Nyemo Malecela -Kagera
MUUGUZI aliyetumbuliwa wakati wa kuondoa watumishi hewa mkoani Kagera, Dezber Solomon (49) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi wa darasa la sita, Alinda Reverian (14) baada ya kumfanyia jaribio la kumtoa mimba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bukoba, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februri 8, mwaka huu saa sita mchana katika eneo la Kilimani nyumbani kwa Vedastina Chreophas.
Kamanda Malimi alidai kuwa Alinda aliyefanyiwa jaribio la kutoa mimba kwa njia isiyokuwa halali na salama, alikuwa anasoma darasa la sita Shule ya Msingi Kilimani iliyoko Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera.
“Siku ya tukio marehemu alikwenda nyumbani kwa Solomon ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kibwenge kilichopo Halmashauri ya Bukoba, ambaye aliwahi kufanya kazi katika Zahanati ya Buzi iliyoko katika halmashauri hiyo.
“Lakini alifukuzwa kazi na Serikali katika zoezi la kuondoa watumishi hewa waliojipatia kazi kwa kutumia vyeti vya kughushi, ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa hana cheti cha kidato cha nne, lakini akaendelea kuhudumia wagonjwa mtaani bila kibali na kwa kificho,” alidai Kamanda Malimi.
Alisema marehemu alikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa ambako inadaiwa alipatiwa matibabu ya maumivu ya tumbo kitendo ambacho ndugu na jamaa wanashuku ndicho kilichosababisha kifo chake.
Kamanda Malimi alisema mtuhumiwa amekamatwa na anaendelea kuhojiwa na polisi wakati mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kagera.
“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo ni kutobolewa kwa mfuko wa uzazi na kuingiziwa madawa sumu katika jaribio la kutoa mimba,” alidai Kamanda Malimi.
Katika tukio lingine, Februari 9, mwaka huu saa tano usiku katika Mtaa wa Rwazi, Kata ya Kahororo, Manispaa ya Bukoba, Buberwa Mberwa (14) mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Kahororo alikutwa akiwa amejinyonga kwa kujitundika kwenye nondo ya dirisha kwa kutumia mkanda wa begi ambao alikuwa akiutumia kufunga suruali.
Alisema marehemu alikuwa anaishi na mama yake pekee baada ya baba yake kuwatelekeza na kusababisha hali yao ya maisha kuwa ngumu.
Inadaiwa kuwa marehemu aliwahi kuwa na tatizo la afya ya akili.
“Inaelezwa kwamba kabla ya tukio hilo, saa 12 jioni marehemu aliporejea nyumbani, aliwakuta watoto wa baba yake mdogo ambao ni Kakuru Laurent (8), mwanafunzi wa darasa la pili Kahororo na Kato Laurent (8), mwanafunzi wa shule hiyo wakichezea mkanda huo akawataka wampe mkanda wake wakamkatalia.
“Walipomuona kachukia waliamua kumpa mkanda wake na kuondoka kwenda kwao kutoka alipokutwa amejinyonga,” alisema Kamanda Malimi.