Kulwa Mzee -Dar Es Salaam
MFANYABIASHARA na fundi simu wa Kariakoo wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu, ikiwemo kubadili namba tambulishi (IMEI) za simu za kiganjani kinyume na sheria.
Washtakiwa hao, mfanyabiashara Abdul Nassoro (36) na Saidi Khalifa (30) ambaye ni fundi simu, walisomewa mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Mmbando.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Esther Martine alidai katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kula njama, kutenda kosa la uhalifu kwa kubadili namba tambulishi za simu Februari 27, mwaka huu.
Shtaka la pili wanadaiwa kubadili namba tambulishi na kuweka namba mpya. Inadaiwa tarehe hiyo hiyo na mahali walibadili IMEI ya simu aina ya Tecno na kuwa namba 354213067976598 na 354213067923426.
Katika shtaka la tatu, wanadaiwa kubadili namba tambulishi za simu za mkononi aina ya Tecno kwa kubadili namba yake tambulishi.
Washtakiwa walikana mashtaka, upelelezi haujakamilika, walirudi rumande hadi leo kwa sababu barua zao kwa ajili ya dhamana zilikuwa zinafanyiwa uhakiki.
Mahakama ilitoa masharti ya kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili, mmoja atoke katika ofisi inayotambulika. Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo kwa washtakiwa kudhaminiwa.