Mwandishi Wetu-Dodoma
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kuwa limefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 23.5 ambazo zilikuwa zikitumika kila mwaka kuendeshea mitambo ya umeme.
Pia katika kipindi cha miaka minne shirika hilo limeweza kupata megawati 400 za ziada ambazo awali hazikuwepo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dodoma kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema kuwa fedha hizo zilikuwa zinatumika katika uendeshaji wa mitambo ya kusukuma umeme katika vituo mbalimbali hapa nchini.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Mtwara, Tunduru, Namtumbo, Songea, Madaba, Ruvuma na Liwale ambavyo vyote hivyo awali vilikuwa vikitumia mafuta kupeleka umeme maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Tunashukuru sasa hivi tumefanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha tokea mwaka 2018, na tunaamini tutazidi kupiga hatua kwa hii miradi tunayoifanya,” alisema Dk. Mwinuka.
Alisema shirika hilo limeongeza ukusanyaji wa mapato hadi kufikia Sh trilioni 1.53. kutoka Sh trilioni 1.2 mwaka 2012/13.
Dk. Mwinuka alisema mafanikio mengine waliyoyapata ni kwenye ufuaji wa umeme, ununuzi, usafirishaji pamoja na eneo la uwekezaji.
Alisema kuacha kufua umeme kwa kutumia mafuta, kumetokana na uwekezaji ambao wameufanya ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta hiyo.
Mbali na hilo, alisema ili kutatua changamoto za umeme Dar es Salaam wamefanikiwa kuboresha kituo cha Ubungo cha kupooza umeme kutokana na kuzidiwa.
“Hivi karibuni tumeboresha kituo cha Ubungo, kutokana na mahitaji ya jijini kuwa makubwa na kusababisha kituo kuzidiwa na megawati 240, hii imesaidia kutatua tatizo la umeme,” alisema Dk. Mwinuka.
Alisema wamefanikiwa kufunga transfoma mpya ambayo ina wezo wa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali tofauti na ilivyokuwa awali.
Dk. Mwinuka alisema kuwa mwaka 2015 mita zilizofungwa ni 1,648,386 ambapo hadi kufikia mwaka jana mita zilizofungwa ni 2,700,682 sawa na ongezeko la mita 1,052,292 sawa na asilimia 63.84.
Alisema Mtwara kulikuwa na tatizo la umeme na wameweza kuongeza mitambo miwili ya gesi asilia yenye KV 4.
Dk. Mwinuka alisema katika kipindi cha miaka minne wameweza kupata megawati 400 za ziada ambazo awali hazikuwepo.
“Kwa ujumla kwa kipindi cha miaka minne tumeweza kupata megawati 400 za ziada ambazo hatukuwa nazo kabla ya 2015,” alisema Dk. Mwinuka.
Alitaja mafanikio mengine ni kushuka kwa gharama za umeme kuanzia mwaka 2016 katika maeneo ya malipo ya huduma pamoja na gharama za maombi.
“Ilikuwa ukitaka kuomba umeme ilikuwa lazima ulipie, hata gharama ya uniti moja iliteremshwa kutoka 2.4 hadi 1.5 kwa uniti na ilitegemea na mteja wa aina gani na hilo ni moja ya fanikio katika huduma yetu ya umeme,” alisema Dk. Mwinuka.