27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lapiga kura kumtimua Gavana Waititu Kenya

Nairobi, Kenya

BUNGE la Seneti la Kenya limepiga kura ya kumwondoa madarakani Gavana wa Jimbo la Kiambu, Ferdinand Waititu maarufu kama Babaya kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Katika hatua ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa nchini Kenya, maseneta 27 kati ya 38 waliopiga kura usiku wa kuamkia Alhamisi.

Wabunge hao waliidhinisha hoja ya kumwondoa madarakani Waititu iliyopitishwa na bunge la kaunti ya Kiambu mnamo Disemba mwaka 2019.

Safari ya kumwondoa madarakani Ferdinand Waititu ilianza mwaka jana katika kaunti yake ya Kiambu wakati madiwani walipopiga kura ya kutokuwa na imani naye.

Madiwani wa Jimbo la Kiambu walidai kuwa Waititu alijihusisha na ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka, ukiukaji wa katiba na sheria nyinginezo, mashtaka ambayo yaliidhinishwa na Seneti.

Inadaiwa kwamba alitumia ushawishi wake kujinufaisha kifedha, kutoa zabuni za mamilioni ya fedha kwa kampuni za jamaa zake kutoa hudumu katika kaunti ya Kiambu.

Mwaka 2019 Waititu, mke wake Susan Wangari Ndung’u na binti yao, Monica Njeri walishtakiwa kortini kwa kuchukua zabuni fedha za Kenya Shilingi milioni 588 (sawa na dola 6,000,000) bila ya kufuata sheria.

Hatua ya serikali ya Kiambu kuzipa kampuni zinazomilikiwa na watu wa familia ya Waititu zabuni inakwenda kinyume na sehemu ya 66 (8A) ya Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa za Umma 2015.

Sehemu hiyo inasema: “Mtu au jamaa za mtu wanapopewa zabuni katika asasi anayosimamia atakuwa, ametenda kosa kwa mujibu wa sheria ya ununuzi na uuzaji bidhaa.”

Ferdinand Waititu ni gavana wa kwanza kuondolewa na bunge la seneti nchini Kenya kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Kuondolewa kwake kumekuja wakati ambapo serikali inaonekana kuimarisha vita dhidi ya ufisadi ambao umekithiri hasa miongoni mwa maofisa wa serikali ya kitaifa na za majimbo.

Wachambuzi wanasema kwamba hatua ya bunge la seneti ya kumtimua Gavana Waititu inatuma ujumbe wa tahadhari kwa vigogo ambao wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

Mwanasheria ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, Daktari Alutalala Mukhwana anasema kutimuliwa kwa Waititu ni ishara kwamba vita dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma vimeanza kuzaa matunda.

“Sasa maofisa wa serikali, wabunge na hata magavana itabidi wawe waangalifu katika matumizi ya fedha za umma. Na hatua ya seneti pia itatoa changamoto kwa idara ya mahakama kuongeza kasi ya kushughulikia kikamilifu kesi za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi miongoni mwa maofisa wa serikali” anasema Dk. Alutalala Mukhwana.

Magavana wengine wanne wanakabiliwa na mashataka ya madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwao Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko kwa jina maarufu Sonko.

Rais Uhuru Kenyatta kila mara ameshtumu idara ya mahakama nchini Kenya kwa madai kwamba haisaidii utawala wake kupambana na ufisadi uliokolea serikalini.

Kwa upande mwingine, jaji mkuu wa kenya amelalamikia vikali kuhusu hatua ya serikali ya kupunguza bajeti dhidi ya idara ya mahakama, jambo ambalo anasema, linavuruga shughuli na usimamizi na utekelezwaji wa haki.

Pia, idara ya mahakama inanyoshea kidole kitengo cha usimamizi wa mashtaka ya umma kwa ushahidi hafifu dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi, jambo ambalo limesababisha kesi nyingi kutupiliwa mbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles