu Katibu huyo alisema kwa Mpwapwa waliochukua ni wagombea 64 huku Kibakwe wakiwa ni 19.

Alisema leo na kesho utaanza mchujo ambapo wagombea wote watajieleza katika Kamati za siasa za Wilaya.

Mkoani Arusha, wagombea 318 kati ya 432 wa CCM, kutoka majimbo saba ya mkoa wa Arusha wanatarajia kuchuana leo katika mchakato wa kura za maoni.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Musa Matoroka, alisema kati ya wagombea 432 waliochukua na kurejesha fomu za kuwania ubunge, wagombea 114 wanatokea Viti Maalum.

Matoroka alisema awali waliochukua fomu walikuwa wagombea 434 ila wagombea wawili kutoka majimbo ya Monduli na Arusha Mjini hawakurejesha fomu.

Alisema mchakato wa kura za maoni katika majimbo yote unatarajiwa kufanyika Julai 20 na 21 mwaka huu kabla ya majina kupelekwa ngazi za juu kwa ajili ya uteuzi.

Alitaja idadi ya wagombea na majimbo wanayotoka kuwa ni Arusha Mjini (91), Arumeru Magharibi (61), Arumeru Mashariki (33),Karatu (53),Ngorongoro (14), Longido (12) na Monduli (24).

Matoroka alisema wagombea wa Viti Maalum ambao ni 114 wakiwa wanatokea Viti Maalum kupitia Jumuiya ya Vijana(UVCCM), Jumuiya ya Wazazi, Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT), kupitia kundi la mkoa, walemavu, wasomi na wafanyakazi.

“Idadi ya wagombea kupitia kila jumuiya na idadi zao kwenye mabano kuwa ni Jumuiya ya Vijana (30), Wazazi (9), U.W.T kupitia mkoa, walemavu, wasomi na wafanyakazi wakiwa (105),” alisema.

CHADEMA TANGA

Katika Mkoa wa Tanga, vijana wengi wamejitokeza kutaka kuwania nafasi za udiwani kwenye Halmashauri ya Jiji la Tanga kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Tanga, ambao wamethibitisha kupokea wanachama kutoka kundi hilo waliorejesha kadi za vyama vingine na kuchukua fomu za kuwania udiwani.

Hayo yalibainika jana baada ya uongozi wa Chadema Wilaya ya Tanga kupokea wanachama 33 kutoka CCM, CUF na ACT- Wazalendo huku waliochukua fomu za kuomba ridhaa ya kuwania udiwani vijana wakiwa zaidi ya 26 kati ya kata 27 zilizopo wilayani hapa.

Wakizungumza baada ya kupokea kadi za uanachama wa Chadema vijana hao walisema wameamua kujitokeza ili kuongeza nguvu ya kisiasa katika chama hicho cha Chadema.

Akizungumza mmoja wa vijana nao Rehema Kassim kutoka Kata ya Duga Jijini Tanga, alisema wameamua kwenda chadema kwa sababu wameona huko ndiko ambapo vijana watajenga mshikamano.

Naye kwa upande wake, Bakari Madskuzi kutoka Kata ya Duga, alisema ameamua kuchukua fomu ya kukiomba chama hicho kimpitishe kuwania udiwani kata ya Duga ili aweze kutatua kero ikiwamo Tarura kuweka udongo mwekundu katika barabara za mitaani na hivyo kuhatarisha afya za wakazi.

Alisema Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura), wameweka udongo mwekundu katika barabara za Magomeni, vumbi linaingia vyumbani, madukani unga unabadilika rangi na kuwa mwekundu, ukiwauliza Tarura wanakwambia huo ni udongo bora badala ya kuweka kipaumbele katika afya.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Tanga, Nuru Athumani alisema kwamba wamefurahishwa kupokea kundi kubwa la vijana walioamua kujiunga na chama hicho ambapo alisisitiza kuwa hiki ni kipindi chao.

Alisema kupitia kundi hilo anaamini kwamba Chadema itapata ushindikatika udiwani wa jimbo la Tanga na kata 27 zilizopo Wilayani Tanga.

SINGIDA

Katika Mkoa wa Singida, wanachama CCM 233 wamechukua fomu za ubunge katika majimbo saba ya mkoa ya kurudisha. Kati yao wanaume ni 215 na wanawake 18.

Miongoni mwao ni wabunge wa majimbo waliomaliza muda kwa nyakati tofauti, akiwemo Mussa Ramadhani Sima (Singida mjini), Mwingulu Nchemba (Iramba magharini), John Lwaji (Manyoni Magharibi), Diana Chilolo (viti maalum), Martha Mlata (Viti maalum) na Justin Joseph Monko (Singida Kaskazini). 

 Pia wapo wastaafu kutoka serikalini akiwemo Ofisa Ustawi wa Jamii Singida Vijijini, Emmanuel Martini Misholi, Ofisa Elimu Wilaya ya Ikungi, Hongoa Mohammed Bayu, wafanyabishara mjini hapa, Hassan Philip Mazala na Hiderali Hussein Gulamali.

Waliochukua fomu na kurejesha kupitia Viti Maalumu UWT ni 15, kupitia Wanawake ni Kundi la Walemabvu ni wawili, sita wamechukua fomu na kurejesha kupitia Viti Maalumu.

Habari imeandaliwa na NORA DAMIAN (DAR), NATHANIEL LIMU (SINGIDA), YOHANA PAUL (MWANZA), RAMADHAN HASSAN (DODOMA) NA OSCAR ASSENGA (TANGA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles