Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Lipuli, inatarajiwa kukutana leo, kujadili ripoti ya benchi la ufundi ili kuanza mshakato wa kuimarisha kikosi hicho.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Haerman Haruna, tayari amekabidhi lipoti yake na kuwapa wachezaji mapumziko ya wiki mbili na watarejea kambini Desemba 10, mwaka huu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Lipuli FC, Ayoub Kihwelo, alithibitisha kupokea ripoti ya mwalimu na kusema watakaa kuanza kuipitia.
Alisema baada ya kukutana watatoa taarifa rasmi ni kitu gani kocha huyo anahitaji, pia kama ni suala la usajili wataanza haraka mchakato huo.
Kihwelo alisema timu yao imekuwa na mwenendo mzuri, lakini wanafahamu mapungufu haukosekani, wataangalia ripoti kisha watayafanyia marekebisho.
“Tunakaa kesho (leo), kupitia ripoti ya kocha wetu, amekabidhi mapema tu na sisi tunataka kuifanyia kazi haraka ili timu itakaporejea kambini kila kitu kiwe sawa,” alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Lipuli ipo nafasi ya saba na pointi 18, ikicheza mechi 12, imeshinda tano, sare tatu na kupoteza nne.