33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Niyonzima: Sitailipa Yanga chochote

harunaaNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

* Adaiwa sh. milioni 152 kwa kukiuka masharti ya mkataba wake

MCHEZAJI Haruna Niyonzima ambaye mkataba wake umevunjwa na klabu yake ya Yanga kwa kile kilichodaiwa kuchoshwa na tabia zake, amedai kuwa hatalipa kiasi cha Dola 71,175 (sawa na Sh milioni 152) kwani suala hilo halipo kwenye mkataba.

Uongozi wa Yanga jana ulitangaza kuvunja mkataba wa mchezaji huyo mahiri wa nafasi ya kiungo, lakini mbali na uamuzi huo klabu hiyo pia ilimtaka mchezaji huyo kuilipa dola za Kimarekani 71,175 kutokana na kanuni mpya ya  Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) inayotaka mchezaji kufanya hivyo kama mkataba wake utavunjwa kutokana na makosa yake.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Niyonzima alikana kutambua taarifa ya kufukuzwa kwake kwa kudai kwamba alipaswa kupewa barua na uongozi wa klabu hiyo ili aweze kulitambua jambo hilo.

“Suala la kuilipa Yanga fedha halipo katika makubaliano tuliyowekeana kwenye mkataba wangu, siwezi kuwalipa hata senti.

“Halafu suala la kufukuzwa mimi nalisikia mtaani wala sijataarifiwa, ninachotaka ni barua na si maneno mbona nilipopeleka barua leo (jana) sikutaarifiwa jambo hilo iweje wazungumze na vyombo vya habari washindwe kuniambia mwenywe,” alihoji.

Yanga Mei 19 mwaka huu, ilimuongezea mkataba wa miaka miwili Niyonzima ambao ungeisha mwaka 2017 kwa lengo la kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho, ambacho kinatarajia kushuka dimbani Februari mwakani katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Hata hivyo, uamuzi wa kuvunja mkataba wake unaonekana kutoiathiri Yanga, kutokana na kufanya vizuri kwa kiungo mpya mkabaji Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, ambaye hadi sasa anaiongoza vema timu hiyo na kuwa kinara katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 30.

Hata hivyo, Msemaji wa klabu hiyo, Jerry Muro, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya tathmini ya muda mrefu juu ya tabia ya mchezaji huyo.

“Hii ni mara ya nne kwa mchezaji huyo kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo vinavunja sheria ya mkataba wake unaomtaka aheshimu sheria na taratibu za klabu,” alisema Muro.

Alisema Desemba 15 mwaka huu, walimwita mchezaji huyo katika kikao cha Kamati ya Maadili ya klabu ambapo mchezaji huyo alikiri kutenda kosa na kudai kwamba, alitakiwa kuandika barua ya maelezo ambayo ilitakiwa kuwasilishwa Desemba 23 mwaka huu.

“Hadi sasa ninavyokwambia hatujapata barua yake, lakini mchezaji huyu anaonekana katika kumbi za starehe ilhali anaumwa kama anavyodai mwenyewe,” alieleza.

Muro aliongeza kuwa tabia ya mchezaji huyo kutaka kuwa juu ya klabu, ndiyo iliyowafanya wachukue uamuzi huo wa kuvunja mkataba aliodai kuwa utakuwa fundisho kwa wachezaji wengine.

“Tutapinga usajili wowote dhidi ya mchezaji huyo hadi hapo fedha anazotakiwa kulipa zitolewe kwa kuwa tunafanya kila kitu kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.

Pia Muro alidai kwa sasa hawatokubali barua yoyote itakayowasilishwa na Niyonzima kwa kuwa tayari uamuzi umetolewa na viongozi wa klabu hiyo na hauwezi kwenda kinyume.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles