Opec yapongeza fedha za Tasaf kutekeleza miradi

0
581

Na CHRISTINA GAULUHANGA -ARUSHA

OFISA Uendeshaji Mkuu wa Mfuko wa Misaada kutoka nchi zinazozalisha na kusambaza mafuta duniani (Opec), Shoragim Shams, ameupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kwa kusimamia vema fedha za miradi zinazotolewa na mfuko huo.

Shams alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya elimu Shule ya Sekondari Oldonyowas, Kijiji cha Oldonyowas, Arusha.

Alisema utoaji fedha za miradi ni jambo moja, lakini utekelezaji ni jambo lingine ambalo Tasaf wamefanikisha kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Sisi tumetoa fedha kwa lengo la kusaidia jamii, lakini zisingeweza kusaidia chochote endapo kusingekuwapo usimamizi thabiti na wananchi wenyewe kujitolea nguvu kazi, kwahiyo nimetembelea na kushuhudia kilichofanyika ni kizuri na Opec tunaipongeza Tasaf na kuahidi kuendeleza kushirikiana nanyi katika awamu nyingine inayofuata,” alisema Shams.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, alisema mwakilishi huyo wa Opec amekuja kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo awamu inayomalizika kwa lengo la maandalizi ya awamu nyingine inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mwamanga alisema katika awamu inayomalizika mambo mengi yamefanyika kwa ufadhili wa wadau hao katika maeneo ya uboreshaji miundombinu ya elimu, afya, maji na barabara.

“Katika shule hii ya Sekondari ya Oldonyowas zaidi ya Sh milioni 470 zimetumika katika ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, mabweni na matundu ya vyoo fedha ambazo zimetolewa na Serikali kupitia Tasaf pamoja na Opec,” alisema Mwamanga.

Aliwapongeza wananchi kwa kujitoa katika nguvu kazi na kusisitiza miradi hiyo utekelezaji wake unahitaji ushirikiano na wananchi ili kuzalisha ajira za muda zitakazojitokeza.

Naye Diwani wa Kata ya Olturoto, Baraka Simon (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC, alisema kukamilika kwa ujenzi wa mabweni hayo kutaweza kubeba wasichana 96 na kuwaondolea changamoto za kutembea umbali mrefu wa kilometa 12 kufika shuleni hapo.

“Ni furaha kwetu, lakini tunaomba awamu ijayo mtufikirie kujenga hata madarasa ya kidato cha tano na sita ili wanafunzi wetu wakimaliza kidato cha nne wasihangaike kwenda mbali,” alisema Simon.

Pia, Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyowas, Geoffrey Ayo, alisema wametekeleza miradi sita ya kupunguza umasikini kupitia miradi hiyo ya Opec na Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here