Na RATIFA BARANYIKWA-DAR ES SALAAMÂ
MIONGONI mwa wanadiplomasia wachache na wanausalama mahiri waliowahi kutokea nchini, ni pamoja na Balozi Augustine Mahiga ambaye Taifa limempoteza mwishoni mwa wiki hii akiwa jijini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea.
Balozi Mahiga ambaye hadi mauti yanamkuta alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria nafasi aliyobadilishiwa Machi 3 mwaka 2019 baada ya Rais Magufuli kumtoa Wizara ya Mambo ya Nje alikohudumu tangu mwaka 2016.
Umoja wa Mataifa, Balozi za Canada, Sweden, Ufaransa, China na baadhi ya viongozi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania wametoa salamu wakimlilia Balozi Mahiga.
Wanasiasa wakiwamo wa wale wa upinzani nao wameonekana kumzungumzia vizuri Balozi Mahiga na wengine wakienda mbali na kumwelezea kwamba alikuwa ni tofauti na wabunge wengine wa CCM hali kadhalika mawaziri.
Balozi Mahiga mbali na kuwa sifa ya mwanadiplomasia mahiri aliyefanya kazi za kimataifa kwa miaka mingi pia amelitumikia taifa katika nafasi nyingine nyingi nyeti ikiwamo ile ya Ukurugenzi wa Usalama wa Taifa.
Amepewa heshima hiyo si tu kwa sababu umahiri wake katika eneo la diplomasia au uzoefu mkubwa na nafasi nyeti alizowahi kushika ndani na nje ya Tanzania, bali kile kilichotajwa na wengi, unyenyekevu na kutopenda kujikweza .
Hilo limeonekana wazi katika ujumbe uliotolewa na si tu na wanasiasa bali na makundi mbalimbli ya watu, wakiwamo wale waliozungumza na gazeti hili.
Hata Rais Magufuli mwenyewe amethibitisha hilo kupitia taarifa ya Ikulu aliyoitoa juzi baada ya kifo chake.
“Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa, marehemu Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu nilomtuma,” ameeleza Rais Magufuli katika salamu zake za rambirambi.
“Leo taifa limepoteza mtu mwema mbobezi diplomasia, rafiki yangu na baba yangu Mzee Mahiga nakulilia sana, tulikuwa wote bungeni tofauti na wabunge na mawaziri wengi wa CCM ulitambua hotuba yetu ukasifu uwezo na ushauri wetu,” ameandika mbunge wa Chadema John Heche kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Balozi Augustine Mahiga licha ya kutajwa mwanadiplomasia mahiri kuwahi kutokea Tanzania, akionekana kama mtu mpole, uamuzi wa Rais Magufuli kumuhamisha wakati huo ulikuja wakati uhusiano wa Tanzania na baadhi ya nchi za magharibi ukionekana kuanza kutetereka.
Balozi Mahiga ambaye alizaliwa Agosti 28 mwaka 1945 akiwa na miaka 74, historia inaonyesha mbali na kushika nyadhifa hizo katika Serikali ya Rais John Magufuli huko nyuma baada ya kutoka kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975 na kuhamia ofisi ya Rais na kisha kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa pia ameiwakilisha Tanzania Umoja wa Mataifa na nchi mbalimbali kwa muda mrefu.
Pia alikuwa Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ofisi ya siasa kwa Taifa la Somalia kutoka mwaka 2010 hadi 2013.
Desemba mwaka 2015 baada ya Rais John Magufuli kushinda kinyang’anyiro cha urais alimteua kuwa mbunge na alipoteua baraza lake la mawaziri alimtangaza Balozi Mahiga kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Balozi Mahiga ni miongoni mwa watu wachache ambao wamepata kufanya kazi ngazi za juu katika awamu zote tano za serikali kuanzia kwa Rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi sasa Rais Dk. John Magufuli.
ALIVYOTINGISHA URAIS 2015
Mwaka 2015 Mahiga alikuwa ni miongoni mwa wananchama wa CCM ambao walichukua fomu ya kuwania urais katika kinyang’anyiro ambacho Magufuli aliibuka na ushindi.
Hatua yake ya kuchukua fomu ya kuwania urais ndani ya CCM akibebwa na haiba yake ya diplomasia lakini pia ile ya kucheza karata zake sawasawa pasipo kuonekana kumdhuru yeyote licha ya kubobea katika kazi ya usalama, Dk. Mahiga alionekana kuwatikisa wenzake waliotia nia ya kuwania nafasi hiyo.
Wengine walijenga hisia kwamba huenda alikuwa ametumwa na wengine walidhani kwamba yalikuwa ni malengo yake mwenyewe.
Licha ya upepo kuvuma upande wa Magufuli huku wagombea wengine walioonekana kuwa na nguvu kubwa kama aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa wakihamia upinzani, Balozi Mahiga hata baada ya jina lake kukatwa katika hatua za awali za kinyang’anyiro hicho alibakia kimya.
Yeye, Jaji Augustino Ramadhan ambaye wamepishana siku tatu tu kuondoka duniani walishiriki mbio hizo na kuacha maswali mengi hasa ukizingatia huko nyuma wamepata kuwa watumishi serikalini.
MAISHA YAKE BINAFSI/KAZIÂ
Mahiga ambaye alikuwa ameoa na kubarikiwa watoto watatu mwaka 1971, alitunukiwa shahada ya Ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka huo huo inaelezwa Mahiga alimaliza shahada yake ya uzamili katika masuala hayo hayo ya sanaa katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada na baadae mwaka 1975 alipata shahada udaktari wa uhusiano wa kimataifa kutoka katika chuo hicho hicho.
Mahiga aliwahi pia kufundisha kama Mhadhiri Mwandamizi wa Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1975 hadi 1977.
Baada ya hapo alihamia katika ofisi ya rais Ikulu akiwa kama Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo.
Kutoka mwaka 1980 hadi 1983 akapandishwa kazi katika ofisi hiyo ya rais na kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Pia kwa vipindi tofauti katika utumishi wake amekuwa mhadhiri mtembezi katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam.
SAFARI YA DIPLOMASIA
Kwa kipindi cha miaka 30 kutoka mwaka 1983 hadi 2013 Balozi Mahiga alifanya kazi ya diplomasia akiiwakilisha nchi yake kama balozi na pia kuwakilisha Umoja wa Mataifa (UN) katika nchi mbalimbali.
Kwa miaka sita kutoka 1983 hadi 1989 alikuwa balozi wa Tanzania nchini Canada na 1989 hadi 1992 akahudumu katika ubalozi wa kudumu wa Tanzania katika ofisi za UN jijini Geneva, Uswizi.
Kutoka mwaka 1992 hadi mwaka 1994 alihudumu kama mwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi UNHCR nchini Liberia.
Kutoka mwaka 1994 hadi 1998 alirudi Geneva na kuwa mratibu na mkurugenzi msaidizi wa Operesheni za Dharura za Wakimbizi katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.
Inaelezwa katika kipindi hicho kulikuwa na vita zilizoangamiza maisha ya maelfu ya watu na kuzalisha mamia ya wakimbizi kutoka nchi za Rwanda, Burundi na DRC.
Kutoka 1998 hadi 2002 alikuwa mwakilishi mkaazi wa UNHCR India, na kutoka 2002 hadi 2003 akawa mwakilishi wa Shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na San Marino.
Mwaka 2003 akateuliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuwa Balozi wa Tanzania katika Ofisi za Kudumu za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York na kusalia katika nafasi hiyo katika muhula wa kwanza wa rais wa nne wa Tanzania Jakaya Kikwete hadi 2010.
Mwaka 2010 akateuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN kipindi hicho Ban Ki-moon kuwa mwakilishi wake maalum kwa Somalia nafasi ambayo alihudumu mpaka Juni 2013.