Mwandishi Wetu-Morogoro
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiasha wote kufika katika ofisi za mamlaka hiyo kulipa kodi ya mapato mapema ili kuepuka misongamao inayojitokezaga katika tarehe ya mwisho Juni 30.
TRA ambayo imejiwekea utaratibu wa mara kwa mara kutoa elimu ya kodi wa walipakodi wake, hivi sasa ipo katika mikoa mbalimbali ikiendesha kampeni kwa wafanyabiashara kwa kupita mlango kwa mlango.
Akizungumza mkoani morogoro baada ya kutembelea baadhi ya wafanyabiashara wa maduka, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Maternus Mallya anasema TRA inafanya kampeni ya kutoa alimu ya kodi mkoani hapo ikiwa ni pamoja na kuhamashisha ulipaji wa kodi mbalimbali za serikali hasa kodi ya mapato ambapo mwisho wa kulipa ni Juni 30 mwaka huu.
Anasema katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Korona TRA isingependa kuwa na misongamano ya watu katika ofisi zake hivyo wafanyabiashara wa mkoani na wilayani wanatakiwa kufika mapema kulipa kodi kabla ya kuepuka misongamano.
Anasema kampeni hiyo itakayomalizika Juni 22 katika mkoa wa Morogoro, pia wanaitumia kupokea maoni na changamoto wanazokutana wafanyabiashara kwenye biashara zao ili ziweze kutatuliwa.
‘‘Tunategemea wafanyabiashara watajitokeza kwa wingi kwenye ofisi zetu ili wafanyiwe makadirio, tumekuta baadhi wamefanya makadirio lakini hawajalipa kodi zao kwa tarehe wanazotakiwa hivyo tunawahimiza ambao bado hawajakadiriwa wafike wakadiriwe,’’ anasema Mallya.
Naye Ramadhani Nasorro mfanyabiashara wa duka la vifungashio anasema kampeni hiyo ya elimu ya kodi imemuwezesha kujua umuhimu wa kutunza kumbukumbu za biashara zake ikiwa ni pamoja na kutoa risiti kwa wateja wake kila baada kuwahudumia.
Anasema kutokana na elimu ya kodi aliyopata atakuwa akiwashauri wafanyabiashara wenzake kufika katika ofisi za TRA kupata elimu hiyo pale watakapokuwa wanahisi hawana uelewa napo ili waweze kujua haki zao.
Kamal Kamal ambaye ni mfanyabiashara wa duka la spea za magari anasema kuwa yeye ni mtoaji mzuri wa risiti za kielektroniki kila baada anapotoa huduma na kwamba changamoto anayokutana nayo ni pale anapomuuzia mteja kifaa cha gari alafu kifaa kile kikawa hakiendani na gari lake mteja anaamua kukirudisha ili arudishiwe pesa.
‘‘Unapomrudishia pesa mteja uliyekwisha muhudumia na mashine imeshasoma kuwa umefanya biashara hiyo ni changamoto kutokana na kuwa TRA hawawezi kuelewa kuwa pesa ilirudishwa kwa mteja wao wanachotaka ni kodi yao hivyo tunaomba watusaidie namna ya kuiweka sawa changamoto kama hiyo,’’ anasema Kamal