MOSCOW, URUSI
SERIKALI ya Urusi imetoa kaul dhidi ya matamshi ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki aliyesema kuwa nchi hiyo inaingilia vita nchini Libya na kueleza kuwa, matamshi hayo hayana ukweli wowote.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, alisema jana kuwa, matamshi ya Rais wa Uturuki kwamba Urusi imekuwa na ushiriki wa kiwango cha juu kabisa katika vita vya Libya si ya kweli.
Ofisa huyo wa Ikulu ya Rais nchini Urusi alieleza wazi kwamba, Rais Vladimir Putin hajatoa amri ya kutumwa vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo huko nchini Libya.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imeendelea kukosoa uingiliaji wa nchi za kigeni na misaada yao kwa wapigani wa jenerali muasi, Khalifa Haftar.
Mgogoro wa Libya ulichukua sura mpya Aprili mwaka jana baada ya kundi linalojiita jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na jenerali muasi, Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi makali kwa ajili ya kuuteka mji mkuu wa Libya Tripoli unaodhibitiwa na Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya.
Nchi za kiarabu, Saudi Arabia, Misri na baadhi ya madola ya Ulaya yamekuwa yakimuunga mkono jenerali Khalifa Haftar na hata kumpatia misaada ya hali na mali.
Uturuki nayo imekuwa ikiipatia misaada ya kijeshi Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa na jamii ya kimataifa licha ya vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo.