CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM
TAKWIMU za mwaka jana za ugonjwa wa saratani zinaonyesha , saratani inayoongoza nchini ni ya shingo ya kizazi kwa wanawake kwa asilimia 47 ikifuatiwa na tezi dume kwa asilimia 23.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam katika Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kitaifa Sabasaba, Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa umma kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORI), Dk. Maguha Stephano alisema, katika maonyesho hayo mwaka huu wamekuja kupima, kutoa elimu na jinsi ya kudhibiti saratani.
Alisema saratani ya shingo ya kizazi imekuwa ikiongoza hivyo ni vema wanawake wakajenga mazoea ya kuchunguza afya za mara kwa mara.Alitaja takwimu hizo za mwaka jana na aina ya saratani kuw
a ni kwa upande wa wanawake na asilimia kwenye mabano ni shingo ya kizazi (47), matiti ( 16), utumbo mpana na mwembama (5.8), koo (5.3) na kichwa na shingo (4.2).
Maguha alisema kwa upande wa wanaume ni tezi dume (23), Koo la chakula (16), kichwa na shingo (12), matezi (9), na utumbo mpana na mnene ni 11.4.
“Tunatoka wito kwa jamii kujenga mazoea ya kupima kwani saratani Ina uwezo wa kutibika ukiwahi hatua ya kwanza na ya pili ukifika ya tatu na nne ni ngumu kutibika,” alisema Maguha.
Maguha alisema katika maonyesho ya mwaka huu wanawake 251 walijitokeza kupima matiti ambapo wawili walibainika na vivimbe, waliopima saratani ya mlango wa kizazi ni 193 na kati yao watatu walibainika kuwa na mabadiliko ya awali na wameanza kupewa tiba.
“Pia wanaume 106 walijitokeza kupima saratani ya tezi dume huku wawili kati yao walibainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo na tumewapa rufaa ili waendelee zaidi na vipimo,” alisema Maguha.
Aliongeza kuwa watu wenye ualbino watano walijitokeza kuchunguza saratani ya ngozi ambapo mmoja alibainika ngozi yake imeharibika zaidi na just ambapo amepewa matibabu ya awali na kumpa ushauri jinsi yya kujikinga na jua.
Wakati huohuo, Dk. Maguha alisema chanjo inayotolewa kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka 14 ina mwitikio mkubwa hivyo muhimu kwa wazazi kuhamasisha watoto wao kupima Mara kwa mara.