30.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waliomfuata Lowassa wakwama mabaraza Chadema

Na FARAJA MASINDE

-DAR ES SALAAM

WAKATI chaguzi za mabaraza ya Chadema zikiendelea, mpaka sasa baadhi ya watu waliohamia kwenye chama hicho na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, wameshindwa majaribio yao ya kutaka kuongoza mabaraza ya chama hicho.

 Chama hicho kikuu cha upinzani kinatarajia kufanya uchaguzi Mkuu wa mwenyekiti Desemba 18, ambapo Freeman Mbowe, ambaye anatarajiwa kuchuana na Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe, bado anapewa nafasi kubwa ya kushinda kuongoza Chadema kwa awamu ya nne.

Mpapa sasa chama hicho kimemaliza uchaguzi kwenye ngazi ya mikoa, kanda, Baraza la Wazee na Baraza la Vijana (Bavicha), huku Baraza la Wanawake (Bawacha), wakitarajia kufanya uchaguzi wao leo.

Jana Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alitangaza matokeo ya uchaguzi wa baraza la wazee ambapo Makongoro Mahanga, alianguka.

Mahanga ni kati ya viongozi mbalimbali walihakihama chama cha mapinduzi mwaka 2015 na Lowassa na kujiunga na Chadema.

Katika nafsi ya Katibu wa Baraza la Wazee, Rodrick Lutembeka alipata kura 113 na kumshinda Mahanga, aliyepata kura 26.

“Chama kimemchagua Lutembeka kuwa Katibu wa  Baraza la Wazee kwa kura 113 baada ya kumshinda mshindani wake, Dk. Milton Mahanga kwa kura 26,” alisema Makene.

Mahanga alikuwa Mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya  CCM kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 na baada ya jimbo hilo kugawanywa na kuzaliwa la Segerea ambako aliliongoza kuanzia mwaka 2010 mpaka 2015.

Hatahivyo licha ya Lowassa kutangaza kurejea CCM Machi mosi, mwaka huu, Dk. Makongoro aliendelea kusalia Chadema ambako alifanikiwa kuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala kabla ya kuomba nafasi hiyo ya katibu wa baraza la wazee ambayo ameangukia pua.

Mbali na Dk. Mahanga mwingine ni, Ali Hemed Mngwali ambaye alikuwa akiwania nafasi ya Katibu Mkuu Bavicha, aliyeambulia kura 13.

“Katika nafasi ambayo uchaguzi wake ulikuwa mzito basi ni hii ya Katibu Mkuu wa Bavicha, kwani ilikuwa na wagombea watano.

“Katika awamu ya kwanza, Gwamaka Mbughi alipata kura 14, Nusrat Hanje alipata kura 14, Noeli Shao alipata kura, Hemed Ali Mngwali alipata kura 13 na Titho Kitalika aliyepata kura 0.

“Baada ya kufanyika kwa raundi ya pili kwa ambayo ilihusisha watu waliopata alama za juu kwa mujibu wa katiba ya chadema, Gwamaka Mbughi alipata kura 19 na Nusrat Hanje alipata kura 23 na kutangazwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Bavicha,”alisema Makene. 

Hemedi alikuwa kiongozi wa kikundi cha 4U Movement ambacho kilikuwa kinamuunga mkono Lowassa ndani ya CCM na baadaye kuahama naye alipojiunga na Chandema Julai 28, 2015.

Kama ilivyo kwa Dk. Makongoro naye baada ya Lowassa kurejea CCM aliendelea kusalia Chadema akihudumu katika idara ya uenezi kabla ya kuwania nafasi ya ukatibu mkuu Bavicha.

Katika nafasi nyingine kwenye uchaguzi huo wa Chadema, nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara imeendelea kushikiliwa na Suzan Lyimo kwa awamu nyingine baada ya kupata kura 135 sawa na ushindi wa asilimia 100.

Alisema BAWACHA atapatikana baada ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anayetetea nafasi yake atakapopigiwa kura za ndiio na hapana.

Alisema katika nafasi ya Mwenyekiti Taifa wa Baraza la Wazee, mshindi ni, Hashim Jumma Issa, aliyepata kura 112 dhidi ya mshindani wake Hugho Kimaryo aliyepata kura 15.

Makene alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar mshindi ni, Iddrisa Mkila kwa kura 74 dhidi ya, Mwanamrisho Taratibu Abama aliyepata kura 64 na Naibu Katibu Bara mshindi ni, Hellen Kayanza, aliyepata kura 78 dhidi ya mshindani wake, Andrew Kimbombo, aliyepata kura 60.

Aidha, Naibu Katibu Zanzibar, mshindi ni Haji Kali Haji aliyepata kura 116 dhidi ya Hamad Mbarouk aliyepata kura 22 na Mwekahazina wa Baraza la Wazee akiwa ni Erasto Gwota.

Alisema kwa upande wa Baraza la Vijana (BAVICHA), Mwenyekiti ni John Pambalu ambaye pia ni diwani wa Butimba jijini Mwanza aliyepata kura 150.

Aidha, katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti  wa Baraza hilo mshindi ni Moza Mushi, Makamu Mwenyekiti Zanzibar mshindi akiwa ni Omar Othman Nassoro na Naibu Katibu Mkuu Bara mshindi akiwa ni Yohana Kaunya.

Kuhusu uchaguzi wa BAWACHA alisema utafanyika leo kwa nafasi mbalimbali huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikiwa na wagombea wanne ambao ni Hawa Subira Mwaifunga, Aisha Yusuf Luja, Mary Elias Nygabona na Marceline Stanslaus.

“Kwa wagombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar wagombea ni watatu ambao ni Maryam Salum Msabaha,Sharifa Suleiman Suleiman na Zeud Mvano Abdulahi huku nafasi ya Karibu Mkuu ikiwaniwa na Grace Tendega.

“Kwa wagombea wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara wako sita na kwa Naibu Karibu Mkuu Zanzibar wagombea ni wawili ambao ni Asya Mwadini Mohammed na Bahati Chumu Haji,” alisema Makene.

Kuhusu utaratibu za uchaguzi alisema Desemba 19, Baraza Kuu la Chama litapitisha Katibu Mkuu na Naibu Karibu wa Chama hicho.

Makene pia alisema kuwa kuhusu kurudiwa  kwa uchaguzi wa Kanda ya Pwani ni kweli utaratibu zitafanyika baada ya kukamilika kwa chaguzi za viongozi taifa wa  Chama hicho unaoendelea jijini Dar es Salaam. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles