25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wachota posho bungeni

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

NA FREDY AZZAH, DODOMA

WAKATI viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakiendelea kusisitiza kuwa hawatarudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameanza kulipwa posho baada ya kurejea bungeni.  Wabunge hao ni John Shibuda na Letisia Nyerere.

Shibuda alifika bungeni juzi saa 5 asubuhi na kujiandikisha kwenye orodha ya wajumbe wa Bunge Maalumu, waliowasili tayari kuanza kujadili sura 15 zilizobaki za Rasimu ya Katiba. Leticia alifika kwenye meza ya kujiandikisha jana saa 6:00 mchana. Tofauti na wajumbe wengine, Leticia alipomaliza kujiandikisha alikimbia waandishi wa habari huku akikataa kupigwa picha.

“Msinipige picha, sitaki, mnajua ni kinyume na sheria kunipiga picha bila idhini yangu?” alisema bila mafanikio. Hata alivyotakiwa kuzungumzia ujio wake ilihali wenzake wamesusia Bunge hilo, alisema “no comment”. Baada ya kujiandikisha, maofisa wa Bunge walimwambia kuwa anaweza kuungana na wenzake kwenye kamati.

Shibuda, alifika kwenye viwanja vya Bunge na kujiandikisha, kisha akatoa udhuru kwa Katibu wa Bunge kuwa anaumwa, hivyo hataweza kuudhuria vikao. Katibu wa Bunge, Yahaya Hamis Hamad, alithibitisha kuwa Shibuda amejiandikisha na ameomba udhuru kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta,  kwamba hataweza kuingia bungeni kwa sababu ya kusumbuliwa na mguu.

“Mimi mwenyewe kweli nilimuona mguu wake umevimba na hata alikuwa hajavaa viatu vya kawaida, aliniomba nimtolee udhuru kwa mwenyekiti, kwamba hawezi kuingia bungeni kwa sababu mguu unamsumbua, lakini ukipona atajiunga na wenzake kwenye kamati,” alisema. Alipoulizwa kuhusu malipo kwa viongozi hao, alisema kwa kuwa wamejiandikisha na kuomba udhuru, watalipwa Sh. 230,000 za kujikimu, lakini posho ya Sh. 70,000 ya kukaa kwenye vikao hawatalipwa. “Nadhani Shibuda itakuwa alilipwa hata jana (juzi),” alisema.

Jumatatu ya Agosti 4, mwaka huu, Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwatuka (CUF), alifika kwenye viwanja vya Bunge na kujiandikisha kwenye orodha ya wajumbe waliofika kwa ajili ya awamu ya pili ya Bunge hilo linalotarajiwa kukaa siku 60. Juzi, Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (Chadema) alionekana ndani ya viwanja vya Bunge.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia ujio wake, alisema alifika kwa lengo la kuchukua gari lake alilokuwa ameliacha na si kuudhuria mkutano unaoendelea. Alisema amekuwa mwanamapinduzi kwa muda mrefu na kuwa hawezi kurejea kwenye Bunge linaloendelea kwa kuwa yeye ni mwana Ukawa damu.

Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliopo mjini hapa, walisema kuna baadhi ya wabunge na wajumbe wengine wa Ukawa wapo kwenye hoteli mbalimbali mjini hapa wakisubiri kusikia misimamo ya viongozi wao ili waingie kwenye vikao vinavyoendelea. Imeelezwa kuwa baadhi ya wajumbe hao, wanasubiri kuona baadhi ya wenzao wakiingia kwenye Bunge hilo ili na wao waingie.

“Watakuja tu hawa, si umeona ratiba kupiga kura kuko mwisho kabisa, lazima tu wanabanwa na njaa warudi, wengi tu wapo Dodoma wanasikilizia wakubwa wao walegeze kamba,” alisema mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo ambaye hakutaka kutajwa gazetini. Alisema amesikia kuna baadhi ya wajumbe wa Ukawa ambao wamejiandikisha, lakini hana uhakika na hilo.

Akizungumzia kuhusu hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa hajapata taarifa za wabunge wa chama chake walioingia kwenye Bunge hilo. Slaa alisema ikibainika kuna mbunge aliyekiuka agizo la chama la kuwazuia kutoshiriki vikao hivyo, atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama. “Mpaka sasa bado sijapata taarifa za uwepo wa wajumbe kutoka Chadema, ila ikithibitika tutachukua hatua kwa mujibu wa utaratibu wa chama kupitia vikao vya maamuzi,” alisema Dk. Slaa  Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles