Andrew Msechu –Dar es Salaam
VIONGOZI wa nchi za Afrika Mashariki wameungana na maelfu ya Wakenya, kuaga mwili wa rais wa pili wa nchi hiyo, Daniel arap Moi, ambaye anatarajiwa kuzikwa leo.
Katika salamu za rambirambi walizozitoa wakati wa ibada maalumu ya misa ya wafu iliyofanyika Uwanja wa Nyayo, Nairobi nchini Kenya jana, viongozi hao walieleza namna walivyomfahamu Moi na kushirikiana naye.
MUSEVENI
Akitoa salamu zake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema kifo kwa binadamu ni lazima, lakini tofauti iliyopo ni kwamba umefariki baada ya kufanya nini.
“Kama ulifanya mambo hovyo basi tunakusahau, au tunakukumbuka kwa mabaya uliyoyafanya.
“Kwenye Biblia tunamkumbuka Pontio Pilato kwa kumnyonga Yesu. Kwa hiyo unaweza kukumbukwa kwa mabaya au kwa mazuri.
“Lakini hapa, hasa Afrika viongozi ni kama daktari. Kama daktari hawezi kugundua ugonjwa wa nchi, hawezi kutibu ugonjwa huo na nchi itakuwa kwenye matatizo.
“Kenya imekuwa na amani tangu uhuru, haijawahi kupata vita. Imewahi kupata misukosuko kidogo, lakini hiyo ilikuwa mchezo. Sisi tuliopata shida ndio tunajua shida ni nini.
“Kwa hiyo hii inamaanisha kwamba waganga wenu hapa, viongozi wenu waliweza kugundua ugonjwa wa nchi yenu na kuwapa dawa inayofaa, na mimi nimeshuhudia miaka yote mchango wa viongozi wa Kenya.
“Mzee Moi na Kenyatta walikuwa na dawa inayoweza kutibu shida za Kenya na za Afrika Mahariki,” alisema Museveni.
Alisema dawa ya kwanza ni uzalendo ndani ya Kenya na anakumbuka kwa waliokuwapo, kulikuwa na vyama vya Kadu na Kanu, ambavyo vilikuwa vyama vyenye misingi yake.
“Lakini 1964 Moi na waliokuwepo kwenye Kadu walijiunga na Kanu na kufanya chama kimoja, ikimaanisha walishagundua umuhimu wa umoja.
“Sifa ya pili Moi alikuwa na roho ya Afrika Mashariki na muda mwingi alikuwa anataka Shirikisho la Afrika Mashariki na hiyo si kisiasa tu, alikuwa anipenda Afrika Mashariki hadi kwenye hisia zake,” alisema Museveni.
KIKWETE
Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alisema alipokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Moi ambaye alimfahamu tangu alipokuwa shule, akisoma habari za Kenya kuhusu kudai uhuru wa nchi hiyo.
“Hata nilipokuwa Waziri wa Nishati na Madini, niliwahi kutumwa na Rais wangu Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi) kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Songosongo hadi Kenya na wazo lake ilikuwa ni tushirikiane katika kuhakikisha bomba lile linatusaidia kuwa na uhakika wa umeme na hatimaye hata kusafirisha gesi.
“Nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje pia nilishirikiana sana na wenzangu wa Kenya akiwemo marehemu Nicolas Biwott katika kurejesha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Rais Moi alikuwa kiongozi shupavu na aliwaongoza vizuri mawaziri na kushirikiana na marais wenzake, yaani Mwinyi na Museveni,” alisema Kikwete.
Alisema alijifunza mengi kuhusu namna ya kushirikiana na kuheshimu watu, hivyo katika kipindi hiki ambacho Wakenya wanapitia pagumu, anawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili wawe na subira na kuvuka salama katika kipindi hiki kigumu.
MKAPA
Katika salamu zake, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alisema Rais Dk. John Magufuli amewatuma marais wawili wastaafu, yaani yeye na Kikwete kwa makusudi kuthibitisha udugu na ushirikiano wa karibu uliopo baina ya nchi hizi mbili.
“Katika miaka 10 ya uongozi wangu, miaka saba nilifanya kazi na Rais Moi na alikuwa ‘mentor’ wangu katika utawala na uongozi,” alisema Mkapa.
Alisoma ujumbe wa Rais Magufuli ambao ulisema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Moi na kwa niaba ya Serikali na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatuma salamu zake za rambirambi kwa Serikali, familia na watu wa Kenya.
Alisema Moi alikuwa ni mzalendo na mwanamajumui wa Afrika (Africanist) na atakumbukwa kwa juhudi zake za kufufua EAC, kusimamia usalama wa kikanda na kusimamia masilahi ya Bara la Afrika katika uwanja wa kimataifa.
SALVA KIIR
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir alisema Moi alikuwa shujaa wa uhuru wa nchi hiyo na wanamkumbuka kuwa mtu muhimu wa amani na usalama katika kanda hii.
“Mwaka 2005 nilipowakilisha watu wa Sudan katika vikao vya amani ya Sudan kupitia SPLM, nilimsikia akisema anamtaka aliyekuwa rais wa Sudan kuwaacha watu wa Sudan Kusini wawe huru na hatimaye mwaka 2011 tulipata uhuru wetu.
“Sudan Kusini ya leo ni matokeo ya kazi yake nzuri na ataendelea kukumbukwa daima kwa juhudi zake za kupatikana kwa taifa hili,” alisema Kiir.
KAGAME
Rais wa Rwanda, Paul Kagame alisema wanaungana na watu wa Kenya, Rais Kenyatta na familia ya Moi kuomboleza msiba huu wa kitaifa.
Alisema anashukuru kwa kupewa nafasi hiyo kutoa rambirambi zake na kueleza machache muhimu kuwa wakati watu wa Kenya wakiomboleza, inakwenda mbali zaidi kwa watu wa Rwanda ambao pia wanaomboleza.
“Tunamshukuru Rais Kenyatta na tutaendelea kuwa pamoja wakati tukiendelea kumkumbuka kiongozi huyu mahiri wa Kenya, ambaye amesaidia Wakenya kuendelea,” alisema Kagame.