MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumaliza kazi na kupendekeza majina ya wagombea watano ya wanachama wake ambao wameomba kuteuliwa kuwania urais wa Zanzibar, tayari wagombea na wapambe wao wameanza kupigana vikumbo vya wajumbe wa NEC kuanza ushawishi.
Kukamilika kwa hatua hiyo ya awali inakwenda kuhitimisha mshikemshike kwa wagombea 32 waliochukua fomu ambapo kati yao 31 ndiyo waliorudisha fomu hizo baada ya kukidhi sharti ya kutafuta wadhamini 250.
Kutokana na hali hiyo kwa siku ya jana jijini Dodoma tayari timu za wapambe wa wagombea ambao wanatajwa kupendekezwa kwenye kinyang’anyiro hicho zimeanza kuwasili jijini Dodoma na baadhi yao kuanza kudhibiti vyumba katika baadhi ya hoteli jijini hapa.
Pamoja na kwamba safari hii CCM kuamua kufanya siri juu ya majina hayo, kwa kile ilichodai kuwa inakwepa kutengeneza makundi MTANZANIA limefanikiwa kupata majina hayo kupitia vyanzo vyake vya ndani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo waliopendekezwa na kikao hicho kilichofanyika juzi na kuhudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa Omar.
Yumo pia Dk. Khalid Salum Mohammed ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo kwa tuhuma za kuanza mbio za urais mapema.
Wengine ni aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Makame Mbarawa.
Mmoja ya mjumbe wa NEC ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazeti aliiambia MTANZANIA jana baada ya kumalizika kwa vikao Kisiwani Unguja, kumekuwa na kazi kubwa kwa baadhi ya wajumbe kupigiwa simu za kuombwa kuungwa mkono kwa baadhi ya wagombea urais kupitia vikao vya chama.
“Huu ni mwaka wa kazi kwa kweli jana(juzi) usiku nilipokea simu si chini ya sita zote zikitaka niunge mkono baadhi ya wagombea (anataja majina), lakini kwa kuwa sasa NEC inakwenda kuamua ni nani atayegombea nimewajibu tusubiri uamuzi wa chama.
“Hili limekuwa ni jambo la kawaida na kubwa ninaamini kabisa CCM tutapata mgombea mzuri ambaye atakwenda kupambana na vyama vingine vya siasa. Na imani inaniambia kwamba tuna kila sababu ya kuomba ili tutokea wamoja kama Mwenyekiti wetu, Rais Dk. John Magufuli anavyosisitiza kila mara.
“Nina hakika tutavuka salama na hii inaonesha kwamba CCM ina siasa iliyokomaa na ina benki ya kutosha na wanachama wake ambao wana sifa bora za kuwania nafasi mbalimbali. Ila kesho(leo) ninaamini nitaanza safari ya kuelekea Dodoma licha ya vikao kuwa Julai 9 kwa kamati mbalimbali za chama na Julai 11-12 kuhitimishwa kwa Mkutano Mkuu wa chama chetu.
“…tunakwenda kumuongeza Magufuli (Rais Dk. John) mitano tena nami kama Mjumbe wa NEC ninaamini tutatoka tukiwa imara zaidi na kwenda kupata Rais wa awamu ya nane wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema Mjumbe ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa chama.
DODOMA KUMEKUCHA
Kwa muda wa wiki moja sasa jijini Dodoma kumekuwa na hali ya shamrashamra za kuashiria kuiva kwa maandalizi ya vikao vya CCM ambapo maeneo mengi yamepambwa na bendera za kijani.
Hata hivyo kwenye baadhi ya hoteli tayari wameanza kutoa agizo la kuanza Julai 10 kutopangisha wateja wapya kwa kuwa hoteli zao zitapokea wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao unaotarajiwa kufanyika Julai 11-12, mwaka huu.
Gazeti hili lilishudia baadhi ya wanachama wa CCM ambao walikuwa wakizunguka na magari kusaka nafasi za watu wao wa karibu ambao watahudhuria mkutano huo ambapo kundi kubwa ni wapambe hasa wa wagombea urais wa Zanzibar.
Hoteli kubwa za jijini Dodoma nazo zimeanza kuwa kwenye maandalizi ya kupokea wageni wakiwamo wabunge wanaomaliza muda wao ambao wengi wao walikuwa wakiishi kwenye hoteli hizo pindi walipokuwa kwenye vikao vya Bunge.
Dodoma ambako vikao vya juu vya maamuzi vya CCM vinatarajiwa kuanza kuketi kuanzia kesho vimelifanya Jiji hilo kuchangamka kutokana na kuonekana wageni wengi.
Vikao hivyo ambavyo vinatarajiwa kuanza Dodoma lweo Julai 6 na 7 ni cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho kitaanza kuchuja majina na kitaketi katika ukumbi wa, Jakaya Kikwete uliopo njia ya kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Jijini hapa.
Julai 8 kitafuatia kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili CCM na Julai 9- Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ambayo itatoa mapendekezo ya majina matano NEC
Julai 10, NEC itapendekeza majina matatu kwenye Mkutano Mkuu.
Julai 11 -12, Mkutano Mkuu wa CCM utachagua jina moja la mgombea wa urais wa Tanzania.
Kutokana na uwepo wa vikao hivyo pembezoni mwa ofisi za makao makuu ya chama hicho (White House) wafanyabiashara wameonekana kuchangamkia fursa ya kuuza vitu mbalimbali ambavyo wanachama na wasio wanachama wananunua.
MTANZANIA lilifika katika eneo hilo na kujionea jinsi ambavyo biashara imechangamka ikiwemo ile ya mashati, magauni yenye nembo ya CCM, matunda na chakula.
Mmoja wa wafanyabiashara, Said Juma, alisema kuwa hali ya biashara kwa upande wake imekuwa nzuri kwani wengi wamekuwa wakifika katika eneo hilo na kununua mashati, magauni na urembo mbalimbali ambao una rangi ya CCM.
“Mimi hapa nauza mashati na vitu mbalimbali vyenye nembo ya CCM mfano bangili, shanga, biashara imekuwa nzuri kila mmoja anayekuja hapa ananunua kitu,” alisema.
Naye, Mwajuma Mwashamba alisema mara baada ya Rais kurejesha fomu ya kugombea urais biashara imechangamka katika eneo hilo.
“Mimi nauza mashati tu, biashara imekuwa nzuri nilikuwa na mzigo wa muda mrefu lakini sasa hivi nakaribia kuumaliza,”alisema.
Huku, Christopher Madilu, ambaye ni wakala wa kutoa fedha jirani na Ofisi za CCM alisema biashara imekuwa nzuri kwani wanaotoa na kuingiza fedha ni wengi.
“Wengi wanatoka kwenye hilo geti la CCM wanakuja hapa kutoa na kuweka fedha nadhani kutakuwa kuna kitu lakini nilisikia kulikuwa kuna vikao vya wenyeviti wa Mikoa wa CCM,” alisema.
Pia, katika maeneo mengine hali ya biashara imechangamka kuanzia katika migahawa ya chakula.
Nyumba za wageni nyingi zimeonekana kuwa na wageni ambapo Mfanyakazi wa Hoteli ya Kidia ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini alisema kwamba idadi ya watu imeongezeka tangu wiki iliyopita.
“Watu ni wengi wengine wamekuja tu kuangalia jinsi ambavyo vikao vya CCM vitafanyika ila wiki iliyopita pia kulikuwa kuna watu wengi kutokana na Wenyeviti wa CCM kuwepo hapa,” alisema.
Julai 4, mwaka huu kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichojifungia jana kimetoka na mapendekezo ya majina ya wanachama watano kati ya 32 waliochukua fomu kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa ratiba inaonyesha majina hayo sasa yatapelekwa Dododma ambapo Julai 9 Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa itapendekeza majina matatu.
Julai 10, Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM itachagua jina moja la mgombea.
Julai 11 – 12, Mkutano Mkuu wa CCM utathibitisha jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa urais Tanzania na upande wa Zanzibar.
Wakati vikao vya juu vya kuchuja majina ya wagombea nafasi ya urais CCM vikianza jana jijini Dodoma, Kwa upande wa Zanzibar tayari vikao vya juu vya kujadili wagombea urais vilikwishaanza tangu Julai 1- 2 kwa Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar kuketi kuchuja majina.
Julai 3 kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar kiliketi kwa ajili hiyo hiyo.
DK. MABODI NA SIRI
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ alisema wameamua kufanya siri juu ya majina hayo matano ili kulinda umoja ndani ya chama hicho.
Alisema kamati hiyo iliyopendekeza majina hayo matano ni sehemu muhimu ya maandalizi na uchujaji wa majina ya wagombea watano wanaotakiwa kuwasilishwa katika Kamati Kuu kwa ajili ya kujadiliwa tena na kumtafuta mgombea mzuri mwenye sifa 12 zikiwemo hekima, kuaminika, kuthamini muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Mabodi alisema baada ya Kamati Kuu kujadili kwa kina majina hayo matano itapendekeza majina matatu na kuyapeleka Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo itachagua jina la mtu mmoja ambaye atapeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya urais wa Zanzibar.
Alisema baada ya hatua hiyo mgombea huyo atapelekwa katika Mkutano Mkuu wa CCM kwa ajili ya kuthibitishwa na kupata baraka za wajumbe wote wa Kamati Kuu ya chama hicho na kuendelea na michakato mingine.
Dk.Mabodi, alisema baada ya kukamilika kwa mchakato huo itaendelea awamu ya pili ya uchukuaji wa fomu kwa nafasi za ubunge, uwakilishi na Udiwani na kufuata utaratibu wa miongozo ya CCM.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, amewasifu viongozi kwa ukomavu wao wa kisiasa kwa kufuata Katiba, miongozo na kanuni za CCM kwa kutobeba wagombea mifukoni.
Alisema kuwa kikao hicho kimesisitiza usiri kwa wagombea hao kwani ndani ya CCM ikibainika miongoni mwao kuna mtu kakiuka utaratibu anaweza kuondolewa na kuchaguliwa mtu mwingine.
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ulianza Juni 15 hadi 30, mwaka huu ambapo jumla ya makada 32 walijitokeza kuchukua fomu hiyo ambao ni, Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Jafar Jumanne Mohamed Hijja Mohamed, Issa Suleiman Nassor.
Wengine ni Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohamed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk.Khalid Salum Mohamed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni Mohamed Aboud Mohamed, Bakari Rashid Bakar, Mgeni Hassan Juma, Ayoub Mohamed Mahmoud, Hashim Salum Hashim, Fatma Kombo Masoud, Hasna Attai Masoud, Maalim Hamad Idd Hamad Idd, Pereira Ame Silima, Shaame Mcha, Mussa Aboud Jumbe na Moudline Cyrus Castico.
MAALIM SEIF NA TAKUKURU
Mwandishi wetu Mauwa Mohammed, kutoka Visiwani Zanzibar anaripoti kwamba, Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amechukua fomu ya kuomba ridha katika chama chake ya kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar mwaka 2020 .
Fomu hiyo amekabidhiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, katika hafla ilifanyika katika ofisi kuu ya chama hicho iliyopo Mtaa wa Vuga mjini Zanzibar .
Malim Seif hadi anachukua fomu hiyo amekuwa ni mgombea pekee aliyechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Chama cha ACT Wazalendo na kuwataka wanachama wengine wenye uwezo na nia ya kugombea kujitokeza kuchukua fomu.
“Ahadi yangu ya kuleta mabadiliko kwa siku mia bada haijaondoka endapo nitapata ridha kwa wananchi ya kuiongoza serikali,” alisema Maalim Seif
Hata hivyo alisema akipata ridhaa ya kuongoza nchi ya Zanzibar hatofukua makaburi kwani yatasababisha kuleta chuki katika jamii na vizazi vijavyo.
“Sitofukua makaburi sitogeuka nyuma nitasonga mbele ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif
Awali, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema kwamba tangu zoezi hilo la uchukuaji fomu kuanza katika chama chao Julai 1, mwaka huu wanafarijika kuona wanachama wengi wamejitokeza kuitikia wito kwa wingi kuchukua fomu.