KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
MAOMBI yaliyowasilishwa na mfanyabiashara James Rugemarila na mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege, ya kutaka waachiwe huru na kwamba hati ya mashtaka ni batili yamegonga mwamba.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.
“Mahakama hii haiwezi kutoa amri kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wala kumwachia mshtakiwa kwa sababu haina mamlaka ya kufanya hivyo na wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mahakama Kuu kwa mujibu wa sheria na kibali cha DPP,” alisema Hakimu Shaidi.
Rugemalira Februari 29, 2020 aliwasilisha hoja ya kumtaka DPP atoe kibali cha kumwachia huru na ikiwa atashindwa kufanya hivyo, basi mahakama hiyo imwondoe katika kesi hiyo huku Makandege ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, akiwasilisha hoja zake Machi 26, 2020 zilizodai kuwepo kwa mapungufu katika hati ya mashtaka yanayomkabili.
Akiiwakilisha Jamhuri jana, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, alidai shauri hilo lililetwa kwa kusikiliza uamuzi mdogo wa mapingamizi ya awali ya mshtakiwa wa kwanza (Rugemalira) na wa tatu katika kesi hiyo.
Akisoma uamuzi huo, Hakimu Shaidi alisema; “mahakama imepitia mapingamizi yenu, mahakama yangu haina mamlaka ya kutekeleza hoja zenu, mahakama hii ina uwezo wa kutaja tu na kusoma maelezo ya mashahidi ikiwa upelelezi umekamilika, na Mkurugenzi wa Mashtaka ametoa kibali cha kuiruhusu Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza kesi hii.
“Yote mnayoyalalamikia mahakama yangu haina mamlaka ya kuyatatua, hivyo kama mnaona kuna mambo hamridhiki nayo, naomba mpeleke hoja zenu Mahakama Kuu,” alisema Hakimu Shaidi.
Mshtakiwa Harbinder Seth aliiomba mahakama hiyo isaidie kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kwani imechukua muda mrefu kuanza kusikilizwa ukiachilia mbali uamuzi alioufanya mwaka jana wa kuandika barua ya kukiri makosa na kuomba makubaliano na DPP bila kupata majibu.
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Shaidi alisema kuwa hakuna mahakama inapenda kuchelewesha kesi, na kuongeza kuwa kama angekuwa na mamlaka angeshaifuta.
Kuhusu barua aliyoandika kwa DPP, Hakimu Shaidi alisema kuwa utaratibu huwa kisheria ni baina ya ofisi ya DPP na mshtakiwa, hivyo mahakama haihusiki kwa chochote bali inasubiri taarifa tu kwa utekelezaji wa maamuzi yatakayofikiwa kwenye makubaliano.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, mshtakiwa Rugemalira alikubaliana na uamuzi wa kwenda Mahakama Kuu na kuomba apatiwe nakala za hukumu hiyo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 21.
Awali Jamhuri katika majibu yao waliiomba mahakama itupilie mbali maombi hayo kwa sababu yamewasilishwa wakati si mwafaka na mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri kama ambavyo mshtakiwa anaomba. Rugemalira aliomba DPP amwondoe katika kesi ya uhujumu uchumi ili awe huru wasaidiane kutafuta Sh trilioni 41 za Serikali.
Katika barua za Rugemalira kwa mahakama, anadai kwamba amemtaka Gavana wa Benki Kuu atoe orodha ya waliopewa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow ili yeye asafishike kwa sababu hajalipwa hata senti moja kutoka katika akaunti hiyo.
Mshtakiwa huyo alidai katoa notisi kwa taasisi nyeti tisa akitaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini amwondoe kwenye kesi ya uhujumu uchumi, asipofanya hivyo atawasilisha hoja rasmi za kuondolewa katika kesi hiyo.
Miongoni mwa taasisi alizopeleka notisi ni ofisi ya DPP kwa Biswalo Mganga, DCI Robert Boaz, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkurugenzi wa Takukuru, Gavana wa Benki Kuu, Kamishna TRA, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Clement Mashamba na Kamishna wa Magereza.
Rugemalira alidai kuna barua alimwandikia Gavana wa BoT akieleza kwamba hajawahi kulipwa hata senti moja kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha.
Miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika Jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mwanasheria Makandege anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000.