25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mwamposa aachiwa kwa dhamana

Mwandishi Wetu -v Dar es Salaam

JESHI la Polisi limemwachia kwa dhamana Mtume Boniface Mwamposa (Buldoza) ambaye alikamatwa yeye na wenzake nane.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya kufanyika ibada ya kuaga miili ya watu 20 ambao walipoteza maisha wakati wakigombea kukanyaga mafuta ya upako Moshi mkoani Kilimanjaro.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ilieleza kuwa katika uchunguzi huo walikamatwa watu nane akiwepo Mwamposa na kuhojiwa kwa kina na baada ya kujiridhisha na yale yaliyokuwa yanahitajika kutoka kwao, wamepewa dhamana kwa mujibu wa sheria ili waendelee kuripoti wakati uchunguzi ukiendelea.

“Uchunguzi bado unaendelea na baada ya kukamilika yatakayobainika yatatolewa na mamlaka husika na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Hivyo kila mmoja anatakiwa awe na subira na uchunguzi unaofanywa na wataalamu, utakapokamilika mtajulishwa.

“Nimekuwa nikipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakiuliza maendeleo ya uchunguzi wa tukio la Watanzania wenzetu 20 waliopoteza maisha huko mkoani Kilimanjaro, baada ya kukanyagana kwenye hitimisho la kongamano la ibada ya maombi Februari 1, 2020 na hatma ya waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi.

“Kama ilivyokwishakuelezwa na viongozi mbalimbali na kwenye taarifa yangu kwenu ya Februari 3, 2020 hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ni kwamba baada ya tukio hilo Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro alituma timu ya maofisa wakiwepo wataalamu wa uchunguzi wa sayansi ya jinai kwenda kuungana na timu ya wataalamu kule Kilimanjaro katika uchunguzi.

“Hivyo kila mmoja anatakiwa awe na subira na uchunguzi unaofanywa na wataalamu, utakapokamilika mtajulishwa,” alisema Misime.

Alitoa taarifa hiyo jana baada ya taarifa iliyotolewa majuzi iliyoeleza kuwa Mwamposa alikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa Dar es Salaam, kwa madai ya kusababisha vifo vya watu 20 na wengine 16 kujeruhiwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kutokana na utelezi wa ‘mafuta ya upako’ aliyowaelekeza kuyakanyaga kwenye ibada ya maombezi.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Februari 2, na ilielezwa kuwa baada ya maafa hayo, mtume na nabii huyo aliondoka na kurejea Dar es Salaam, ambako aliendelea na ibada katika Viwanja vya Tanganyika Packers, ambapo ndipo anapoendeshea ibada zake kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema walimkamata Nabii Mwamposa Dar es Salaam, alipokuwa amekimbilia mara baada ya kutoroka mkoani Kilimanjaro kutokana na tukio la waumini wake kugombea kukanyaga mafuta ya upako na kusababisha vifo.

Alisema wanaendelea na upelelezi utakapokamilika wanatarajia kumpandisha kizimbani.

“Katika maeneo yale hakupatikana kirahisi, tulikuwa tuna taarifa kwamba atasafiri kwa ndege, sasa tulifuatilia tukaambiwa aliondoka na usafiri wa gari kwa muda mchache alioondoka tumefanikiwa kumkamata alfajiri jijini Dar es Salaam,” alisema Simbachawene.

Aliwataka wengine wote wanaofanya shughuli kama hizo au kusababisha mkusanyiko wahakikishe kwamba hawasemi maneno au kusababisha maneno yatakayosababisha msisimko kwa waumini au kwa wafuasi wao na hata kupoteza maisha kwa hiyo tuchukue tahadhari na hata watu wanatoka salama katika mikusanyiko.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya, sura Namba 337 na hasa kifungu cha 9 na cha 19, Waziri wa Mambo ya Ndani, ndiye anayesajili jumuiya hizi za kijamii lakini pia madhehebu ya dini na shughui zote za taasisi za watu binafsi.

“Hivyo jukumu la kuhakikisha kwamba amani inakuwepo katika taasisi hizo za kidini na hivyo ndiyo maana nimesema niseme na niwape pole sana familia hizi za watu 20 waliofariki na wale waliojeruhiwa.

“Lakini ni lazima kama Serikali tuchukue hatua stahiki kwa sababu inasikitisha watu kwamba una idadi kubwa ya watu umewakusanya mahali, mwenye jukumu la kuhakikisha usalama wao ni wewe uliyewakusanya hapo pamoja na jukumu la Serikali la kuhakikisha kwamba watu wanakuwa salama lakini kwa idadi kubwa ya watu watu wa namna,” alisema Simbachawene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles