SERIKALI imesema watu 631 mkoani Mwanza wameugua ugonjwa wa kipindupindu kati ya Januari hadi Desemba 15, mwaka huu ambapo kati yao 19 wamefariki dunia.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo wakati akizungumza na madiwani pamoja watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu wiki iliyopita.
Wakati Mulongo akitoa takwimu hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Lwakyendera Onesmo aliliambia MTANZNAIA jana kwamba wagonjwa wapya wameendelea kuripotiwa na 14 wamelazwa katika wilaya za Magu, Sengerema na Nyamagana.
Dk. Lwakyendera alisema licha ya kuwapo mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo, lakini kumekuwapo na ongezeko la wagonjwa wapya ndani ya mwezi huu ambapo Desemba 25 kulikuwa na wagonjwa watano.
“Desemba 26 mwaka huu wagonjwa wapya waliongezeka kutoka watano na kufikia 11 na hao ni kutoka wilaya za Nyamagana, Sengerema na Magu, sasa leo tunapozungumza na wewe wamefikia 14.
“Kambi za wagonjwa hao zipo Wilaya ya Nyamagana katika Zahanati ya Igoma, Sengerema ipo kule Kahunda na Magu imewekwa Kisesa, tatizo la ugonjwa huu ni watu wengi kuishi milimani pamoja na kutokuwa na vyoo bora wao wanachimba vishimo vidogo vidogo,”alisema Dk. Lwakyendera.
Mganga mkuu huyo alisema kutokana na hali hiyo wameunda timu iliyoshirikisha sekta mbalimbali ili kupambana na ugonjwa huo na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaishi mazingira ya usafi na kufuata kanuni za usafi.
Awali, Mulongo alisema wastani wa wagonjwa wapya 15 walikuwa wakiugua kwa siku katika vipindi tofauti ambavyo ugonjwa huo ulikuwa ukilipuka katika wilaya saba za mkoa wa Mwanza.
Aidha Mulongo aliagiza madiwani wote pamoja na mkurugenzi kuiagiza kamati ya afya kupita mitaa yote na kuhamasisha wananchi kuzingatia afya.
“Ile hospitali ya wilaya haipo katika mazingira ya kuwahudumia wananchi, kwanza ni chafu na haina baadhi ya huduma, naomba wahusika wote wakiwamo waganga wa wilaya na hospitali mjiangalie sana, asiyetaka kubadilika ajiandae kuuza nyanya mitaani,”alisema.