Aveline Kitomary – Dar es Salaam
ZAIDI ya Madaktari Bingwa 50 wa mifupa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwemo Tanzania, wamepewa mafunzo ya upasuaji mifupa ya unyayo na kifundo cha mguu kwa njia ya kisasa zaidi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yalitolewa na Taasisi ya Mifupa (MOI) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Madaktari Bingwa cha COSECSA na Chama cha Madaktari wa Mifupa nchini Uingereza (BOFAS).
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface, alisema taasisi hiyo imekuwa ikiwapatia wataalmu wake mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa lengo la kuwapa mbinu mpya ili waendane na mabadiliko ya teknolojia ya matibabu yanayobadilika kwa kasi duniani.
“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya hususani kwenye Taasisi ya MOI, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha wataalam wanapata mbinu za kisasa zaidi ili waweze kuwahudumia wagonjwa vizuri na kupata matokeo bora hivyo tunaendelea kuweka msisitizo kwenye mafunzo,”alisema Dk Boniface.
Pai alisema Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kuwapeleka wataalam nje ya nchi ili kupata mafunzo hayo hivyo kuleta wataalam nchini kumeweza kuokoa fedha nyingi kwa nchi na nchi zingine.
Kwa upande wake mkufunzi mratibu wa mafunzo hayo kutoka MOI, Dk Samwel Nungu, alisema washiriki wa mafunzo hayo wametoka katika nchi za Tanzania, Sudan, Zambi na Zimbabwe huku lengo likiwa ni kuongeza ujuzi wa juu zaidi kwa Afrika.
“ Lengo letu ni kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuongeza idadi ya wataalmu hivyo tumekuwa tukiendesha mafunzo hayo kwa kuleta wataalam kutoa mafunzo hapa nchini badala ya kutumia gharama kubwa kuwapeleka wataalam kupata mafunza bara la Ulaya na Marekani,”alibainisha.
Naye mkufunzi kutoka nchini Uingereza Dk Rick Brown alisema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kutoa huduma bora na za kisasa za matibabu ya mifupa hivyo ni furaha yao kuona Afrika inafanya vizuri katika matibabu.