Anna Potinus
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyemaliza muda wake, Prof. Mussa Assad ameahidi kumpa ushiarikiano wowote atakaouhitaji CAG mpya, Charles Kichere kwani wao wanafahamiana kwa kipindi kirefu tangu akiwa anafundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 5, alipokuwa akimkabidhi Kichere ofisi ambapo amesema kuwa akihitaji kitu kutoka kwake au kutokana na ujuzi wake binafsi atakuwa tayari kumsaidia.
“Kichere nimefahamiana naye kwa muda mrefu sana sio mtu mgeni kwangu hivyo ninachoahidi ni kwamba akihitaji chochote kile kutoka kwangu binafsi au kutokana na ujuzi wangu wa miaka mitano nitampa, siku yoyote akipiga simu nitakuwepo kwaajili yake.
“Kichwani kwangu mimi ni mtu ambaye ninapenda nipande bamia nilisimamie liote liingie jikoni nile kwahiyo kwasababu hiyo katika miezi miwili iliyopita nilianza kuwekeza katika kilimo hivyo ni nachokifikiria sasa hivi nikae shambani kwangu na kupumzika kule lakini wakinihitaji watu wa mjini watanipigia simu nitakuja kufanya kazi zangu,” amesema Prof. Assad.
Kichere amechukua nafasi hiyo kuanzia jana Jumatatu Novemba 4, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.