25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jabali la siasa Kenya lang’oka

WaandishI Wetu

RAIS mstaafu wa Kenya, Daniel arap Moi, amefariki dunia jijini Nairobi, akiwa na umri wa miaka 95.

Akitangaza kifo chake jana asubuhi, Rais Uhuru Kenyatta alisema Moi ambaye alikuwa Rais wa pili wa Kenya, baada ya mwasisi wa taifa hilo, Jomo Kenyatta, alifariki dunia jana alfajiri.

Alisema mzee Moi (1924-2020) alifariki dunia Hospitali ya Nairobi ambako amekuwa akitibiwa mara kwa mara.

Msaidizi wa kibinafsi wa mzee Moi, Lee Njiru pia alithibitisha kuwa rais huyo wa pili aliyetawala Kenya kwa miaka 24 tangu 1978 hadi 2002 ameaga dunia.

Moi alikuwa rais wa Kenya kwa miaka 24 kabla ya kuacha madaraka mwaka 2002 baada ya Wakenya kumchagua kwa kura nyingi Mwai Kibaki.

ALILIWA KILA KONA

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Dk. John Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kifo cha rais huyo mstaafu.

Rais Magufuli aliandika: “Kwa niaba ya Serikali na Watanzania, nakupa pole Mhe. Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kuondokewa na Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi.

“Watanzania tutamkumbuka kwa uongozi wake mahiri, jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Kenya na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Rais Yoweri Museveni wa Uganda, pia kupitia akaunti yake ya Twitter aliandika: “Nimepokea kwa majonzi taarifa za kifo cha mzee Daniel arap Moi, rais wa zamani wa Kenya.

“Sina shaka kuwa Kenya, Afrika Mashariki na Bara la Afrika limepoteza kiongozi shupavu. Nilikutana kwa mara ya kwanza na mzee Moi mwaka 1979 baada ya kumwondoa madarakani dikteta Iddi Amin.”

Katika ujumbe mwingine, Museveni aliandika: “Alikuwa ni mtu muhimu Afrika Mashariki. Aliunga mkono Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushirikiano wake kwa nguvu zote. Yeye, mzee Hassan Mwinyi na mimi mwenyewe tulifufua EAC ambayo ilishakufa. Ninatuma rambirambi zangu kwa Rais Uhuru Kenyatta, familia ya Moi na Wakenya wote kwa msiba huu mzito.”

Mwanasiasa mkongwe nchini, Pius Msekwa, alisema Moi alijitahidi kuipeleka Kenya katika hatua ya juu ya maendeleo licha ya kukabiliwa na matatizo ya ukabila.

“Ni msiba mzito, kifo cha mtu yeyote kinasikitisha, lakini anapokufa kiongozi mkubwa wa nchi, tena wa miaka mingi, inaleta simanzi kwa wale aliokuwa anawaongoza na sisi tuliokuwa viongozi katika nchi zetu wakati mmoja na yeye.

“Tunamkumbuka tulivyokuwa tunafanya mawasiliano katika mambo mbalimbali, kwa hiyo ni huzuni kubwa, amejitahidi kuipeleka Kenya katika hatua ya juu zaidi ya maendeleo, alifanya vizuri kwa kadiri ya uwezo wake.

“Unajua Kenya kuna matatizo mengi ya ukabila, kwa hiyo kupata mwafaka juu ya jambo ni vigumu, lakini katika hali pamoja na matatizo hayo aliweza kuipeleka nchi akaifikisha hapo ilipo,” alisema Msekwa ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alisema Moi atakumbukwa kwa kuiunganisha upya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Ni msiba mkubwa Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla, Moi ni kati ya viongozi ambao walitumikia nchi zao kwa muda mrefu, pamoja na matatizo ambayo tulikuwa tunapata katika nchi zetu, lakini katika uongozi wake Kenya ilipiga hatua kubwa.

“Amekuwa mmoja wa viongozi ambao wameimarisha umoja katika nchi zetu, hasa baada ya kuvunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki, yeye ni mmoja wa watu waliofanya juhudi kuirudisha tena.

“Haikuwa kazi rahisi kwa hali ilivyokuwa, lakini alishirikiana na wenzake miaka 20 iliyopita tukapata jumuiya,” alisema Jaji Warioba.

Alisema pia Moi aliondoka madarakani kwa amani baada ya kumaliza muda wake tofauti na viongozi wa mataifa mengine ambao wamekuwa waking’ang’ania na kusababisha migogoro. 

“Ni kati ya viongozi ambao aliachia madaraka kwa njia halali na Kenya pamoja na matatizo yake imekuwa ni nchi ya amani,” alisema Jaji Warioba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabi, alisema Moi atakumbukwa kwa kujishusha na kuomba radhi kwa wale aliowakosea sambamba na kuwasamehe waliomkosea.

“Tumempoteza mwanasiasa nguli ambaye alikuwa kiongozi shupavu katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa sababu ya historia yake ya kupigania haki za Waafrika.

“Katika uongozi wake tunajua namna alivyokuwa anapigania haki za Waafrika kuhusu masuala ya kujitegemea, ushirikiano na mengine ya kijamii.

“Tunaona namna alivyokuja ‘ku–apologize’ (kuomba radhi) kwa wale aliowakosea katika utawala wake, akaomba asamehewe kwa sababu yeye ni binadamu na si malaika.

“Kwa hiyo kauli hiyo ni fundisho kwa viongozi wengine kwamba wasifanye mabaya na kama yapo wakumbuke kuomba radhi,” alisema Muhabi.

Profesa wa Historia na Taaluma za Maendeleo katika Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala, alisema Moi aliongoza vizuri Kenya kwa kufuata nyayo za Rais wa kwanza wa nchi hiyo, hayati Jomo Kenyata ambaye falsafa yake kubwa ilikuwa ni ya mfumo wa kibepari.

“Alijitahidi wakati wa utawala kwa sababu yeye ndiye alipokea kijiti kutoka kwa Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta.

“Aliongoza Kenya mpaka yalipokuja mageuzi ya siasa ya mfumo wa vyama vingi ndiyo aliachia ngazi,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema licha ya kufuata nyayo za Kenyatta, pia atakumbukwa kwa kuidhinisha mfumo wa vyama vingi vya siasa kutoka ule wa chama kimoja uliodumu kwa miaka mingi nchini humo.

“Kenya ilikuwa na mfumo wa vyama vingi kikatiba, lakini uhalisia ulikuwa mfumo wa chama kimoja tangu mwaka 1982.

“Mwaka 1991 aliidhinisha mfumo wa vyama vingi na aliunda kamati ya Chama cha Kanu kupata maoni ya wanachama kwa sababu kilikuwa ni kipindi cha harakati za kudai mfumo wa vyama vingi dunia nzima na uchaguzi wa kwanza kwa mfumo wa vyama vingi ulifanyika 1992,” alisema Profesa Mpangala.

Hata hivyo alisema dosari mojawapo katika utawala wa Moi ni tatizo la ukabila ambalo lilisababisha migogoro mikubwa na mauaji hasa wakati wa uchaguzi.

“Kenyatta alikuwa ni Mkikuyu na Moi alikuwa anatoka Rift Valley, lakini hakuweza kuondoa tatizo la ukabila Kenya. Ulipokuja mfumo wa vyama vingi ukabila ulijitokeza na kila chaguzi zilikuwa zina migogoro mikubwa na mauaji na tatizo liliibuka kwake (Rift Valley).

“Uchaguzi wa mwaka 1997, Rify Valley na Pwani kulikuwa na mapigano isipokuwa uchaguzi wa mwaka 2002 ambao ndiyo uliing’oa Kanu madarakani ulikuwa wa amani,” alisema Profesa Mpangala.

MOI NI NANI

Moi aliingia madarakani baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa Kenya, mzee Jomo Kenyatta.

Yeye alikuwa mwanasiasa aliyetaka kupendwa zaidi na wananchi kuliko alivyokuwa mtangulizi wake, Jomo Kenyatta, hata hivyo alishindwa kuvunjilia mbali utawala wa kiimla wa Jomo Kenyatta na badala yake yeye mwenyewe akajikuta katika hali ya kuwadhulumu wapinzani wake wa kisiasa.

Alibatizwa jina la “Profesa wa Siasa” kwa vile alivyoweza kukabiliana na wapinzani wake. Hata hivyo utawala wake ulimalizika na sifa mbaya kwa kuwa Serikali yake ilidumaza uchumi na ufisadi ukashamiri.

Moi alizaliwa Septemba 2, mwaka 1924, katika jamii ya wakulima katika kaunti ya Baringo, katikati magharibi mwa Kenya.

Jina lake la kwanza lilikuwa Toroitich arap (mwana wa) Moi, lakini baadaye akabatizwa katika Ukristo na kupewa jina la Daniel. Alipewa jina hilo la Wamishenari Wakristo akiwa mwanafunzi.

Moi alikuwa mmoja wa wanasiasa wachache mashuhuri waliofanikiwa, ambaye hakutoka katika mojawapo ya makabila mawili makubwa nchini Kenya – Wajaluo na Wakikuyu.

Alitoka jamii ndogo ya Tugen, mojawapo ya makundi yanayounganisha kabila kubwa la Wakalenjin.

Alianza kufanya kazi kama mwalimu mwaka wa 1945 katika shule ya African Government School na mwaka mmoja baadaye akiwa na umri wa miaka 22 akateuliwa kuwa mwalimu mkuu.

Baada ya kuhamishwa mara mbili alirudi Kapsabet mwaka 1954 akiendelea kushikilia cheo cha mwalimu mkuu, kazi ambayo aliifanya hadi mwaka 1957.

Hakushiriki kwa vyovyote vile katika harakati za vita vya Mau Mau dhidi ya wakoloni, lakini alipendelea kundi hilo ambapo alitaka sana Kenya kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.

Wakati wa mapambano hayo aliwapa makazi wanachama watano wa Mau Mau kwenye mojawapo ya mashamba yake kwa majuma kadhaa.

Machi 1957 Moi alikuwa mmoja wa watu weusi nane waliochaguliwa kuwa wanachama wa Bunge la Ukoloni kwa Kiingereza Legislative Council ambalo kwa kifupi lilifahamika kama LegCo.

Mapema mwaka 1960 alikuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa kuhudhuria mkutano katika Lancaster House jijini London, ambapo Katiba mpya iliandaliwa na kuwapa Waafrika viti vingi katika Bunge.

Mwaka 1961 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, na katika Baraza la Mawaziri la muungano wa vyama vya kisiasa vilivyoshirikisha Kanu (Kenya African National Union), Kadu (Kenya African Democratic Union – Chama cha Moi) baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.

Wakati huo alishiriki katika mikutano mingi iliyokuwa ikiandaa Kenya kwa ajili ya kukabidhiwa uhuru.

Lengo lake kwa wakati huu lilikuwa kuundwa kwa Serikali ya majimbo ambapo Serikali hizo ndogo zingelinda masilahi ya makundi ya wachache nchini Kenya.

Kenya baadaye ilipata uhuru mwaka 1963 na Jomo Kenyatta akawa Waziri Mkuu, naye Moi akateuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Kilimo katika muungano wa upinzani. Siasa za Kadu zilidorora kisha chama hicho kikavunjiliwa mbali.

Wengi wa viongozi wa Kadu, Moi akiwemo, walijiunga na chama tawala cha Kanu.

Moi alikuwa mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa Taifa la Kenya, Jomo Kenyatta.

Mwishoni mwa mwaka uliofuata, wakati Kenyatta alipotawazwa kuwa Rais, Moi aliapishwa kama waziri wa mambo ya ndani.

Hiki kilikuwa cheo muhimu kwa sababu yeye sasa alisimamia idara ya polisi na pia wajibu wake ulikuwa kudumisha amani na usalama wa kitaifa.

Akiwa bado anashikilia wizara hiyo, mwaka 1967 aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais na Naibu mwenyekiti wa chama cha wabunge wa Kanu.

Wakati akishikilia wizara hiyo mataifa mengi ya kigeni yalikiri kuwa Kenya lilikuwa mojawapo ya mataifa yaliyokuwa na wafungwa wachache sana wa kisiasa.

Ilikubalika pia kuwa hakukuwa na dhuluma na ukandamizaji kisiasa nchini humo kama ilivyokuwa katika mataifa mengine yaliyokuwa yamepata uhuru.

Wakati Kenyatta alipofariki Agosti mwaka 1978, Moi aliyekuwa makamu wa Rais alichukua wadhifa wa kaimu Rais.

Mara tu alipotwaa madaraka hayo, alisema kuwa ataendelea na uongozi wa Kenyatta ulioegemea uongozi wa mataifa ya Magharibi, angefuata nyayo.

Ilipofika Oktoba alichaguliwa kwa wingi wa kura kuongoza chama cha kisiasa cha pekee nchini Kenya wakati huo ambapo alichaguliwa pia kuwa Rais wa Pili wa Kenya.

Baada ya uchaguzi kufanywa, Novemba mwaka uliofuata alifanyia Serikali yake mabadiliko makubwa ambayo yalikuwa hayajashuhudiwa tangu Kenya kujinyakulia uhuru mwaka 1963.

Alifanya kila juhudi kuimarisha uwezo wa Rais ili anufaike zaidi kwa madaraka.

Wizara mpya kama vile za Mali ya Asili na Mazingira zilibuniwa na nyingine kama vile za Kilimo ziligawanywa.

Agosti 1982 kulitokea jaribio la mapinduzi, lakini lilizimwa na wanajeshi waaminifu kwake.

Baadaye mwezi huo Rais alivunjilia mbali kikosi cha Jeshi la Wanahewa, ambao wengi wao waliongoza jaribio hilo la mapinduzi.

Tukio hilo lilimpa nafasi Rais Moi kuimarisha madaraka yake kwa kuwatimua wote walioshiriki au kushukiwa kushiriki katika jaribio hilo la mapinduzi.

Imeandikwa na ANDREW MSECHU NA NORA DAMIAN

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles