25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Mhasibu Wizara ya Afya kizimbani kwa utakatishaji Sh bilioni 1.7

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MHASIBU Wizara ya Afya, Luis Lymo (54) na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Christian Social Services Commission, Peter Maduki (61), wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 280 yakiwamo ya wizi na kutakatisha Sh bilioni 1.7.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

Walisomewa mashtaka hayo na mawakili wa Serikali, Zakaria Ndaskoi akisaidiana na Genes Tesha.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 150 ya kughushi, 128 kuiwasilisha nyaraka za uongo, wizi shtaka mmoja na kutakatisha fedha shtaka moja.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya mwaka 2017 na 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika mashtaka hayo, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi hundi mbalimbali  na kuzisaini kwa jina la Upendo Mwingira bila ridhaa yake, huku wakijaribu kuonyesha kuwa mshtakiwa Luis Lymo alikuwa akilipwa fedha hizo kama kamisheni na Taasisi ya Christian Social Services Commission wakati si kweli.

Katika mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo, washtakiwa wanadaiwa kuwasilisha hundi mbalimbali walizoghushi katika Benki ya Standard Chartered.

Inadaiwa washtakiwa hao kwa nyakati tofauti waliandaa taarifa ya fedha ya uongo (bank statement), wakionyesha akaunti namba 01080002404200 iliyopo katika Benki ya Standard Chartered, NIC Life House ilikuwa na zaidi ya Sh bilioni 1.7 wakati wakijua ni uongo.

Katika shtaka la wizi, kati ya Machi 30 mwaka 2017 na Oktoba 2018 katika benki hiyo, washtakiwa wanadaiwa waliiba zaidi ya Sh bilioni moja mali ya Taasisi ya Christian Social Services Commission.

Kwa upande wa shtaka la utakatishaji fedha, washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha zaidi ya Sh bilioni moja wakati wakijua fedha hizo zilitokana na zao la kosa la kughushi.

Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Shtaka la utakatishaji wa fedha halina dhamana, hivyo washtakiwa walipelekwa rumande hadi Januari 20, kesi yao itakapotajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,695FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles