24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Watatu wapandishwa kizimbani kwa ubadhilifu wa fedha

Derick Milton, Simiyu

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafikisha mahakamani watumishi watatu wa halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh. milioni 24.9.

Watumishi hao ni pamoja na Ofisa Ardhi wa halmashuari hiyo, Magesa Magesa, mhasibu msaidizi, Augustina Kitau na Fundi Mchundo, Jackson Mahendeka ambapo walisomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mary Nyangusi.

Akisoma Mashtaka yao mbele ya hakimu huyo Wakili wa serikali, Tawabu Yahaya alielezea mahakama kuwa washitakiwa hao wanatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za mradi wa upimaji wa viwanja wilayani humo.

Katika shtaka la kwanza, Wakili Tawabu alisema kuwa kati ya Juni 04 na Septemba 30 mwaka jana, katika eneo la Nyashimo wilayani humo washtakiwa wote kwa pamoja waliandaa hati ya malipo ya uongo na kufanikiwa kulipwa kiasi hicho cha pesa kinyume cha sheria kifungu namba 333,3335(d)(i) na 337 vya kanuni ya adhabu.

Katika Shtaka la Pili, wakili Tawabu alielezea Mahakama hiyo kuwa kati ya tarehe hizo watuhumiwa wote kwa pamoja walifanya udanganyifu kwa kutumia hati ya malipo namba 473116V1902668 iliyokuwa na kiasi cha Sh. milioni 42,524,000 ambapo kati ya fedha hizo Sh. milioni 24,974,000 zilikuwa ni malipo hewa kinyume na sheria namba 342 na 337 vya kanuni ya adhabu.

Washtakiwa hao walikana makosa hayo na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa wa serikali watakaosaini dhamana ya Sh. milioni 10 kila mmoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria ili kupata dhamana.

Mshtakiwa wa kwanza alifanikiwa kupata dhamana lakini mshtakiwa wa pili na wa tatu walikosa dhamana baada ya kushindwa kukidhi vigezo vilivyotolewa na mahakama.

Kesi hiyo namba 57 ya mwaka 2020 imeahirishwa hadi itakaposomwa tena Mei, 04.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles