FARAJA MASINDE– DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati, Dk. Merdad Kalemani, amesema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) halina mpango tena wa kutumia mitambo ya IPTL, Aggreko na Symbion katika kuzalisha umeme kwa kuwa ilikuwa ikisababisha shirika hilo kujiendesha kwa hasara ya Sh milioni 439 kwa mwaka.
Alisema, walipoondoa mitambo hiyo ya ufuaji umeme shirikahilo lilikuwa likiokoa karibu kila mwezi Sh bilioni 6.9 zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kuendeshea mitambo hiyo kupitia kununua mafuta mazito.
Dk. Kalemani aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akiainisha mafanikio ya Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne iliyopita ya Uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.
Alisema, awali Tanesco ilikuwa inanunua umeme kwa bei ya juu hatua ambayo ilikuwa ikichochea gharama za umeme kuongezeka kwa watumiaji, jambo ambalo serikali imelipiga marufuku.
“Hivyo, tumeondoa pia mitambo mikubwa ya IPTL uliokuwa na megawati 103, mtambo wa Aggreko uliokuwa na megawati 48 na Symbioni megawati 129 ambapo kwa kufanya hivyo tumeokoa fedha Sh bilioni 138, haya ni mafanikio makubwa ya utendazaji wa njia za kusambaza umeme.
“Kutokana na huduma hizo kupatikana hapa nchini, ikiwamo kuimarika kwa miundombinu na ukarabati uliofanyika, kupitia upya matumizi ya Shirika, tulibaini kuwa lilikuwa likipata hasara ya Sh milioni 439 kwa mwaka, hivyo kwasasa halina hasara kutokana na juhudi ziliofanyika.
“Hasara hizo zilikuwa zinatokana na kutumia mafuta mazito ya kuendeshea umeme wa IPTL wa kuzalisha umeme megawati 103, hivyo unanunua mafuta ya Sh bilioni moja unauza umeme unaotokana na fedha hiyo unapata Sh milioni 800, unapata hasara ya milioni 200 jambo ambalo lilikuwa likisababisha hasara kubwa, hivyo tumekataa kuendelea na utaratibu huo wa hasara,” alisema Dk. Kalemani.
Alisema baada ya kufanyika kwa uamuzi huo kumechochea sasa shirika hilo kuanza kujiendesha kwa faida kubwa hatua mbayo itachochea kusukuma zaidi maendeleo.
“Hatua hiyo sasa imefanya Shirika kujiendesha kwa faida hivyo kuchochea kutoa gawio kwa serikali la Sh bilioni 1.43 kwa mwaka wa fedha uliopita, lakini pia kama Rais Magufuli alivyotuelekeza kujisimamia shirika kwasasa halipati ruzuku kutoka serikalini badala yake linajiendesha lenyewe na kwa faida kubwa,” alisema.
Upatikanaji umeme nchini
Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme nchini, Dk. Kalemani alisema kuwa imekuwan ikiimarika siku hadi siku na kwamba kwa mwaka 2015 kulikuwa na megawati 1,038 katika gridi ya taifa huku mwaka huu ikifikia megawati 1,602.34 sawa na ongezeko la megawati zaidi ya 480.
“Hii yote imechangiwa na kuwapo kwa miradi ya Kinyerezi I na II ambayo imekuwa ni kichocheo cha ongezeko hili, hatua ambayo imechagia kuwapo kwa umeme wa kutosha, pia tumekarabati mitambo ya Kitadu, Kihansi na Mtera.
“Pia tumeimarisha miundombinu ya usafirishaji umeme nchini kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mikoa yote inaunganishwa kwenye gridi ya taifa, mfano njia ya kutoka Mbagara hadi Mtwara ambao ni umbali wa kilometa 512 za umeme wa Kilovolt 132, kwani mikoa ya kusini haikuwahi kuunganishwa na gridi ya taifa kwa miaka yote hivyo ni jambo la kujivunia,” alisema Dk. Kalemani.
UPATIKANAJI WA VIFAA
Alisema mwaka 2015 transfoma zilizokuwa zimefungwa nchini zilikuwa ni 12,200 na kwamba kwasasa zimefika 23.000 sawa na asilimia 100, hatua ambayo imesaidia kupatikana kwa umeme wa kutosha.
“Maeneo mengi kwasasa umeme haukatikin kutokana na kuboresha teransfoma na kuondoa zilizochoka, sawa na eneo la nguzo ambalo nalo limeimarika kwa kuwa sasa zinapatikana nchini hatua mbayo imeokoa fedha Sh bilioni 162 na hakuna upungufu wa nguzo.
“Hilo pia tumelifanya kwenye eneo la mita za luku ambapo hadi sasa tuna viwanda vitatu vinavyoweza kuzalisha mita zaidi ya milioni 2.5 ikilinganishwa na mahitaji yetu ambayo ni milioni 1.6.
“Hata Bwawa la Mtera maji yameongezeka na kufikia mita za ujazo zaidi ya 696.7 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa, hivyo hali ya umeme uliopo unatosha kwasasa na kunaziada ya megawati 280 hadi 300 kwa siku,” alisema Dk. Kalemani na kuwahimiza wakandarasi kusambaza umeme kwa wakati ili kuwaondoa wananchi gizani.
Alisema hadi kufikia Juni 31, mwakani vijiji vyote nchini vitakuwa vimeunganishwa na umeme na kuwa nchi ya kwanza kwa Afrika Mashariki kufikia hatua hiyo.
Aidha, aliwataka wawekezaji waonajenga vituo vya mafuta kuhakikisha kuwa katika kila vituo vitatu wanavyojenga kimoja kinakuwa kijijini ili kusaidia nguvu kazi ya taifa ambayo ni vijana kuendelea kufanya shughuli zao huko waliko pamoja na kuondoa tabia ya vijana kuuza mafuta kwenye chuoa za maji.
Kuhusu akiba ya mafuta, Dk. Kalemani alisema kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta yote ikiwa ni pamoja na mafuta ya Petroli, Dizeli, Ndege na mafuta ya taa.