29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Tahadhari corona

WAANDISHI WETU – DAR/MIKOANI

KASI ya virusi vya ugonjwa wa corona inazidi kuenea huku Watanzania wakitakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kama njia ya kuepuka maambukizi hayo.

Jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza ongezeko la wagonjwa wa corona baada ya watu wengine wawili kuthibitishwa Visiwani Zanzibar na Dar es Salaam ambao  wote ni raia wa kigeni.

Hiyo inakuja siku moja baada ya juzi kutangaza kufungwa kwa shule zote kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini.

Serikali imethibitisha hayo baada ya wagonjwa hao wawili kufanyiwa vipimo vya maabara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Alisema sampuli ya kwanza ni ya mwanaume, raia wa Marekani, 61 ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam.

Mgonjwa huyo ametengwa katika sehemu maalumu kwa taratibu nyingine za kitabibu, pia ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu naye.

Zanzibar kwa upande wake imesema sampuli ya pili iliyopokelewa ni ya mwanaume mwenye umri wa miaka 24, raia wa Ujerumani.      

WATU 27 WASUBIRI VIPIMO

Kutokana na kile kinachoonekana kuendelea kudhibiti maambukizi hayo ya corona, Serikali imesema kuwa sampuli za watu 27 wanaodaiwa kushirikiana kwa namna moja ama nyingine na mgonjwa wa kwanza wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, Isabela Mwampamba (46), zimetumwa Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dar es Salaam.

Majibu ya sampuli hizo yanatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa.

Isabela ambaye ni mmiliki wa shule binafsi ya Upendo Friends iliyopo jijini Arusha, anaendelea na matibabu katika eneo maalumu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  alisema hadi sasa katika Mkoa wa Arusha, watu hao 27 wakiwemo waliokuwamo katika hoteli aliyofikia Isabela wako chini ya uangalizi maalumu.

“Kwa upande wa Arusha sasa hivi tunafuatilia watu 27 ambapo leo (jana) wako siku ya tatu na maendeleo yao ni mazuri, hivyo kuanzia sasa wakati wowote majibu ya sampuli yatatolewa,” alisema Ummy.

IDADI YA WAGONJWA

Alisema hadi kufikia jana wamethibitisha uwepo wa virusi hivyo kwa wagonjwa wawili baada ya kufanyiwa vipimo vya maaabara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii Dar es Salaam.

“Sampuli ya kwanza ni  hiyo mwanaume raia wa Marekani (61), mkazi wa jijini Dar es Salaam na amewekwa mahali maalumu kwa ajili ya taratibu nyingine za kimatibabu ikiwemo  kufanya ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu naye.

“Baada ya kushauriana na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamad Rashid, napenda kutangaza sampuli ya pili iliyofanyiwa vipimo na kuthibitisha uwepo wa virusi hivyo iliyopokelewa kutoka Zanzibar ni ya mwanaume (24) ambaye ni raia wa Ujerumani.

“Muhimu kila mmoja wetu kuzingatia maelekezo ya kujikinga ugonjwa huu yanatolewa mara kwa mara, hivyo kwa sasa tuna wagonjwa watatu wenye maambukizi ya virusi hivyo,” alisema Ummy.

Hata hivyo taarifa ya Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid ilisema mgonjwa huyo ni raia wa Ghana aliyeingia Zanzibar akitokea Ujerumani. 

MAABARA KUWA MOJA

Ummy alisema tangu wametangaza kisa cha kwanza cha mgonjwa wa corona nchini, kumekuwa na maswali kwanini sampuli zote zinapelekwa Maabara ya Taifa, Dar es Salaam.

“Ufafanuzi ni kwamba kirusi hiki kinapimwa katika maabara maalum ambapo kuna ngazi, kwa nchini ni maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii tu ambayo iko ngazi ya tatu katika upimaji wa sampuli wa virusi ambavyo vina hatari ya kuambukiza kwa kiasi kikubwa

“Kama mlikuwa mnafuatilia kabla ya Februari 15, barani Afrika, Kusini mwa Sahara, ilikuwa na maabara mbili tu ambazo zilikuwa na uwezo wa kupima kirusi hiki cha corona, maabara ya Afrika Kusini na Senegal.

“Hata sisi tumefanya kazi kubwa ya kuhakikisha maabara yetu inakuwa na uwezo wa kupima sampuli, kupitia jukwaa hili niwatoe wasiwasi Watanzania tuliweka mipango sampuli ikichukuliwa inasafirishwa vipi, tumeshasaini mikataba pia jinsi ya kusafirisha sampuli,” alisema Ummy.

Alisema hata wakati wa tishio la ebola, sampuli zote zilikuwa zinapelekwa Dar es Salaam na kuwa katika mlipuko wa corona kuna vipimo vya kupima haraka – ‘rapid test’, ambavyo ni vya awali na wameshaandaa utaratibu wa kuhakikisha wanavipata kwa haraka ili kusambaza katika maabara za ngazi ya mikoa.

VITUO VYA AFYA

Ummy amevitaka vituo vyote vinavyotoa huduma za afya hususani binafsi kuhakikisha wanapokuwa na mshukiwa watoe taarifa kwa mamlaka husika na kila mkoa kuna timu ya dharura.

“Tumeona kwa Dar es Salaam kila mgonjwa anaambiwa nenda Muhimbili akiwa na mafua. Kuna kitu kinaitwa ‘standard case definition’, siyo kila mwenye mafua, homa au kikohozi basi ni mshukiwa wa corona, hiyo inasababisha kutoa mzigo kwa mfumo mzima wa utoaji huduma za afya.

 “Vituo vya Serikali na binafsi vizingatie miongozo iliyotolewa na wizara kuhusu hatua za kupeleka wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona,” alisema Ummy. 

MGONJWA AOMBA RADHI

Akizungumzia hali ya mgonjwa wa kwanza, Isabela, Waziri Ummy alisema anaendelea vizuri na kuwa aliwasiliana naye asubuhi hana kifua, kikohozi, wala homa na amekuwa akijipima homa mara tatu kwa siku.

 “Sasa hivi Isabela anaendelea vizuri na yupo tayari kutoa elimu na taarifa zaidi kwa wananchi juu ya kujikinga kwani tumeona watu wameanza ku-panic na kuwa na hofu na kutoa taarifa nyingi za uongo ambazo hazijathibitishwa,” alisema Ummy.

Aidha alilazimika kumpigia simu Isabela ambaye aliridhia kuwekwa ‘Live’ katika mkutano na wanahabari na aliomba radhi kutokana na kuwa mgonjwa wa kwanza na kuzua taharuki kubwa nchini.

“Nashukuru sana waandishi wa habari na Watanzania wote kwa ujumla, naendelea vizuri. Cha kwanza namshukuru Mungu kwa kunilinda na wananihudumia vizuri.

“Lakini pia nawashukuru Watanzania, ninatamani kusema kwamba ninawaomba msamaha kwa maana kwamba ya kuwa mgonjwa wa kwanza wa corona Tanzania imeleta taharuki nchi nzima na watu wengi wameona kwamba mimi ni kisababishi, niko hapa kuomba msamaha mkubwa.

“Ni jambo limeshatokea, mimi naamini Mungu ataendelea kutuponya. Natamani nitoe ujumbe huu kwa Watanzania tutumie wakati huu kuelimishana ugonjwa ukoje na siyo kukuza jambo kwani ni ugonjwa uko duniani kote, kwani hofu ni kubwa zaidi ya corona,” alisema Isabela.

KITENGO MAGONJWA YA MLIPUKO

Awali Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Udhibiti na Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Milipuko, Dk. Janneth Mghamba, alisema timu ya taifa iliwasili mkoani Arusha  kushirikiana na mkoa huo kufanya ufuatiliaji kwa mgonjwa wa kwanza.

Alisema kwa sasa wanafuatilia watu hao 27 waliokuwa naye karibu na wamefanya mawasiliano na wanaendelea vizuri na wataendelea kuwepo mkoani Arusha ili kuweka mikakati ugonjwa usisambae zaidi.

“Mgonjwa anaendelea vizuri sana, hana homa kwa sababu dalili kubwa tunazoangalia ni homa, kukohoa na kubanwa na mbavu na tumechukua sampuli za waliokuwa karibu naye na mrejesho tutatoa tukimaliza,” alisema Dk. Mghamba.

Akizungumzia matumizi ya kujikinga vikiwemo vitakasa mikono (sanitizer) na vile vya kuziba pua na mdomo, alisema vifaa hivyo vinatakiwa kuvaliwa maeneo yenye msongamano wa watu badala ya kuvaliwa kama vinavyovaliwa sasa na baadhi ya watu.

“Mask zinavaliwa na tafiti zimeonyesha inavaliwa na mtu mwenye maambukizi kusudi asimwambukize mwingine, ila pia zinaweza kuvaliwa kwenye maeneo yenye msongamano.

 “Lakini kwa sababu Serikali imepiga marufuku msongamano, hatutegemei kukuona wewe unavaa mask unapita sehemu ambayo hakuna msongamano,” alisema Dk. Mghamba.

ATHARI ZA MASK

Akizungumzia athari za mask, Dk. Mghamba alisema kuwa inaweza kuwa kubwa kwani watu wegi bado hawajui kama zinatakiwa kubadilishwa kila baada ya saa nne.

“Ukikaa nayo siku nzima ni hatari, inaweza kukuletea athari zaidi,” alisema Dk. Mghamba.

MUFTI AFUNGA MADRASA

Katika kile kinachoonekana kuchukua tahadhari na kudhibiti kasi ya maambukizi ya corona, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir, amewataka walimu wa madrasa  zote nchini  kuzifunga ili kuepusha kuenea kwa virusi  hivyo.

Pamoja na hali hiyo amewataka Waislamu waliopo kwenye maeneo yanayoshukiwa  kuwa na wagonjwa wa corona kutohudhuria swala ya Ijumaa na swala zote za jamaa kwa kuwa ni haramu.

Alisema uamuzi huo umefikiwa na kikao cha dharura kilichoketi wiki hii cha Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambacho kilijadili mwenendo wa ugonjwa huo na tabia zake.

Mufti alisema uamuzi wa kufunga madrasa kunatokana pia na agizo la Serikali la kusitisha masomo kwa shule zote kuanzia ngazi za awali hadi vyuo vikuu.

“Tunawaomba waumini wote wa Kiislamu kutekeleza agizo hili kwa lengo la kuokoa nafsi zetu zisiangamie, ni ibada kubwa na mtekelezaji wa amri na maagizo haya atalipwa  thawabu zisizo na kifani,” alisema Mufti Zubeir.

Alisema mamlaka zinazohusika zikitangaza karantini kwa eneo lolote, Waislamu wa eneo hilo wanaruhusiwa na sheria ya Kiislamu kutohudhuria swala ya Ijumaa na swala zote kwani lengo la swala ni kujenga umoja, pia kuleta masilahi na manufaa kwa waumini.

Alisema Muislamu yeyote atakayepatwa na maradhi hayo ni haramu kwake kuhudhuria swala ya Ijumaa na swala za jamaa kama ambavyo ni haramu kwake kuchanganyika na watu wengine kwani kufanya hivyo ni kuisambaza na kueneza ugonjwa huo kwa wenzake.

MPAKA WA NAMANGA

Aidha Waziri Ummy alifanya ukaguzi eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga ambako aliagiza wataalamu wa afya mipakani kote nchini kuwa makini katika kufanya ukaguzi kwa wasafiri wanaopita.

Alisema moja ya dalili kubwa ya magonjwa ya corona ni pamoja na homa kali, hivyo ndiyo maana kipimo hicho hufanyika ila ni muhimu zaidi kuhoji wasafiri kabla ya kuwaruhusu kupita ili kubaini historia ya maeneo waliyotoka.

“Maofisa afya mipakani tunatakiwa tuweke umakini zaidi katika ukaguzi wa wasafiri na watu wanaopita katika maeneo yetu, siyo kuangalia joto la mwili tu. Jana nilikuwa naangalia China, kuna mtu amemeza vidonge vya kushusha homa kusudi aweze kupita, maofisa afya ni wajibu wenu kufanya uchunguzi zaidi,” alisema Ummy.

JET YAFUNGA OFISI

Kutokana na athari ya maambukizi ya virusi vya corona, jana uongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ulitangaza kufunga kwa muda ofisi na badala yake wafanyakazi watafanya shughuli zao wakiwa nyumbani.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru, ilieleza kuwa chama hicho kina  wajibu wa kujikinga na kukinga watu wanaowazunguka pamoja na mazingira. 

“Hivyo basi, tunaomba wanachama wetu mfanye kazi kwa usalama na kwenye mazingira salama. Uongozi umeamua kusitisha kazi/shughuli zote ofisini kuanzia leo, na ofisi itafungwa kwa kipindi kisichopungua wiki tatu. Tutawajulisha kadiri taarifa zitakavyokuwa zinapatikana. 

“Kuna taarifa nyingi zinarushwa kwenye mitandao ya jamii kuhusu Covid-19. Sio dalili zote zitaonekana, na ndio maana tuchukue tahadhari kama ifuatavyo: Osha mikono pamoja na koki ya bomba kila wakati kwa sabuni ya maji na maji safi na salama. Usishike koki, kishikio cha mlango, baada ya kunawa mikono, tumia karatasi, kisha itupe.

“Osha vyombo kwa maji na sabuni, hasa vijiko, vikombe, glasi. Mjitahidi mkiwa kazini kwenye kutafuta habari kuvaa mask, na msiazimane. Ukirudi nyumbani, vua nguo bafuni na uoge kabla hujakaa na familia yako.

“Kama huna sanitizer, tumia kilevi kama whisky, K-Vant, Konyagi n.k kufuta mikono, kalamu, miwani, compyuta. Tumia vifaa vya kazi vyako binafsi na usiazime kwa mtu au kutoka kwa mtu. 

“Iwapo utajisikia uchovu, maumivu kidogo kama malaria, pima uhakiki sio malaria. Kisha kaa nyumbani mara moja na unywe maji kwa wingi kila mara, ili kirusi kishuke na kisiingie kwenye mapafu,” alisema Dk. Ellen.

TMDA YATOA ELIMU

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa mafunzo maalumu kwa watumishi wake ya kupambana na kuzuia corona.

Mafunzo hayo yalitolewa na Ofisa Majaribio na Usalama wa dawa wa mamlaka hiyo, Dk. Alex Nkayamba katika ofisi za TMDA zilizopo Dar es Salaam.

Dk. Nkayamba alieleza kuwa watumishi hao kutoka idara mbalimbali za mamlaka hiyo waliweza kupokea mafunzo na watakuwa mfano na walimu kwa wengine katika maeneo ya kazi na nyumbani.

“Hadi sasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetangaza uwapo wa visa vitatu vya wagonjwa wa corona, ugonjwa huo umekuwa ukienea kwa kasi karibu nchi mbalimbali duniani ambapo tayari mamlaka zimewataka wananchi kuchukua hatua mahsusi za  kujikinga na kuondoa hofu.

“Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuziba mdomo wakati wa kukohoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara ama kwa vitakasa mikono (hand sanitizer) pamoja na kuepuka sehemu zenye mikusanyiko ya watu,” alisema Dk. Nkyamba.

MOROGORO YAJIPANGA

Serikali mkoani Morogoro imetenga moja ya wodi katika Hospitali ya Wilaya ya Morogoro iliyopo Mkundi kuwaweka  karantini wagonjwa wa corona pindi watakapohisi kukumbwa na ugonjwa huo.

Hayo yalibainishwa jana kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Manispaa ya Morogoro kilichowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa halmashauri, viongozi wa dini, watu maarufu, wafanyabiashara na wanahabari.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alisema tahadhari hiyo imechukuliwa na manispaa kuhakikisha wananchi hawapati maambukizi hayo.

Aliagiza kituo kikuu cha mabasi Msamvu, viwandani, hospitali, vituo vya mabasi na kwenye usafiri wa jumuiya kuwekwa huduma ya maji ya kunawa sambamba na kuhakikisha usafi unafanywa kwenye maeneo husika.

HABARI HII IMEANDALIWA NA JANETH MUSHI (ARUSHA), CHRISTINA GAULUHANGA,  AVELINE KITOMARY (DAR ES SALAAM) NA ASHURA KAZINJA (MOROGORO)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles