FRANCIS GODWIN,IRINGAÂ
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema Tanzania haitazuia raia wa China kuja nchini kutokana na kuwa na urafiki wa muda mrefu.
Alisema Wachina wanaokuja nchini, hawakimbii virusi vya ugonjwa Corona kwao, bali wanarejea kuendelea na kazi walizoziacha .
Alisema umakini wa kuwapima umeongezwa maeneo ya viwanja na ndege ,bandari na mipakani ili kuona wageni wanaoingia nchini wanachunguzwa kama wana maambukizi.
Mhandisi Nditiye aliyasema hayo jana, wakati akijibu maswali ya wanahabari mkoani Iringa, baada ya kukamilisha uzinduzi wa mnara wa simu wa Kampuni ya Haloteli katika Kijiji cha Isoliwaya wilayani Kilolo .
Alisema wametengeneza miundombinu mizuri maeneo yote ambayo wageni wanaingia ili kuwabaini kabla ya kuingia nchini .
“Tumeweka utaratibu kuanzia viwanja vya ndege ,bandari hata kwenye stesheni zetu na maeneo mengine kuona hakuna virusi vya Corona vinavyoingizwa nchini maana tunawapima na kuwaweka karantini kwa siku 14 kwa mujibu wa taratibu zinazotakiwa za umoja wa kimataifa,”alisema.
Alisema kumekuwapo na ushirikiano mkubwa na wageni katika utekelezaji wa kazi hiyo.
Alisema Serikali haiweze kuwazuia raia na nchi nyingine duniani Kuja nchini kwani kila mgeni anayetaka kuja nchini anakaribishwa kuja Tanzania .
Katika hatua nyingine,Mhandisi Nditiye amewataka wale wote waliotumia namba zao za vitambulisho za Taifa (NIDA) kuwasajilia marafiki zao laini za simu kujisalimisha kwenye makampuni ya simu ili kufuta usajili huo kabla ya sheria kuchukua mkondo wake .
Hata hivyo ametoa onyo kali kwa vijana wanaosajili laini za simu kwa alama za vidole kuacha kutumia kitambulisho cha NIDA cha mteja kusajili laini zaidi za kuuza .
Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto akishukuru serikali kwa kufanikisha mawasiliano katika jimbo hilo alisema hadi sasa maeneo mengi wananchi wanapata mawasiliano ya simu na vijiji vichache kama Ilambo Kata ya Ibumu ndiko kuna shida ya mawasiliano.