28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Madaktari bingwa waokoa maisha Mloganzila

Aveline Kitomary -Dar es salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Profesa Lawrence Museru, amesema hospitali hiyo ina madaktari bingwa 52 hali inayowezesha kutoa huduma nzuri za matibabu na kupunguza idadi ya vifo kwa wagonjwa.

Ufafanuzi huo aliutoa jana Dar es Salaam, kujibu taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuongezeka kwa idadi ya vifo Mloganzila, hali inayosababishwa na watoa huduma kuwa ni madaktari wanafunzi.

Profesa Museru alisema kuwa madai hayo si ya kweli na watoa taarifa hiyo wana nia ovu iliyojificha.

“Moja ya sababu ambazo zimeelezwa na mtoa taarifa kwamba madaktari wanaotoa huduma ni wanafunzi waliopo katika majaribio si za kweli, tuna madaktari bingwa 52, madaktari wa kawaida 50 na kwa sasa kuna madaktari tarajali 53,” alisema Profesa Museru.

Alisema madaktari hao wanashirikiana na kutoa huduma na madaktari wengi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili – Upanga na wengine wawili wabobevu wenye hadhi ya uprofesa kutoka nchini Korea. 

“Hivyo sio kweli kwamba madaktari ambao wapo mafunzoni wanafanya kazi bila usimamizi, kwani hospitali imeweka utaratibu wa kila mgonjwa anayefika kupata huduma anaonwa na daktari bingwa kwa ajili ya maamuzi.

“Takwimu tulizonazo zinaonyesha kwamba wagonjwa wanaotibiwa Mloganzila wameongezeka katika makundi yote, wagonjwa wa nje wameongezeka kutoka 17,115 katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia 25,493 katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia 48.8.

“Wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa wameongezeka kutoka 1,459 katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba mwaka 2018 na kufikia wagonjwa 2,795 katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia 91.6.

“Wakati huo huo idadi ya vifo (mortality rate) ikipungua kutoka asilimia 14.9 iliyokuwepo katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba 2018 na kufikia asilimia 10.4 katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2019 kwa upande wa Mloganzila,” alisema Profesa Museru.

Akizungumzia upande wa Upanga, alisema takwimu zinaonyesha kwamba katika kipindi cha robo cha Julai hadi Septemba mwaka 2018 wagonjwa waliolazwa walikuwa ni 12,375 na kulitokea vifo 1,000 sawa na asilimia 8.1.

“Vilevile katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2019 MNH Upanga ililaza wagonjwa 17,230 na kati ya hao vifo vilikuwa 1,673 ambayo ni asilimia 9.7 (mortality rate), hivyo basi takwimu kati ya MNH-Mloganzila na MNH-Upanga za asilimia ya wagonjwa waliofariki hazitofautiani sana ambapo MNH-Upanga ni asilimia 9.7 wakati MNH-Mloganzila ni asilimia 10.4 katika robo ya Julai – Septemba, 2019,” alisema Museru.

Alisema malengo yao ni kuhakikisha huduma bora zitaendelea kupatikana, hivyo kuwataka Watanzania wenye jukumu la kuelimisha jamii kuzungumza na wataalamu ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles