Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amemteua Mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa Katibu Mkuu mpya pamoja na manaibu wake wawili na Mjumbe wa Kamati Kuu mmoja.
Uteuzi huo umetangazwa leo Ijumaa Desemba 20 alfajiri katika uchaguzi wa chama hicho unaoendelea jijini Dar es Salaam baada ya kuridhiwa na Baraza Kuu la chama hicho ambapo Salum Mwalimu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa chama hicho, Benson Kigaila, kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara.
Wakati huo huo, baraza hilo pia limepokea na kuridhia jina la Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho baada ya kuteuliwa na kutangazwa na Mbowe.
Kwa ujumla viongozi wapya walioteuliwa katika uchaguzi huo kuanzia nafasi ya Mwenyekiti ni Freeman Mbowe ambaye ametetea nafasi yake hiyo, Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed.
Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu, John Heche, Sarah Katanga, Gibson Meseiyeki, Michael Mwaitenda, Patrick Ole Sosopi, Grace Kiwelu, Suzan Kiwanga, Yahya Omary na Zeud Mvano.