DAMIAN MASYENENE – SHINYANGA
ZIKIWA zimebaki siku chache kufika tarehe ya mwisho ya uandikishaji wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole na kitambulisho cha taifa, wananchi mkoani Shinyanga wameomba Serikali iiwezeshe vifaa zaidi na vituo vya uandikishaji Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ili kurahisisha kazi hiyo.
Ombi hilo la wananchi limekuja kutokana na kile wanachokidai kuwa ni uwapo wa vituo vichache vya uandikishaji ambavyo havikidhi mahitaji na idadi ya watu pamoja na vifaa vichache, ikiwamo mashine na kompyuta visivyomudu idadi kubwa ya watu wanaojitokeza.
Wakizungumza na MTANZANIA katika kituo cha uandikishaji cha Nida Mkoa wa Shinyanga ambacho ni pekee kwa manispaa hiyo, Mamee Boniphace mkazi wa Mwasele na Esther Masanja walisema kwa nyakati tofauti kuwa wanatumia gharama kubwa kusafiri kufuata namba za Nida kutokana na kutegemea kituo hicho kimoja.
Kutokana na hilo, wameomba kurahisishiwa huduma kwa kutumia namba hizo katika simu za mkononi.
“Watu ni wengi, lakini kituo ni kimoja tu kwa wilaya nzima, nimekuja hapa tangu saa 3 asubuhi na sasa hivi ni saa 10 jioni sijala… watu wanachoka na kukata tamaa, mizunguko ni mingi sana mpaka ruhusa kazini watu wanatuchoka, naomba watuongezee muda, bado hautoshi,” alisema Mamea.
Kwa upande wake, Justine Meshack mkazi wa Kata ya Mwasele, Manispaa ya Shinyanga, alishauri Serikali iongeze vifaa viweze kukidhi mahitaji kwa siku chache zilizobaki (hadi Januari 20) kwani maeneo mengi yanakabiliwa na changamoto ya uchache wa vitendea kazi.
“Nimekuja kuchukua namba na leo ni safari ya tatu, mara ya kwanza niliambiwa nisubiri baada ya wiki tatu nilipokuja nikaambiwa nije baada ya wiki mbili, lakini ndiyo kama hivi tangu saa tatu asubuhi nimekaa tu hapa, hakuna kinachoendelea… mimi naona shida ni uchache wa mashine, ipo moja tu haikidhi mahitaji ya watu waliopo,” alisema Meshack.
Akizungumzia uandikishaji unavyokwenda huku akitolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali, Ofisa Msajili wa Nida Mkoa wa Shinyanga, Nathaniel Njau alisema wanakwenda vizuri na kwamba wanaojitokeza kwa sasa ni wale wanaokuja kujiandikisha kwa mara ya kwanza.
Njau alisema wale waliokuwa wameandikishwa awali wanaendelea kupata namba zao na pia kupitia ofisi za watendaji wa kata na kutumiwa ujumbe mfupi kwa njia ya simu za mkononi.
Alisema changamoto kubwa imekuwa kwa wananchi kusahau taarifa zao ama kujiandikisha mara mbili kwa taarifa tofauti.
Aliwasihi wananchi kujitokeza kujiandikisha kwani vitambulisho vya taifa vina manufaa lukuki na si kukariri tu kwamba ni kwa usajili wa laini za simu.
“Changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa, huduma zinaendelea, namba zote zilizotolewa katika mkoa wetu zimeshagawiwa kwa wananchi, kwa siku kituo chetu tunapokea wastani wa watu 300-400.
“Lakini mashine yetu ina uwezo wa kuandikisha watu 500 kwa siku, kwa hiyo bado tuna uwezo wa kukidhi mahitaji na tunazo kompyuta tatu za uandikishaji… changamoto ni wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe za mwisho, lakini watu waliopo wanatosheleza,” alisema Njau.
Usajili wa laini za simu za mkononi kwa njia ya alama za vidole na unatarajiwa kukoma Januari 20, mwaka huu ambapo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), itazima laini zote ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo huo.