28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Samatta awapigia magoti mashabiki Tanzania

Badi Mchomolo

MSHAMBULIAJI wa timu ya Aston Villa, Mbwana Samatta, amewataka mashabiki zake kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuwashambulia wachezaji wa timu hiyo.

Samatta ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ amejiunga na klabu hiyo wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea K.R.C Genk ya nchini Ubelgiji kwa kitita cha pauni milioni 10.

Baada ya mchezaji huyo kujiunga na Aston Villa, kurasa za mitandao ya kijamii ya klabu hiyo iliongezekana mashabiki kwa kiasi kikubwa ikidaiwa kuwa wengi wao ni Watanzania ambao wanamshabiki mchezaji huyo.

Mashabiki walianza kuandika maneno machafu mara baada ya mchezo wa kwanza wa mchezaji huyo akiitumikia Aston Villa dhidi ya Leicester City kwenye Kombe la Carabao hatua ya nusu fainali ambapo mchezaji huyo alitolewa kipindi cha pili na timu yake ikafanikiwa kushinda mabao 2-1 na kuingia fainali.

Katika mchezo huo Samatta hakufunga bao, lakini baadhi ya mashabiki waliamini angeweza kufunga bao endapo wachezaji wenzake wangempa pasi katika eneo la hatari.

Mashabiki walikwenda mbali zaidi wakimtaja nahodha wa timu hiyo Jack Grealish kuwa ni mchoyo na alikuwa anamnyima Samatta pasi za mabao.

Samatta alipata nafasi ya kuwa kwenye kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu England mwishoni mwa wiki iliopita dhidi ya Bournemouth na kufanikiwa kufungua ukurasa wake wa mabao huku timu yake ikifunga mabao 2-1.

Hata hivyo, mashabiki waliendelea kuwashambulia wachezaji wa Aston Villa kwa madai wanamnyima pasi Samatta. Mashabiki wanatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza katika kufikisha ujumbe wao jambo ambalo limemuibua Samatta na kuwaomba wasiendelee kufanya hivyo.

Kutokana na hali hiyo Samatta alitumia ukurasa wake wa Twitter kisha kuandika.

“Mashabiki wa soka Tanzania nafahamu kuwa mnanipenda kijana wenu na mnapenda nifanye vizuri katika timu yangu mpya, lakini nawaomba muache kutoa maneno ya kashfa au yenye malengo mabaya kwenye akaunti za timu au wachezaji, binafsi sifurahishwi,” alitwiti Samatta.

Mashabiki hawakuanzia kwenye michezo hiyo miwili, walianza tangu mchezaji huyo alipowasili mjini Birmingham kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ili kujiunga na kikosi hicho.

Baada ya kufanyiwa vipimo alikaa zaidi ya siku tatu kabla ya kutambulishwa, hivyo mashabiki wakaitumia mitandao hiyo kwa kuwashambulia Aston Villa hasa wakiwataka kuharakisha suala la utambulisho wa mchezaji huyo.

Samatta anaamini kitendo hicho kinaweza kumuharibia kwa wachezaji wenzake au viongozi kwa kuwa wanaweza kuyatafsiri maneno hayo ambayo hayana maana yoyote.

Samatta anatarajia kuiongoza timu hiyo katika safu ya ushambuliaji kwenye mchezo unaofuata wa Ligi Kuu England dhidi ya kikosi cha kocha Jose Mourinho, Tottenham. Februari 16, huku Aston Villa wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Huo ni mchezo mgumu kwa Aston Villa ambao wanahitaji ushindi katika kila mchezo ili kujihakikishia nafasi ya kutoshuka daraja. Kwa sasa wanashika nafasi ya 17 wakiwa na pointi 25 baada ya kucheza michezo 25.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles