Theresia Gasper -Dar es salaam
UONGOZI wa Yanga umetangaza kuhairisha Mkutano Mkuu wa dharura wa klabu hiyo ambao awali ulipangwa kufanyika Februali 16, mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julias Nyerere, Dar es Salaam.
Badala yake , mkutano huo sasa utafanyika Mei mwaka huu katika tarehe ambayo itatangazwa baadaye.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alitaja sababu ya kuhairishe mkutano huo kuwa ni kupata muda zaidi wa kujipanga.
“Ni kweli tumehairisha mkutano kwa sababu ilikuwa ni kwa ajili ya kubadilisha mfumo kwa upande wa wanachama ila tumeona ni bora tupange kwa pamoja ikiwa na mabadiliko ya uendeshaji wa klabu,” alisema.
Alisema wanahitaji kujumuisha mambo mengi katika mkutano mkuu huo, tofauti na awali ambapo agenda kuu ilikuwa mabadiliko kwa upande wa uanachama.
Ajenda nyingine zilizotangawa awali za mkutano huo zilikuwa ni ufunguzi wa mkutano, kuthibitisha akidi ya mkutano, kupitisha ajenda ya mkutano, kuwasilisha na kuainisha mapendekezo ya katiba, kupigia kura mapendekezo ya marekebisho ya katiba na kufunga mkutano.