Mwandishi Wetu- Kampala
TIMU ya Taifa ya wanawake walio na chini ya miaka 20, Tanzanite imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uganda, katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia, uliofanyika jana Uwanja wa KCCA jijini Kampala.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Januari 19 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tanzanite iliishinda pia mabao 2-1.
Tanzanite ambayo inafundishwa na kocha, Bakari Shime imesonga mbele na kuikaribia ndogo yake ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia ambazo zimepangwa kupigwa Agosti mwaka huu nchini Costa Rica.
Mabao ya Tanzanite jana yalifungwa na Diana Lucas na Opah Clement.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo Shime alisema anafurahi kuona kile anachokitoa kwa wachezaji wake wanakifanyia kazi na ushindi huo unazidi kumpa moyo nwa kuwafikisha mbali vijana wake.
“Ni kazi nzuri ambayo imekua ikionyeshwa na vijana wangu, wananipa moyo na kuipa nchi sifa kubwa kwa upande wa wanawake, tutazidi kupambana kuona tuinafika mbali zaidi katika mashindano haya”alisema Shime.