*Msaidizi wa IGP afariki dunia kwa mafuriko
NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA
GERALD Ryoba ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu, amefariki dunia na familia yake baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na mafuriko mkoani Dodoma jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, aliwambia waandishi wa habari jana, kwamba tukio hilo lilitokea eneo la Kibaigwa mjini hapa.
Alisema kwamba, Ryoba na familia yake, walikuwa wakitoka mkoani Geita wakielekea jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T 516 DEP aina ya RAV 4 lililokuwa na watu sita.
Kamanda Misime aliwataja waliokuwa katika gari hilo, kuwa ni Ryoba mwenyewe, watoto wake ambao ni Gabriel Gerald Ryoba, Godwin Gerald Ryoba na mkewe, Fidea Kiondo.
Wengine ni dereva wa gari hilo ambaye ni askari polisi mwenye namba F 3243, Koplo Ramadhan na msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sara ambaye ni mwenyeji wa Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma.
“Tukio hilo lilitokea jana, saa tatu usiku katika eneo la Kibaigwa linalojulikana kwa jina la bwawani wilayani Kongwa.
“Polisi tulipata taarifa, kuwa kuna maji mengi yanapita katika eneo hilo na yamesababisha magari kushindwa kupita kwani yalikuwa yakitiririka kutoka maeneo ya Njoge na Hembahemba.
“Polisi wetu walipokwenda eneo la tukio, waliambiwa kuna gari limesombwa na maji hayo na gari hilo lilikuwa limezama na yalikuwa yakionekana matairi tu.
“Kwa hiyo, kilichofanyika, askari walizuia magari yasipite hadi maji yalipoanza kupungua ndipo wakaruhusu magari yaanze kupita,” alisema Kamanda Misime.
Pamoja na hayo, alisema walianza kuitafuta gari hiyo na ilipofika usiku wa manane, walifanikiwa kuipata huku kukiwa na watu wawili waliokuwa wamepoteza maisha.
“Baada ya kukata lile gari maana lilikuwa limepondeka, tukafanikiwa kutoa mwili wa Fidea John Kiondo ambaye ni Mwalimu wa Manispaa ya Temeke ambaye ni mke wa Mkaguzi wa Polisi, Gerald Ryoba ambaye ni Msaidizi wa afande IGP,”alisema Kamanda huyo.
“Kwa kuwa tuliambiwa kwenye gari hilo kulikuwa na watu wengine sita, polisi waliendelea na harakati za kutafuta miili mingine ambapo tulifanikiwa kupata mwili wa dereva wa gari hilo mwenye namba F 3243, Koplo Ramadhan ambaye naye alifariki dunia.
“Tuliendelea kutafuta na baadaye tukampata mtoto wa miaka mine, Gabriel Ryoba na hatimaye tukapata mwili wa Godwin Ryoba na mwishoni mwili wa mkaguzi huyo wa polisi ulipatikana jana saa nne asubuhi.
“Kwa hiyo, watu wote sita waliokuwa kwenye gari hilo, tulifanikiwa kuwapata, lakini wakati tunaendelea kutafuta kwenye mkondo huo wa maji, tumefanikiwa kupata miili mingine miwili na hivyo kuwa na miili minane,”alisema Kamanda huyo.
“Kati ya miili hiyo mingine miwili, mmoja umetambulika kwa jina la Ludege ambaye ni Ofisa Mifugo, Kata ya Pandambili, Kongwa na mwingine haujafahamika.
“Kwa hiyo, tumeacha taarifa kwa wananchi mbalimbali inaonekana hayo maji yameanzia mbali na yalikuwa mengi sana na inawezekana kuna watu wengine pia wamesombwa.
“Kwa hiyo, tumewaambia wananchi kama wataona mwili wowote, watupatie taarifa haraka ili tukatoe msaada,” alisema.
Akizungumzia miili ya marehemu, alisema wanajiandaa kuisafirisha kwa ajili ya mazishi.
“Huyo koplo ambaye alikuwa ni dereva, ni mwenyeji wa Lindi na msaidizi wa afande IGP ni mtu wa Geita. Hivyo basi, tunatarajia kuisafirisha miili hiyo yote kwa ajili mazishi katika maeneo husika,” alisema Kamanda Misime.