24.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Masoko ya madini yaingizia Serikali Sh bilioni 66

Mwandishi wetu -Dodoma

KATIBU Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini Machi mwaka jana, Serikali imekusanya maduhuli ya Sh bilioni 66.57 na kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume ya Madini jana, Profesa Manya alisema tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini hadi Januari mwaka huu, usimamizi wa masoko ya madini umeimarika.

 Alisema katika kipindi hicho madini yaliyouzwa ni kilo  9,237.34 za dhahabu, karati 12,973.14 za madini ya almasi, kilo 20,099.17 za madini ya bati na kilo 514,683.28 za madini ya vito.

Profesa Manya ambaye alizungumza jana jijini Dodoma, alisema kabla ya kuanzishwa kwa soko kuu la dhahabu Geita, ukusanyaji wa mapato ulikuwa wastani wa Sh milioni 599.04 yaliyotokana na wastani wa mauzo ya kilo 101.97 kwa mwezi kwa takwimu za miezi mitano kabla ya kuanzishwa kwa soko.

Alisema baada ya kuanzishwa soko, makusanyo yaliongezeka hadi kufikia wastani wa Sh bilioni 2.39 kwa mwezi yaliyotokana na wastani wa mauzo ya kilo 360.94 zilizouzwa katika kipindi cha miezi 11 tangu soko hilo kuanzishwa Machi mwaka jana.

Profesa Manya alisema kwa kipindi cha Oktoba mwaka jana pekee katika soko kuu la dhahabu Geita, Serikali ilikusanya Sh bilioni 3.6 kutokana na mauzo ya kilo 537.6.

Kwa soko la Chunya Mbeya, Profesa Manya alisema kabla ya kuanzishwa kwake wastani wa Sh milioni 177.96 zilikusanywa kutokana na mauzo ya dhahabu yenye uzito wa wastani wa kilo 29.67  kwa mwezi ikiwa ni takwimu za miezi minne kabla ya kuanzishwa kwa soko.

Alisema mara baada ya kuanzishwa kwa soko hilo Mei, 2019 ndani ya miezi tisa, Serikali ilikusanya wastani wa Sh milioni 961 kutokana na mauzo ya dhahabu kilo 176.24 kwa mwezi.

Awali akielezea uanzishwaji wa masoko ya madini 28 na vituo vya ununuzi wa madini 28, Profesa Manya alisema kuanzishwa kwa masoko ya madini kulitokana na changamoto iliyokuwa inaikabili sekta ya madini kwa kipindi kirefu, hasa ya utoroshaji na biashara haramu ya madini.

Alisema manufaa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, ni pamoja na  kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata bei stahiki za madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles