27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Simbachawene atoa maagizo mapya kamatakamata bodaboda, wananchi

Mwandishi wetu-Dodoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amepiga marufuku operesheni za polisi kukamata wananchi, bodaboda bila kutoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya.

Simbachawene alisema hayo jana wakati akizungumza katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama cha Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma na baadaye kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya.

Alisema ukamataji usio na mpangilio hauna tija na unaweza kuvunja amani badala ya kujenga amani.

“Wananchi wanawalalamikia askari wetu sana kukamata bodaboda bila sababu, sio bodaboda tu hata kukamata kamata hovyo watu, ukamataji mwingine unakua kama kukomoana, hauna tija, hauleti amani, badala yake unasababisha amani itoweke.

 “Yaani msako fulani unatungwa hauna kichwa wala miguu, hauna maelekezo yoyote ya Mkuu wa Jeshi la Polisi au chombo, ni watu tu wanajitungia wanaondoka na pikipiki yao wamepakiana wanaenda kufanya operesheni ambayo haina utaratibu,” alisema Simbachawene.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama ni vya wananchi, na operesheni yoyote haipaswi kufanyika bila mkuu wa wilaya kupewa taarifa ambapo ndio utaratibu unapaswa kuwa hivyo.

Pia Simbachawene aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuifanya wilaya hiyo kuendelea kuwa na amani na utulivu na wananchi kuendelea kuwa na imani na viongozi hao.

“Endeleeni kuwa karibu na wananchi, kwa kusikiliza kero zao na pia kuzitatua, epukeni malalamiko ya hapa na pale yasiyokuwa ya lazima,” alisema Simbachawene.

Simbachawene aliewaomba viongozi wa wilaya hiyo kujipanga vizuri katika maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi, wananchi kupitia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na taasisi zote za utawala, mnapaswa kuwa na ushirikiano mkubwa ili kujenga msingi wa uchaguzi utakaokuwa wa amani na utulivu,” alisema Simbachawene.

Alisema mwaka wa uchaguzi haupaswi kuwa na vurugu, ni mwaka ambao unapaswa kuwa na utulivu kwasababu ni jambo zuri la kidemokrasia linafanyika.

“Rai yangu kwa wananchi, tunapaswa kujenga utulivu kuanzia sasa kuelekea uchaguzi mkuu, hatupaswi kuwa na vurugu, ni mwaka ambao amani na utulivu wa nchi unajengwa kuanzia sasa, mshikamano wa vyombo vyetu ndio msingi wa kujenga uchaguzi utakao kuwa wa huru na haki ambao utafanya mwaka huu,” alisema Simbachawene.  

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Jabir Shekimweri, alimshukuru waziri huyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yake.

Naye Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mpwapwa (OCD), Maulidi Manu, alisema ujio wa waziri huyo umewasaidia zaidi kwa kujipanga zaidi, na kufuata maagizo yote aliyoyatoa kwa Jeshi la Polisi wilayani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles