Elizabeth Hombo-Dar Es Salaam
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florence Luoga, amesema kiwango cha fedha katika mzunguko wa fedha, kimekuwa ni cha kuridhisha ambacho kinaweza kutosha kwa miaka mitano ijayo.
Kutokana na hilo, alisema uchumi umekaa vizuri na kwamba wana akiba ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 500.
Profesa Luoga alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu fedha.
“Uchumi umekaa vizuri tuna akiba ya kutosha ya zaidi dola za Marekani bilioni 500, kwa maana hiyo, kiwango cha fedha katika mzunguko kimekuwa cha kuridhisha kwa kigezo cha Benki Kuu (clearing balances).
“Kupitia vikao maalumu vya kila siku asubuhi, Benki Kuu tunaangalia hali ya kila benki na endapo kuna benki ina upungufu wowote tunaisaidia kwa kutumia nyenzo zilizopo kulingana na kanuni,”alisema.
NOTI CHAKAVU
Akizungumzia kuhusu noti zisizokidhi ubora (chakavu) katika mzunguko wa fedha, aliyataka mabenki kuhakikisha fedha isiyokidhi ubora inarudishwa BoT na kubadilishwa fedha safi inayokidhi ubora.
“Kuna kipindi imetokea kuwepo kwa noti zisizokidhi ubora yaani chakavu katika mzunguko wa fedha. Benki Kuu ina sera ya sarafu safi (clean money policy), ambayo lengo lake ni kuhakikisha kuwa fedha iliyoko katika mzunguko ni safi.
“BoT inayaasa mabenki kuhakikisha pesa isiyokidhi ubora inarudishwa BoT na kubadilishwa na fedhaa safi inayokidhi ubora.
“Kwa upande wa wananchi, ifahamike kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kutunza vizuri fedha ili isichakae. Hii itasaidia kupunguza gharama za uchapishaji wa noti kwa kufidia zile zilizochakaa,”alisema Profesa Luoga.
FEDHA BANDIA Ni UHUJUMU UCHUMI
Kuhusu kuwepo wa fedha bandia katika mzungumzo, Profesa Luoga alisema BoT kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, imekuwa ikifuatilia na tayari imekamata wahusika wa fedha bandia Arusha, Dar es Salaam na Kigoma.
“Watuhumiwa waliokamatwa wanashikiliwa na vyombo vya usalama na tayari wamefikishwa mahakamani. Kwa kushirikiana na vyomba vya usalama, Benki Kuu inaendelea kufuatilia wahalifu wengine wanaojihusisha na uhalifu huo,”alisema.
Alisema tayari wamekamata watu saba ambao wanatengeneza au wanazungusha fedha bandia na kwamba hilo ni kosa la uhujumu uchumi na atakayekutwa na Sh 500 ya bandia, adhabu yake itakuwa sawa na yule atayekutwa na Sh milioni 10 au zaidi.
“Ukikutwa na Sh 500 au 1,000 kosa lako ni lile lile la uhujumu uchumi na utaadhibiwa sawa sawa na yule atakayekutwa na Sh milioni 10 au zaidi,”alisema.
SEKTA YA KIBENKI
Alisema bado Tanzania iko nyuma katika matumizi ya huduma za kibenki, hivyo kusababisha malipo mengi kufanyika nje ya mfumo wa kibenki kitendo ambacho kinatoa mwanya kwa watu kutapeliwa na Serikali kukosa mapato.
Alisema hatua ya BoT kufunga maduka ya fedha za kigeni imeleta matokeo chanya kwani kwa sasa mabenki yanaweza kupata fedha za kigeni za kutosha kukidhi mahitaji yao bila kutegemea BoT.
“Hatua mbalimbali kama vile kuhakikisha kuna ukwasi wa kutosha kuwezesha shughuli za uchumi, usimamizi mzuri na kuwepo kwa biashara halali ya fedha za kigeni kumechangia katika kuongezeka kwa faidi kwa mabenki.
“Kuongezeka kwa mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi mfano kutoka wastani wa asilimia 2.8 mwaka 2017 kufikia asilimia 11.1 Desemba mwaka jana,”alisema.
HAZINA YA DHAHABU
Aidha alisema ni mpango wa Serikali na BoT kuanzisha hazina ya dhahabu ambapo jambo la kwanza wanaangalia dhahabu iliyochakatwa au kusafishwa kwa asilimia 99.9.
Alisema hazina hiyo itaanzishwa kutokana na sehemu ya akiba ya fedha za kigeni ambayo ni juu ya kiwango cha chini kinachohitajika.
AKIBA YA FEDHA ZA KIGENI
Alisema kufikia Desemba mwaka jana, kiwango cha fedha za kigeni kimekuwa cha kutosha kwa uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi sita ambayo ni zaidi ya kiwango cha chini kinachohitajika kwa miezi minne.
“Pamoja na Serikali kugharimia miradi ya kimikakati inayoendelea sasa, mwenendo wa kiwango cha fedha za kigeni umeendelea kuongezeka hasa baada ya kudhibiti mahitaji ya fedha za kigeni kwa kufungia maduka ambayo yalikuwa hayafuati taratibu za biashara hiyo.
“Thamani ya shilingi imeendelea kuwa tulivu, kufungwa kwa maduka ya fedha kumeimarisha sana utulivu huu kwani kabla ya hapo ilikuwa inacheza kutokana na mahitaji katika soko (demand) yasiyokuwa ya kweli,”alisema.
MFUMUKO WA BEI
Kuhusu mfumuko wa bei, profesa Luoga alisema umeendelea kuwa tulivu, chini ya lengo la asilimia 5 la nchi za Jumuiya ya Africa ya Mashariki (EAC).
“Mfano kwa Januari mwaka huu, ilikuwa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.7,”alisema.