YOHANA PAUL – MWANZA.
KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo ametoa wito kwa wote waliojenga ama wanaoendesha shughuli zao kando ya Ziwa Victoria kuchukua tahadhari kutokana na ongezeko la usawa wa maji wa ziwa hilo unaokadiliwa kufikia mita 1134. 28 kwa kuwa inaweza kusababisha uharibifu wa mali zao na hata kuhatarisha maisha yao.
Profesa Mkumbo, alitoa wito huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akihitimisha ziara yake mkoani Mwanza iliyolenga kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maji inayosimamiwa na Wakala wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) sambamba na kuhudhuria jukwaa la Wadau wa Bonde la Maji la Ziwa Victoria (LVBWB).
Alisema kwa mujibu wa vipimo vilivyochukuliwa Machi 4, mwaka huu inaonyesha ongezeko la usawa wa maji ziwa victoria limevunja rekodi ya mwaka 1965 ambapo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kushuhudia ongezeko kubwa la usawa wa maji kwenye ziwa hilo.
Alisema ongezeko la hilo la usawa wa maji huenda likazidi kukua kadri siku zinavyojongea kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambazo kwa namna tofauti zimeonyesha uwepo wa mvua nyingi zinazotarajiwa kuendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali Mwanza, ikiwa mojawapo.
“Tunaposikia taarifa kama hizi za ongezeko la usawa wa maji ziwa victoria ni wajibu wa kila mwananchi aliyejenga kando ya ziwa au wale wanaoendesha shughuli zao kando kando ya ziwa kuchukua tahadhari mapema, ikiwamo kuangalia namna ya kuhamisha shughuli zao kutoka maeneo hayo ili kuepuka hasara inayoweza kujitokeza.
“Natoa wito kwa wakala wa maji kutekeleza miradi yake kwa kuzingatia vipimo halisi vya ongezeko hili, usawa wa maji utakapopungua isiwe na athari kwa huduma za maji kwa wananchi wetu na badala yake umakini utumike na ongezeko hili pia lisisiwe kikwazo cha huduma ya maji.
“Pia niwakumbushe wananchi wote hasa wamiliki wa mahoteli kujenga majengo yao kwa kuzingatia sheria ambazo zinataka ujenzi wa majengo uanze mita 60 kutoka chanzo cha maji ikiwemo mito na ziwa ili kuepusha na changamoto kama hizi, tunazozishuhudia ambapo hadi sasa baadhi ya wamiliki wa mahoteli jijini mwanza waliojenga kando ya ziwa tayari wameanza kulazimika kujenga kingo ili kuzuia maji yanayozidi kusogea,” alisema Prof.Mkumbo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) Mkoa wa Mwanza Warioba Sanya, mbali na changamoto iliyopo sa hivi ya ongezeko la usawa wa maji ziwa victoria alimhakikishia Profesa Mkumbo kuendelea kutumia vizuri bajeti ya maji iliyotengwa mkoani mwanza ikiwemo kiasi cha Sh bilioni 1.5 kilichotolewa kwa kila wilaya kulenga kutatua kero ya maji ambapo fedha hizo zinatarajia kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi wapatao milioni 1.5 mkoani hapa.
Mkurugenzi wa Raslimali za Maji LVBWB alisema hadi sasa Tanzania ina bahati ya kuwa na maji ya kutosha ambapo inakadiriwa kuwa na kiasi cha kilomita za ujazo 25,000, ikiwemo maji yanayopatikana ziwa Victoria ambalo litatajwa kuongezeka usawa wa maji hivyo iwapo maji haya yatatumika kwa mipango mizuri yanaweza kuwa na tija na kuchangia kuinua uchumi wa taifa lakini vinginevyo yatabaki kuwa hasara.