28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yazipiga jeki shule Simiyu vifaa vya Sh mil 10

Na DERICK MILTON – SIMIYU

BENKI ya NMB imetoa vifaa vya ujenzi katika Shule ya Msingi Sanungu iliyoko Kata ya Somanda na Shule ya Sekondari Ng’wang’wali, Kata ya Nyangokolwa, Halmashuari ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Vifaa hivyo zikiwamo meza na viti vya walimu pamoja na wanafunzi, mabati, misumari na mbao vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 10 vilikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga na viongozi wa halmashuari hiyo.

Katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika kwenye shule zote mbili jana, Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse, alisema NMB imekuwa benki kinara nchini kushiriki na wananchi katika shughuli za maendeleo.

Akitoa maelezo ya vifaa vilivyotolewa Shule ya Msingi Somanda, Magesse alisema kuwa vifaa hivyo ni pamoja na mabati 108, mbao pamoja na misumari vikiwa na thamani ya Sh milioni tano.

Alisema kuwa uongozi wa shule hiyo chini ya Diwani wa Kata, Robert Rweyo waliomba kusaidiwa vifaa hivyo kwa ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ambavyo vimejengwa na wananchi na vimefikia hatua ya kuezekwa.

“Baada ya kupokea maombi haya, kama benki tulifurahi kwani yalilenga katika vipaumbele vyetu ambavyo ni elimu pamoja na afya, kama benki tumekuwa tukitumia zaidi ya Sh bilioni moja kila mwaka kusaidia jamii katika shughuli za maendeleo,” alisema Magesse.

Kwa upande wa Shule ya Sekondari Ng’wang’wali, Magesse alisema benki hiyo imetoa meza 36 na viti 36 kwa wanafunzi, huku meza 10 na viti 10 vikiwa kwa walimu vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni tano.

Magesse alisema shule hiyo ya sekondari ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya meza za walimu pamoja na viti, hali ambayo ilikuwa ikiwasababisha kutotekeleza majukumu yao ya kufundisha kwa ufasaha.

“Tunatambua kama benki mchango huu ambao tumetoa leo utakuwa chachu kwa shule zote kufanya vizuri kwenye matokeo yake na kuinua kiwango cha elimu na tunahakikisha tutaendelea kuwasaidia wananchi ambao ndiyo wateja wetu,” alisema Magesse.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Nyangokolwa, Lukonge Nyankali, aliishukuru benki hiyo kwa mchango huo.

“Walimu wamekuwa wakitumia madawati ya wanafunzi kufanya kazi zao, hasa kusahihisha kazi za wanafunzi, lakini leo wamepata meza tunashukuru sana na watafanya kazi kwa bidii kwani wamepata vifaa vizuri vya kufanyia kazi zao,” alisema Nyakali.

Naye Diwani Kata ya Sima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashuari hiyo, Robert Rweyo aliishukuru benki hiyo huku akiahidi ujenzi huo kukamilika mapema. Akipokea vifaa hivyo kwa shule zote mbili, Mkuu wa Wilaya, Kiswaga aliipongeza NMB akisema imekuwa ni benki bora hapa nchini kwa kutoa mchango kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles