Na MARY MWITA -ARUSHA
JESHI la Polisi limejivua lawama za kuua kesi za unyanyasaji na ukatili kwa watoto na kusema baadhi ya wazazi wamekuwa wakikaa vikao katika ngazi ya jamii na kukwamisha mashauri hayo.
Mkuu wa Polisi Mkoa Jamii Mkoa wa Arusha, Joswam Kaijanante,
alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanasheria na watoa huduma za kisheria jijiji Arusha jana.
Alisema polisi wamekuwa wanatupiwa lawama za kuzima kesi lakini ukweli ni kuwa baadhi ya wazazi wanazima kesi kwa kukaa vikao katika jamii jambo ambalo siyo sahihi .
Kaijanante alisema wazazi wanaozima kesi za ukatili wa watoto hawana budi kuchukuliwa hatua
na kutaka wanasheria na wadau wa haki za watoto kushirikiana na polisi kukabiliana na changamoto hiyo inayokwamisha haki za watoto na kuzidisha ukatili katika jamii.
Naye Mwanasheria wa Taasisi ya Sky, Mary Kinabo, alisema wazazi wenye kushiriki katika ukatili dhidi ya watoto kwa kuzima kesi za watoto wao, wakibainika wanapaswa kuchukuliwa hatua ili iwe fundisho kwa wengine.
Kinabo alisema watoto ni wazazi wa kesho hivyo wanapaswa kulelewa katika njia ipasayo ili kuwajengea msingi bora wa maisha ambao hauna ukatili na uonevu.
Kwa upande wake Msajili Msaidi wa Huduma ya Msaada Kisheria Jijini Arusha, Ahadi Msangi, alisema mkutano na wadau wa sheria unafungua ukurasa wa kushirikiana kusaidia watu kupata haki hususani wanawake na watoto.
Msangi alisema Jiji
la Arusha liko mstari wa mbele kutetea haki za binadamu na ndiyo maana wameamua kuungana kwa pamoja na wadau wa elimu ili kubaini changamoto zinazokwamisha haki kwa wananchi na kushirikiana kuzitatua na kuwezesha watu kupata haki zao.
Jukumu la kulinda haki za mtoto ni la kila mtu na jamii haina budi kukemea ukatili dhidi ya watoto na wanawake.