32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

RITA yaja na mapendekezo sheria ya ufilisi

emmy hudsonNa Mwandishi Wetu

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) inakusudia kufanya marekebisho makubwa ya kimfumo, baada ya kuja na mependekezo yanayolenga kuwapo kwa sheria ya ufisili.

Hatua hiyo inatajwa kuwa itawaweka mahala pagumu baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, kampuni na mashirika ya kimataifa yanayotangaza kufilisika kwa njia za ujanjaujanja.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RITA, Emmy Hudson  alisema hadi sasa hakuna sheria mahsusi inayosimamia na kuratibu shughuli za ufilisi.

“Kutokana na kukosekana kwa sheria hii, tumeandika andiko tumelipeleka wizarani kwetu (Wizara ya Katiba na Sheria) ambako tunaamini utaandaliwa muswada kwa ajili ya kupelekwa bungeni, ili marekebisho ya sheria yaweze kufanywa.

“Tuna upungufu kwenye sheria ya makampuni na ufilisi, tunashindwa kuchukua hatua kwa makampuni ya nje yenye matawi yake hapa nchini pindi yanapotangaza kufilisika,” alisema Hudson.

Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana mpaka sasa hakuna utaratibu wa kisheria unaoipa mahakama mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusu ufilisi wa makampuni ya nje.

“Naamini kama andiko letu litafanyiwa kazi ipasavyao, sheria mpya itaweka misingi na taratibu za ufilisi wa makampuni ya nje yenye matawi yao hapa nchini…ule mchezo wa kukwepa kodi utaisha.

“Sheria itaweka utaratibu utakaoipa mahakama mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusu ufilisi wa makampuni ya nje yenye matawi hapa nchini,”alisema Hudson.

Alisema sheria  zilizopo hazitoi kipuambele  cha malipo kwa wafanyakazi wakati na baada ya ufilisi, lakini ujio wa sheria mpya utasaidia kutoa kipaumbele cha malipo wakati na baada ya ufilisi kwa kuweka sharti  la wafanyakazi kulipwa kwanza kabla ya wadeni wengine.

“Katika eneo hili, wafanyakazi wengi wamekuwa wakiumia, makampuni ya nje yakija hapa kwetu yanafungua biashara zao, mwisho wa siku wanatangaza kufilisika wanaoumia ni wafanyakazi wazalendo…hili tumeliona tunaamini mabadiliko ya sheria yataondoa kabisa kilio cha watu wetu…hatupendi kuona wanakuja wanavuna  kisha wanaondoka,”alisema Hudson.

Alisema umefika wakati wa kuwa  na sheria moja ambayo itasimamia taasisi zote, tofauti na sasa ambako kila mmoja inajisimamia yenyewe.

“Tungekuwa na mfumo wa sheria moja inayosimamia masuala haya naamini tungekuwa mbali, hivi sasa kila taasisi ina sheria zake hata wenzetu wa Brela (msajili wa makampuni), kimsingi wanaotekeleza jukumu la ufilisi ni wanasheria na wahasibu waliosajiliwa.

Alisema mabadiliko ya sheria hiyo, yanatokana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia mwaka 2010, ambapo Tanzania ilikuwa ya 126 lakini mwaka 2014 iliporomoka hadi nafasi ya 146 kati ya nchi 189 duniani.

“Takwimu hizi zinaonyesha wazi ipo kila sababu ya kupitia upya mfumo wetu tulionao kuhusu ufilisi. Wenzetu wa Kenya, Singapore,Uingereza  na Malaysia wamefanikiwa katika hili,”alisema Hudson.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles