26 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Viti Maalumu Chadema nao waanza kupukutika

 RAMADHAN HASSAN– DODOMA

IKIWA imebaki miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendea kukimbiwa na wabunge na sasa kibao kimehamia kwa wale wa viti maalumu.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema ilipata wabunge 72, kati yao wa majimbo wakiwa 35 na wa viti maalumu 37.

Jana wabunge wawili wa viti maalumu; Joyce Sokombi na Susanne Maselle, walitangaza kujiunga na Chama cha NCCR Mageuzi.

Mbali na wabunge hao, tayari wenzao zaidi ya 10 wa majimbo wametangaza kuhama na kujiunga CCM na NCCR Mageuzi, huku wengine wakiwa bado hawajatangaza watajiunga na chama gani. Wabunge wa majimbo ambao wametangaza kung’atuka Chadema ni Pauline Gekul (Babati Mjini), James ole Milya (Simanjiro), Joseph Mkundi (Ukerewe), Marwa Ryoba (Serengeti), George Waitara (Ukonga), Godwin Molel (Siha), Cecil Mwambe (Ndanda) na Julius Kalanga (Monduli), ambao wote wamejiunga CCM.

Pia hivi karibuni, Mbunge wa Vunjo, Joseph Selasini na Athony Komu (Moshi Vijijini), walitangaza kuwa baada ya Bunge kwisha watajiunga na NCCR Mageuzi.

Mbali na wabunge hao, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali akiwa anachangia bungeni, aliomba kujiunga na CCM, huku Mbunge wa Momba, David Silinde, ambaye chama chake kilimvua uanachama, akisema atatafuta chama kingine cha kujiunga nacho.

Fukuto ndani ya Chadema limeonekana kuongezeka hivi karibuni baada ya baadhi ya wabunge kutotii agizo la mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, aliyewataka kukaa wiki mbili bila kukanyaga eneo la Bunge ikiwa ni sehemu ya kujikinga na corona.

Baadhi ya wabunge wa chama hicho waliokaidi agizo hilo ni pamoja na Sokombi na Maselle ambao jana walitangaza kujiondoa kwenye chama hicho ikiwa ni siku chache tangu wapewe onyo kali kutokana na kukaidi kwao agizo la chama.

Mbali na wabunge hao, wengine waliokaidi agizo hilo walikuwa ni Sabreena Sungura, Latifa Chande, Dk. Immaculate Sware, Anne Gidery, Rose Kamili, Lucy Mlowe na Mariamu Msabaha – wote wa viti maalumu.

Wengine ni Mbunge wa Moshi Mjini, Japhari Michael, Komu, Selasini, Silinde, Lijualikali, Mbunge wa Bukoba mjini, Wilfred Lwakatare na Mbunge wa Kataru, Willy Qambalo. 

Kutokana na kukaidi huko agizo la chama, Chadema iliwafukuza uanachama wabunge wake wanne wakiwamo Selasini na Komu ambao kabla ya kufukuzwa, walishatangaza kuhamia NCCR Mageuzi baada ya Bunge kuvunjwa.

Pia Chadema kilitangaza kuwavua uanachama Silinde na Lwakatare kutokana na kukaidi agizo la chama la kutoingia bungeni na pia kukikashfu pamoja na viongozi wake.

Uamuzi huo ulitolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika Mei 11, mwaka huu ambaye alisema wabunge hao wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari na kutoa maneno ya kashfa na kejeli dhidi ya maagizo ya chama na viongozi.

KIBAO VITI MAALUMU

Akizungumza na waandishi wa habari jana ijini hapa, Mbunge wa Viti Maalumu, Massele alisema baada ya Bunge la 11 kuahirishwa, watashirikiana na wanawake wa NCCR Mageuzi kulitumikia taifa.

Maselle alizitaja sababu zilizowasukuma kujitoa katika chama hicho kuwa ni pamoja na kutokuheshimu katiba ya chama ilihali msingi mkuu wa kuanzishwa kwa mageuzi ya mfumo wa vyama vingi ni vuguvugu la kudai katiba mpya ya Tanzania.

Sababu nyingine ni kutotekelezwa kwa vitendo kwa demokrasia ndani ya chama hicho hali iliyosababisha kukiukwa kwa haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa na kutolea mfano wa wabunge wenzao wanne; Selasini, Komu, Silinde na Lwakatare kufukuzwa uanachama bila kusikilizwa.

‘‘Ndani ya Chadema hakuna haki ya kusikilizwa, ukiukwaji wa haki ya kuhoji matumizi ya michango na fedha za ruzuku. Mfano sisi wabunge wa viti maalumu kila mmoja wetu kwa mwezi huchangia chama Sh 1,550,000 ambapo tangu mwezi Januari 2016 mpaka mwezi Aprili 2019 ambapo ni miezi 40 kuna milioni 62/-.

 “Wabunge wa viti maalumu tupo 37, hivyo tumechangia zaidi ya Sh bilioni 2.2. Ieleweke wazi kuwa hoja yetu hatulalamikii kuchangia chama kwa kuwa ni wajibu wetu kufanya hivyo, hoja ni kwamba fedha hizi matumizi yake hayajawahi kuwekwa wazi na hakuna mwanachama anayeruhusiwa kuhoji popote,” alisema Maselle.

Alisema pia wanakerwa na sababu ya mfumo wa madaraka kuhodhiwa na wachache, wengi wao wakiwa ni wanaume na hivyo kuwepo mwanya wa unyanyasaji wa kijinsia na kingono.

‘‘Ndani ya chama hiki kuna mgawanyiko mkubwa unaotokana na baadhi ya watu kujiona wao ni bora kuliko wengine, na kwa bahati mbaya sana jitihada zote za kutaka kuondokana na hali hii ili tubaki tukiwa wamoja tunapoelekea Uchaguzi Mkuu zimeshindikana.

“Tumechoshwa na makundi ya kibaguzi hadi bungeni, kwa sisi wabunge uchangiaji katika vikao vya Bunge unaenda kwa kufahamiana na wengine tumefanywa wapiga makofi wa wanaoitwa maarufu, yaani super stars,” alisema Maselle.

SABABU ZA KWENDA NCCR MAGEUZI

Wabunge hao walizitaja sababu zilizowavutia kwenda NCCR Mageuzi kuwa ni mfumo wake wa kuendesha chama kitaasisi ambao itikadi yake ni utu huku msingi wake ukiwa ni haki za binadamu.

Sababu nyingine ni katiba yake pamoja na mambo mengi mazuri yaliyopo, kwamba imeweka wazi usawa wa kijinsia.

Walitolea mfano Makamu Mwenyekiti wa Taifa na Katibu Mkuu ni wanawake na kuwa chama cha mfano hapa nchini kuzingatia usawa wa kijinsia.

 Mbali na sababu hizo, walisema katiba na kanuni za uendeshaji wa chama zimeziba mianya ya uvunjifu wa amani ndani na nje ya chama hivyo kulinda amani ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles